NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
MKUU
wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, ameunga mkono wazo la wanaharakati
wa haki za binadamu Pemba, linaloelekea kutaka kupiga marufuku, wananchi
wakiwemo watu wenye ulemavu, la kuendeleza kuwa omba omba mitaani.
Mkuu huyo wa wilaya, aliyasema hayo leo Januari 31, 2023 ofisini kwake mjini
Chake chake, wakati akizungumza na kamati hiyo, iliyoongozwa na Mwenyikiti wake,
Tatu Abdalla Msellem, wakati ilipofika kuonana na Mkuu huyo wa wilaya, kwa
ajili ya kupata mwelekeo kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo.
Alisema, wazo la kamati hiyo ni zuri, maana hata wao kama
wilaya, linawaumiza kichwa, ingawa walikuwa wakifanya kwa kuwafuata mtu mmoja
mmoja, na kufanikiwa kiasi.
Alieleza kuwa, sasa kama imejitokeza kamati ya kupinga
jambo hilo, wilaya itatoa kila aina ya ushirikiano, ili kufanikisha zoezi hilo,
kwa haraka na umakini.
Mkuu huyo wa wilaya, alifahamisha kuwa, utamaduni na
silka ya wazanzibari sio kufanya omba omba kama kazi ya kila siku na hasa na
wengine kwa kisingizio cha ulemavu wao.
‘’Tunasaidiana pale ambapo mmoja wetu anashida kubwa,
lakini sio mtindo wa kuamka asubuhi na kuanza kuomba omba, kama ndio kazi ya
kila siku,’’alisisitiza.
Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya ya Chake chake, ameitaka
kamati hiyo kutumi busara, hekma, elimu na ushawishi wa hali ya juu, wakati
watakapolifanya zoezi hilo.
Wakati huo huo, Mkuu huyo wa wilaya ameitaka kamati hiyo
kukutana na masheha wa wilaya yake, ili kuliwasilisha wazo hilo, ili wakati utakapofika
iwe rahisi.
Mapema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Tatu Abdalla Msellem,
alisema kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, la kuondoa omba omba katika miji yote
ya Pemba, watakutana na wakuu wa wilaya husika, ili kupata baraka zao.
Alisema, awali jambo hilo walikutana na Idara ya watu
wenye ulemavu Pemba Januari, 27 mwaka huu, ili kupata mchango wao na kuunga
mkono zoezi hilo.
Mwenyekiti huyo alisema, kwa sasa jambo hilo halionekani
kubwa la kutisha, ikilinganishwa na miji mengine, lakini ndio maana wanataka
kuliondosha, kabla halijakuwa kubwa.
‘’Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, sisi hili jambo linatuumisha
kichwa, na ndio maana tukaona tukutane na wakuu wa wilaya zote za Pemba, ili
kupata baraka zao kabla ya kulindoa,’’alifafanua.
‘’Sisi tuanze haraka kulitekeleza zoezi la kuondoa omba
omba, iwe ni wale watu wenye ulemavu au wengine, kwani linachafua sifa na
heshima ya wazanzibari,’’alieleza.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mussa Seif Mussa,
alisema Baraza la taifa la watu wenye Ulemavu, limeshalibariki jambo hilo, na
sasa kazi iliyobakia, ni kuandaa mpango husika.
‘’Mmoja ya mpango husika, kwanza ni kuongeza wajumbe wa kamati
kutoka kwenye viongozi wa dini, kisha kuwafuatilia omba omba wote shehiani
mwao, ili iwe rahisi kukutana nao,’’alieleza.
Kamati hiyo, inaundwa na wajumbe kutoka Baraza la taifa
la watu wenye ulemavu, wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi wa habari,
jumuiaya ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar, viongozi wa dini na Idara ya
ustawi wa Jamii.
Mwisho
Comments
Post a Comment