NA ZUHURA
JUMA, PEMBA:
ZAIDI ya
watu 300 kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Marekani, wanatarajiwa kushiriki katika
Kongamano la sita la Kiswahili la kimataifa, litakalofanyika Disemba 17 na 18 katika
Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari Afisa Mdhamini Wizara ya
Habari, Utamaduni, Vijana, Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mafamau alisema kuwa,
maandalizi ya Kongamano hilo yameshafikia asilimia 90.
Alisema kuwa, ni faraja kwa kisiwa cha Pemba, kufanyika
Kongamano hilo, kwani wananchi walio wengi, watanufaika kwa namna mbali mbali kutokana
na wageni watakaoingia pamoja sambamba na kujifunza mambo mbali mbali ya
Kiswahili na utamaduni.
‘’Kwa kweli tunaona fahari Kongamano hili kufanyika kisiwani
hapa, wageni wengi wataingia na kushiriki, hivyo wananchi watanufaika kwa namna
moja ama nyengine’’, alisema Mdhamini huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar
Saade Said Mbarouk alisema kuwa, mada mbali mbali zitawasilishwa katika
Kongamano hilo, ili kukuza na kukiimarisha Kiswahili ulimwenguni.
‘’Tunawaomba wananchi waendelee kujisajili ili kuweza
kushiriki na kikamilifu katika Kongamano hilo ambalo watajifunza na kujionea mambo
mbali mbali’’, alisema.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Kongamano hilo Amina Ali Khamis
alieleza kuwa, shabaha ya kufanya kongamano hilo ni kuhakikisha maendeleo ya
Kiswahili yanakuwemo katika sayansi na teknolojia.
‘’Shabaha yetu ni kuhakikisha Kiswahili kinatumika duniani
kote, kinasambaa, kiwe ni bidhaa na fursa, hivyo katika kongamano hilo tutakuwa
na maonyesho, utalii wa ndani na usiku wa mswahili’’, alisema Makamu huyo.
Alisema kuwa, ipo nafasi ya watu kushiriki katika Kongamano
hilo, ambapo mwananchi anatakiwa kuchangia shilingi 50,000 na mwananfunzi
anatakiwa kuchangia shilingi 30,000 kwa kila mmoja.
Nchi ambazo watu wake watashiriki katika Kongamano hilo la la sita na la kwanza kwa Pemba la kimataifa la Kiswahili ni Tanzania Bara na Visiwani, Kenya, Marekani, Comoro,
Uganda, Rwanda na Burundi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment