NA ZUHURA
JUMA, PEMBA:
WATU
wenye ulemavu kisiwani Pemba wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuweka
kitengo maalumu cha kuwapatia huduma, ili kuepuka usumbufu wanaoupata wakati
wanapofika kutaka huduma za matibabu.
Walisema kuwa, wameona kwamba kuna vitengo mbali mbali
vimewekwa ikiwemo vya Ukimwi, kitengo cha maradhi ya macho, viungo, kifua kikuu
na vyengine, ingawa wao hawajatengewa, jambo ambalo linawapa usumbufu wakati
wanapofika hospitali.
Walieleza kuwa, ipo haja kwa Wizara husika kuwawekea kitengo
chao maalumu ambacho kitakuwa kina mahitaji yote ya watu wenye ulemavu, ikiwemo
kuweka miundombinu imara ya ufikiaji, wakalimani pamoja na madaktari ambao
watakuwa wanajua lugha za alama.
Wakizungumza katika kongamano la Watu Wenye Ulemavu ambalo
liliwashirikisha wadau mbali mbali, walieleza kuwa wanapoifuata huduma ya afya
wanateseka sana, hivyo watakapowekewa kitengo chao wataondokana na usumbufu
ambao wanaupata.
āKitengo ni muhimu kwetu kwa sababu tutakuwa na āone stop
centerā yetu ambayo itakuwa na huduma mbali mbali zinazoendana na hali yetu
tuliyonayoā, walisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wenye ulemavu Pemba
(JUWAUZA), Hidaya Mjaka Ali alisema, changamoto kwenye huduma za afya bado
zipo, ikiwemo za ufikiwaji, ukosefu wa wakalimani pamoja na madaktari kutokujua
lugha za alama.
āTunakumbana na changamoto mbali mbali wakati wa kuitafuta
huduma ya Afya ikiwemo huduma ya ufikiaji, ukosefu wa wakalimani pamoja
madaktari kutokujua lugha za alama, hivyo tunapofika tunazubaa zubaaā, alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Pemba
(ZANAB) Suleiman Mansoor Suleiman alisema kuwa, wasiiona hawana wasimamizi wakati
wanapofika hospitalini au vituo vya afya, hivyo huzubaa tu na wakati mwengine
hurudi bila kupata huduma.
āTutakapowekewa kitengo ,tunapofika tutapatiwa huduma kwa
urahisi na haraka zaidi, kwani tunaamini kuwa kutakuwa na mambo yote ambayo
yanastahiki tuwe nayoā, alieleza.
Nae Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka MECP-Z Pemba, Haji Ali
Hamad alisema, wamekuwa wakifanya mikutano na makongamano mbali kwa lengo la
kuhakikisha kwamba changangamoto za watu wenye ulemavu zinatatuliwa na wanapata
huduma stahiki.
āMadrasa inafanya kila juhudi kuona kwamba watu wenye ulemavu
wanapata haki, fursa na huduma sawa na watu wengine, ili wasijisikie unyonge,
kwa sababu mpaka sasa bado wanaona wanatengwa na jamiiā, alisema Ofisa huyo.
Aliitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu na
badala yake wawape mashirikiano ili kuona kwamba wanapata haki zao za msingi na
huduma stahiki.
MWISHO.
Comments
Post a Comment