NA HAJI NASSOR, ZANZIBAR:::
MAKAMU wa Pili wa rais Zanzibar Hemed
Suleiman Abdallah, asubuhi ya leo Disemba 13, 2022 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi,
katika jukwaa la mwaka la pili la msaada wa kisheria Zanzibar.
Shughuli hiyo
inatarajiwa kufanyika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi mjini Unguja, na
tayari matayarisho ya shuguli hiyo, yameshakamilika kwa asilimia 100.
Kwa mujibu
wa taarifa kutoka kwa baadhi ya watendaji wa Idara ya Katiba na Msaada wa
Kisheria Zanzibar, walisema jambo jengine ambalo limeshamilika ni kupatikana
kwa ukumbi husika.
Afisa sheria
wa Idara hiyo Pemba Bakari Omar Ali, alisema wajumbe watarajiwa wa jukwaa hilo,
wakiwemo kutoka kisiwani Pemba tayari wameshawasili kisiwani Unguja.
Alisema
jukwaa hilo, ambalo litadumu kwa muda wa siku mbili, pamoja na mambo mengine,
litaangalia manufaa ya uwepo wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria kwa
wananchi wa Zanzibar.
Alisema,
aidha wajumbe hao waalikwa wakiwemo wasaidizi wa sheria, watoa msaada wa
kisheria, wanasheria, waendesha mashtaka, mahakimu, wanufaika wa msaada wa
kisheria, masheha na wanaharakati kutoka Unguja na Pemba, watajadili kwa
pamoja.
‘’Kupitia
jukwaa hili, kwa vile ndio pekee linalowakutanisha wadau mbali mbali, pia ni
nafasi kwao kujadili na kubuni mwarubaini wa upatikanaji wa haki,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Afisa huyo wa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria
Pemba, aliwaomba waalikwa waote kufika mapema ukumbini hapo leo hii.
Alisema kwa
vile mgeni rasmi anatarajiwa kuwahi, ni vyema kwa kila aliyepata mwaliko,
kuhakikisha anafika kwa wakati kwenye ukumbi huo, uliopo Chuo cha Utalii
Maruhubi.
Baadhi ya
tasisi zilizoalikwa ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu, Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar, TAMWA, vyuo vya
mafunzo, watu maarufu, waandishi wa habari na wasaidizi wa sheria.
Hili ni
jukwaa la pili la msaada wa kisheria kufanyika hapa Zanzibar, chini ya Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, ambapo moja na mambo mengine, ni kuwakutanisha
wa wadau sheria kujadili kwa pamoja.
Mwisho
Comments
Post a Comment