NA HAJI NASSOR, UNGUJA
MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed
Suleiman Abdullah, amewataka wasaidizi wa sheria na watoa msaada wa kisheria kuendelea
kufanya kazi zao kwa uweledi, na hasa kuelekeza nguvu zao, katika mapambano ya
udhalilishaji, rushwa na dawa za kulevya.
Alisema,
bado jamii inakabiliwa na changamoto hizo, hivyo ni wajibu wao kuendelea
kutumia weledi wao, ili wananchi waishi kwa salama, bila ya kuwa na changamoto
hizo.
Makamu huyo
wa Pili, ameyasema hayo leo Disemba 13, 2022 ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi
mjini Unguja, kwenye jukwaa la pili la msaada wa kisheria Zanzibar,
lililoandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar.
Alisema,
serikali inayoongozwa na Dk. Mwinyi inaelewa kazi inayofanywa na wasaidizi wa
sheria, hivyo lazima wazidishe kasi na juhudi za kuhakikisha wanaifikisha elimu
hiyo kwa jamii.
Makamu huyo
wa Pili alisema, serikali itaendelea kuwa karibu mno na Idara ya Katiba na
Msaada wa Kisheria, ili kuona wanafanikisha malengo yao, ya kuifikia jamii.
‘’Muelewe
kuwa kazi hii ya utoaji wa masaada wa kisheria ni kazi ya kujitolea, na malipo
yenu ni kwa Muumba zaidi, hivyo endeleeni kuwasaidia wananchi wanyonge, ili
wapate haki zao kisheria,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Makamu huyo wa Pili, alisema yuko tayari kuusaidia mfuko wa msaada wa
kisheria, mara utakapoanzishwa, ili kuhakikisha unasaidia kusukuma mbele utoaji
wa msaada wa kisheria.
‘’Mheshimiwa
Waziri, mimi naunga mkono uanzishwaji wa mfuko huo, na niko tayari hata mshahara wangu mmoja
kuweka, na naamini na wengine watasaidia,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Makamu huyo wa Pili ameipongeza Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Zanzibar, kwa juhudi zake za kuhakikisha, wanaielewesha jamii, wajibu na haki
zao kisheria.
‘’Juzi
nilitembelewa na mwananchi mmoja, ambae ni mnyonge na ameelezea kupata haki
zake, akisema waliomsaidia ni wasaidizi wa sheria, tena bila ya malipo,
hongereni kwa hili,’’alieleza.
Kwa upande
wake, Waziri wa Nchi Afisi ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar
Haroun Ali Suleiman, ameiagiza Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, kuifanyia
marekebisho sheria y msaada wa kisheria Zanzibar no 13 ya mwaka 2018.
‘’Ushauri wa
wenzetu wa tasisi ya LSF kuwa sasa sheria yetu tuifanyie marekebisho, ili
itambuwe uwepo wa mfuko wa maalum wa msaada wa kisheria, kama ilivyo kwa
wenzetu wa Tanzani bara kwenye sheria yao,’’alifafanua.
Hata hivyo
alisema, ni wazo zuri kuwa wasaidizi wa sheria wapatiwe ofisi ndani ya ofisi za
wilaya, ili waendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Akisoma
maazimio yatokanayo na jukwaa la kwanza, Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada
wa Kisheria, Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, amesema sasa wasaidizi wa sheria
wanashirikiana vyema na vyombo vya habari.
Alisema,
hata wakati wa shamra shamra za siku 16 za kupinga ukatili, wasaidizi wa
sheria, walivitumia vyombo vya habari kufikisha ujumbe wa kupambana na
unadhalilishaji.
Alieleza
kuwa, Idara pia imefanikiwa kuwaptia mafunzo ya kuwakumbushia sheria mpya,
wasaidizi wa sheria, ili waendane na kasi ya utoaji huduma.
Nae Afisa
Mtendaji Mkuu wa taasisi ya ‘LSF’ Lulu Mwanakilala amesema kutakuwa na mfuko wa
msaada wa kisheria, ambapo serikali na wadau, ndio wenye jukumu la kuutunisha.
‘’Kwa mfano
Tanzania bara, kwenye sheria yao jambo hilo limo, hivyo ni wakati wa Zanzibar,
kufanya marekebisho ya sheria msaada wa kisheria namba 13 ya mwaka 2018, ili
kuingiza kipengele hicho,’’alisema.
Hata hivyo
alisema, kwa mwaka wa fedha ujao, watazidisha kasi ya kushirikiana na Idara ya
Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar.
Aidha LSF
imeshafanya mazungumzo na wizara husika, ili kuona wasaidizi wa sheri,a
wanakuwa na ofisi kwenye majengo ya TAMISEMI, ili kupunguza gharamza kukodi.
Aidha
tunataka kuona kuwa, mahakama zinatenga ofisi za wasaidizi wa sheria, kwenye
vitengo jumuishi kama ilivyo kwa wenzao wa Tanzania bara.
‘’Tunaahidi
kuendelea kuwa bega kwa bega katika kuwajenga uwezo watoa huduma za msaada wa
kisheria, ili kutimiza matakwa ya wananchi, yanayoongezeka kwa kasi,’’alieleza
Naibu Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Omar Haji
Gora, alisema jukwaa hilo ni utekelezaji wa sera ya mwaka 2017 na sheria ya
msaada wa kisheria no 13 ya mwaka 2018.
Alieleza
kuwa, LSF imekuwa karibu mno na Idara ya Katiba, Msaada wa Kisheria, katika
kufanikisha majukumu yake hasa ya kuhakikisha, wananchi wanapata haki zao na
ufumbuzi wa mambo ya kisheria.
Katika
jukwaa hilo la siku mbili mada kadhaa zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa wa msaada wa kisheria kwa kwa watu wenye ulemvu, uimarishaji wa
vituo vya msaada wa kisheria, katika vyuo vikuu, saikolojia ya jamii na
upatikanaji wa msaada wa kisheria ambapo ujumbe wa mwaka huu ni ‘’Uimarishaji
wa Huduma Bora na endelevu za utoaji wa msaada wa kisheria Zanzibar ‘’.
Mwisho
Comments
Post a Comment