NA HAJI NASSOR, PEMBA
RAIS wa Baraza la Habari Tanzania MCT, Jaji
Mstaafu Bernad Luanda, amewataka wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa wanachama wa
baraza hilo, kutoa michango yao ya kina, ili kupata katiba mpya, ya baraza
hilo.
Aliyasema hayo leo Januari 8, 2026 wakati
akifungua mkutano mkuu huo, kwa njia ya kielektroniki ya ‘ZOOM’, uliowanganisha
wanachama kadhaa hai.
Alisema MCT inawategemea mno wanachama hao, katika
kulipeleka mbele baraza hilo, na kwa kuanzia ni lazima, kuwa na katiba
inayokwenda na wakati.
‘’Niwaombe sana wanachama nyinyi hai wa MCT, leo
kutoa maoni yenu, ambayo naamini, yatakuwa ndio dira ya kupata katiba mpya,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Rais huyo wa MCT aliwatakia
kheir ya mwaka mpya wanachama wake wote, na kuwataka kuutumia vyema, katika
kufanikisha malengo yao.
Akiwasilisha uchakataji wa maoni kuelekea katiba mpya
ya MCT, mjumbe wa sekretariet Mwanzo Lawrence Milinga, alisema moja ni kutaka
kuipa hadhi ya kipekee ofisi ya MCT iliyopo Zanzibar.
Eneo jingine ni kukuangalia uwezekano wa kuliwezesha
baraza hilo, kuendelea kujitegemea na kuacha mfumo wa kutegemea wafadhali, kama
hapo zamani.
Aidha Milinga, alisema sektretariet imeona kuwa, pia
kwenye katiba hiyo ya MCT, kuwapa nafasi wanachama ambao wanamadeni, wanaweza
kuomba upya uanachama, baada ya wajumbe kuangalia mwenendo wake hapo awali.
Katika hatua nyingine, alisema maoni mingine ambayo
yamependekezwa kwenye katiba hiyo ni, kuangalia uwezekano wa kulipandisha hadhi
baraza hilo.
Awali Katibu Mtendaji wa ‘MCT’ Ernest Sungura,
alisema mkutano huo kufanyika kwa njia ya zoom, ni mapendekezo ya wanachama,
kwa mkutano uliopita.
Hata hivyo, amewakumbusha wanachama ambao wana
madeni, kuhakikisha wanalipa ada zao, ili baraza hilo liendelee kufanya kazi
zake.
Nae Happiness Nkya mjumbe wa bodi ya MCT,
alipendekeza kuwa, ni vyema wakaguzi wa ndani wakawa karibu kiutendaji na
washughulikiaji wa fedha, ili iwe rahisi wakati wa ukaguzi.
Katika mkutano huo mkuu maalum, wanachama waliyapitisha
mapendekezo ya katiba na kuingizwa kwenye katiba kwa asilimia 92, ambayo ni
zaidi ya theluthi tatu ya idadi ya wanachama.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake, Baraka Sunga,
alisema ameyakubali kwa asilimua 100 mapendekezo hayo, na sasa kugeuka kuwa ni
vifungu ndani ya katiba ya MCT.
Katiba ya Baraza la Habari Tanzania MCT iliasisiwa
mwaka 1995, kabla ya kufanyiwa marekebisho mwaka 2016, na kuanza ukusanyaji wa
maoni ya marekebisho mingine kwa mwaka 2026.
Mwisho

Comments
Post a Comment