Mhariri mkongwe, mchapishaji na mkufunzi, Ndimara Tegambwage, ametunukiwa tuzo ya Mafanikio ya Maisha ya Uandishi wa Habari (LAJA) kwa mwaka 2022.
Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kama Mgeni Rasmi wa sherehe za Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2021 zilizofanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam alimkabdihi Ndimara Tuzo ya LAJA .
Pia alimkabidhi hundi ya mfano ya sh. milioni 10 kama zawadi ya LAJA.
Jina la Ndimara kama mshindi wa LAJA lilitangazwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye baada ya mtangazaji veterani Rose Haji kusoma wasifu wake.
Ndimara ana uzoefu mkubwa wa zaidi ya miaka 40 katika vyombo vya habari.
Miongoni mwa michango yake katika tasnia ya habari alikuwa mmojawapo wa waliochagiza kuanzishwa kwa Baraza la Habari la Tanzania (MCT) la wanahabari wenyewe na kuanzisha ofisi ya Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-Tan) .
Alivutiwa na uandishi wa habari tangu akiwa shuleni na alifanyakazi Idara ya Habari Maelezo na baadaye gazeti la Uhuru.
Miongoni mwa habari kubwa alizowahi kuandika ni pamoja na harakati katika kipindi kuelekea uhuru wa Zimbabwe ambayo ilikuwa ikiitwa Rhodesia ya Kusini..
Hapa nchini aliandika na kuibua masuala mazito ikiwa pamoja na habari za uhaba wa mahindi wakati yalikuwa yakioza kutokana na uhifadhi mbaya.
Ndimara alichapisha gazeti la Radi na pia vitabu kimojawapo ni Duka la Kaya.
Pia amekuwa mkufunzi kwa wanahabari.
Kabla ya kutangaza jina la Ndimara kwa tuzo ya LAJA, Nnauye alisema anamfahamu mtunukiwa tuzo hiyo kabla hata kupewa karatasi yenye jina lake. Alisema baada ya kusikia haya yote ,anamjua vizuri sasa kuliko awali.
Ndimara anakuwa mtu wa sita kupata tuzo hiyo, baada ya hayati Fili Karashani, mtangazaji nguli Hamza Kassongo, Mariam Hamdani, mwandishi mashuhuri na mwanasafu Jenerali Ulimwengu, na mtangazaji veterani Rose Haji. (CHANZO MCT)
Comments
Post a Comment