Wadau wa haki za watoto hasa watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 10 wanahitaji kujadili na kuweka mpango mzuri wa kuwalinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili.
Taakwimu zilizotolewa hivi karibuni na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaonesha kuwa jumla ya watoto 1, 173 waliathirika na vitendo vya udhalilishaji na ukatili mwaka 2022.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo jumla ya matukio 883 (asilimia 75%) ambayo yaliripotiwa ni kwa watoto hao wenye umri kati ya miaka 11 hadi 17.
Kwa mukhtadha huo, TAMWA-ZNZ inaona kuna umuhimu mkubwa wa kulipa kipaumbele kundi hili na kuona ni matatizo gani yanayolikabili ili kutafuta muafaka wa tatizo.
Utafiti wa kihabari wa TAMWA ZNZ uligundua kuwa matatizo ya matumizi mabaya ya kimtandao kwa vijana wa kiume yanachochea kutaka kujihusisha na masuala ya ubakaji, wakati tamaa kwa watoto wa kike inachangia kujiingiza katika masuala hayo.
Asilimia 63 ya watu walilaumu vijana wa kiume kuangalia video na picha chafu ambao asilimia 18 ya watu walisema mtoto wa kike ana tamaa kubwa.
Katika hali zote hizo hawa ni watoto na wahitaji kulindwa ili waweze kupita vizuri kwa mafanikio katika kipindi chote cha mpito hasa kwa vile nchi na dunia inazungumzia kutokumuacha nje mtu yeyote katika maendeleo.
Aidha Sheria ya Mtoto No.6 ya 2011 imelenga kuimarisha ulinzi, matunzo na haki za watoto. Ni kinyume na sheria kufanya vitendo vya ukatili zidi ya watoto na ndio maana, sheria hii ilitoa ulinzi wa mtoto katika Nyanja zote kwa kuzingatia Zaidi umri usiopungua chini ya miaka 18, kama inavyoeleza katika kifungu namba 19 (1) (b) cha Sheria hiyo ambacho kinasema “kwa madhumuni ya Sheria hii, mtoto yuko katika mazingira magumu na anahitaji matunzo na ulinzi ikiwa mtoto huyo; anajihusisha na tabia ambayo ni, inaweza kuwa na madhara kwake au kwa mtu mwingine yeyote,...”
Hivyo ni vyema suluhisho litafutwe la kuwalinda na kutoa adhabu kali kwa wahalifu na siyo kurukia katika suluhisho la kutaka kupunguza umri wa ridhaa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu hivi sasa.
Moja kati ya suluhisho ni kupata ushahidi wa haraka haraka kabla watoto hao hawajageuza ushahidi wao kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo hofu ya visasi, pesa na ngono hivyo kufanya kesi kuwa ngumu kutoa maamuzi.
Kwa kuona hayo, TAMWA -ZNZ inawaasa wazazi, walezi, taasisi, Serikali na Jamii kwa ujumla kuwasaidia zaidi watoto katika makuzi yao, na sio kuwatupia lawama au kutaka kupunguza umri wa kuridhia.
Comments
Post a Comment