NA HAJI
NASSOR, PEMBA:::::
MAHAKAMA
kuu kanda ya Pemba, imesema itahakikisha sasa inawapatia stahiki zao zote
mashahidi wanaofika mahakamani, ikiwa ni pamoja na nauli, ili kusiwe na mkwamo
wa kesi hasa za udhalilishaji unaosababishwa na mashahidi.
Hayo yameelezwa leo Septemba 21, 2022 na Naibu Mrajisi mahakamu hiyo kisiwani Pemba Faraji
Shomari Juma, wakati akizungumza na waandishi wa habari mahamani Chake chake,
pembeni ya kikao kazi za kusukuma kesi, kilichofanyika mahakamani hapo.
Alisema, kwa sasa mahakama imeshajipanga vizuri, kuhakikisha mashahidi
wanaofika mahakamani, wanapatiwa stahiki zao zote, ikiwemo nauli na kuona
hakuna kesi inayokwama, kwa kukosa mashahidi.
Alieleza kuwa, kesi kadhaa zikiwemo za udhalilishaji wa wanawake na
watoto, zimekuwa zikikwama kutokana na mashahidi kutofika mahakamani, na kusema
ikiwa sababu ni kuogopa kukopwa nauli na mahakama, sasa hilo halipo tena.
‘’Ni kweli tumegundua kuwa, kesi nyingi zimekuwa zikifutwa ama
kuondolewa mahakamani, kutokana na mashahidi kutofika mahakamani, licha ya
kupelekewa hati za wito,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Naibu Mrajisi huyo wa mahakama kuu kanda ya
Pemba, alisema wamekuwa wakipokea kesi nyingi, ingawa mwisho wake, hulazimika
kuziondoa kutokana na kukosa mashahidi.
Kwa upande Wakili wa serikali Seif Mohamed Khamis, alisema wakati
umefika sasa, kwa sheria kuchukua mkondo wake, ikiwa watajitokeza mashahidi,
wanaokataa kutii wito wa mahakama.
Alieleza kuwa, licha ya juhudi zinazochukuliwa na vyombo vya sheria, kuwaelimisha wananchi katika kufika mahakamani kutoa ushahidi, ingawa bado juhudi hizo hazijazaa matunda.
‘’Njia ya kufanya, ili mashahidi wafike mahakamani, ni kuendelea
kuwaelimisha wananchi na kesi kuendeshwa kwa kasi, ili wanaohitajika mahakamani
wasiochoke,’’alieleza.
Kwa upande wake, Mkuu wa upelelezi wa Jeshi la Polisi wilaya ya Wete
Fakih Yussuf Mohamed, alisema changamoto bado ni kubwa kwa mashahidi, kutofika
mahakamani, licha ya kufikishiwa wito kutoka mahakamani.
‘’Jamii bado haijataka kusimamia na kutilia mkazo, suala la
upatikanaji wa haki, ndio maana imekuwa vigumu kufika mahakamani kutoa
ushahidi,’’alieleza.
Aidha alisema, inashangaaza kuona walalamikaji siku ya kwanza wanafika
kituo cha Polisi kwa hasira, kulalamikia jambo lililotokezea, ingawa baada ya
muda, hukataa kutoa ushirikiano.
Hakimu wa mahakama ya mkoa Chake chake Luciano Makoye Nyengo, alisema
inasikitisha kuona jalada la kesi lililoanzia Polisi na kisha kupitia ofisi ya
Mkurugenzi wa mashataka, ingawa kisha mashahidi hawaonekani mahakamani.
‘’Kesi inamiezi yake, ikifika bila ya mashahidi kufika mahakamani,
mahakama hutakiwa kuiondoa, kinchojitokeza lawama hizo hutupiwa mahakimu na
majaji,’’alieleza.
Mratibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za kulevya dawa
za kulevya Pemba Omar Juma Mbarouk, alisema mfumo wa mahakama wa kuwaita mashahidi
wote kwa siku kwa kesi moja, ni mzuri na unaweza kupunguza changamoto.
‘’Kesi za dawa za kulevya ni nzito kuzifuatilia na kuzigundua, sasa
tunapozileta mahakamani, lazima mahakimu na majaji wawe makini katika
kuziendesha,’’alieleza.
Mwisho
Comments
Post a Comment