NA HAJI
NASSSOR, PEMBA::::
JAMII ya
Zanzibar, imeshauriwa kuwapeleka hospitali haraka, ndugu na jamaa zao,
wanapowaona na dalili kadhaa ikiwa ni pamoja na kutokwa na jasho lisilo la
kawaida hata kwa msimu wa baridi, kwani hiyo ni moja ya dalili za kuugua kifua
kikuu.
Dalili nyingine za kifua kikuu zilizoanishwa ni kikohozi cha
wiki mbili zau zaidi, kutoa makohozi yaliyochanganyika na damu, kukonda na
kupungua uzito kusiko kwa kawaida pamoia na homa za mfululizo.
Hayo yameelezwa na mtaalamu kutoka kitengo shirikishi cha
maradhi ya ukoma, kifua kikuu na Ukimwi Zanzibar, Said Khamis Ahmada, wakati
akiwasilisha mada ya kifua kikuu, mbele ya waandishi wa habari, kwenye mkutano
uliofanyika leo Septemba 18, 2022, Maabara ya afya ya jamii Wawi Chake
chake Pemba.
Alisema jamii, haina njia mbadala wanapowagundua wapendwa wao
na moja ya kati ya dalili hizo au na nyingine, bali wawafikishe vituo vya afya
na hospitalini, ili kufanyiwa uchunguuzi wa afya zao.
Alieleza kuwa, maradhi ya ukoma yanatibika, ikiwa mtu
anapojihisi kuwa na mabadiliko mwilini mwake, na kukutana na muhudumu wa afya,
na kisha kuanza dozi mapema kwa wakati.
‘’Lazima jamii isithubutu kuwachelewesha ndugu na jamaa zao
kuwafikisha hospitalini, na kuanza kufanyiwa uchunguuzi na kisha kuanza dozi,
ikiwa hali imelazimika hivyo,’’alifafanua.
Hata hivyo alisema, ugonjwa kifua kikuu upo wa aina mbili kuu,
moja ukiwa ni ule unaoshambulia nje ya mapafu, ambao kwa kawaida, haumbukizi na
ule unaoshambulia ndani ya mapafu unaoambukiza.
Nae Mratibu wa Kikfua kikuu na Ukoma kanda wa Pemba dk. Hamad
Omar Hamad, alisema kwa idadi ya wananchi wa Zanzibar, kuwa na watu 7,524
wanaoishi na Virusi vya Uki,mwi ni kubwa mno.
‘’Utafiti uliofanywa na shirika la misaada ya Marakani UNAIDS
Globan HIV mwaka 2019, ulionesha watu milioni 38 wanaishi na VVU, na kati ya
hao milioni 25.4 wanatumia dawa za kupunguza mali ya VVU na watu milioni 1.7
waliambukizwa VVU mwaka 2019,’’alifafanua.
Hata hivyo alisema utafiti huo kwa Zanzibar, uligundua kuwa,
kuna asilimia 0.4 ya watu wanaoishi na VVU, tokea pale alipogundulika mgonjwa
wa mwanzo, hospitali ya Mnazi mmoja Unguja mwaka 1986.
Kuhusu ugonjwa wa Uviko19, aliitaka jamii, kuendelea kuchukua
tahadhari za maksudi, kwani ugonjwa unaosambaa kwa mfumo wa hewa, ni rahisi
kuupata.
‘’Waliogundulika na magonjwa mbali mbali wamekuwa wakipewa
majina kadhaa, yanayoonesha unyanyapaa na kurejesha nyuma mikakati ya
kutokomeza magonjwa hayo,’alieleza.
Akifungua mkutano huo Meneja Mpango wa Shirikishi wa magonjwa
ya Ukimwi, Kifua kikuu na Ukoma Pemba Khamis Hamad Khamis, alisema vyombo vya
habari ni nyenzo pana ya kutoa elimu ya kupambana na magonjwa hayo.
‘’Tafiti zinaonesha kuwa, hadi mwaka 2020 duniani kulikuwa na
watu milioni 10, waliopata ugonjwa wa kifua kikuu na kati yao, milioni 1.5 sawa
na watu wote wa Zanzibar (sensa 2012) waliripotiwa kufariki dunia,’’alifafanua.
Baadhi ya waandishi wa habari akiwemo Mchanga Haroub Shehe wa
Shiria la Utangazaji Zanzibar ZBC, na mwenzake kutoka Sauti ya Ist-qama Salim Ali
Msellem, walisema mikakati endelevu inahitajika ili kutokomeza magonjwa hayo.
Mwisho
Comments
Post a Comment