NA ZUHURA JUMA, PEMBA @@@@
MKAGUZI wa shehia ya Pandani Wilaya ya Wete, Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi amesema, katika kuwaunga mkono Marais kwenye suala la matumizi ya nishati safi ya kupikia, ameamua kutoa majiko ya gesi wananchi, ili kuwaondoshea usumbufu wanaoupata.
Alisema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia na kuwezesha upatikaji wa gesi kwa urahisi na kwa bei nafuu, hivyo katika kuliendeleza hilo, ameona ni vyema kuwaunga mkono marais hao kwa kuwasaidia wananchi kuwapatia Nlnishati hiyo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi majiko hayo kwa akimama wa kaya masikini kwenye shehia za Pandani, Mlindo na Mjanaza, Inspekta Khalfan alisema kuwa amewapatia majiko hayo ili waweze kutumia nishati safi ya kupikia ambayo itawarahisishia katika shughuli zao za kila siku.
"Matumizi ya kuni na mkaazi yana athari nyingi kwa mazingira, kiuchumi na hata nyinyi wenyewe kwa afya zenu, hivyo muendelee kutumia hii nishati safi ya kupikia, kwa ajili ya kuwarahisishia shughuli zenu pamoja na kuepuka madhara," alisema.
Aidha alisema kuwa, kila mmoja kwa nafasi yake ana jukumu la kuhimiza juu ya uhifadhi wa mazingira kwani iwapo yataharibiwa kila mmoja atakuwa ni muathirika, hivyo Jeshi la Polisi wakiwa wadau wa mazingira kupitia mradi wa 'mazingira salama' wameliona hilo na ndipo Inspekta huyo akaona Kuna haja ya kuweza kuwasaidia akinamama hao.
Inspekta Khalfan pia aliwataka wanufaika wa nishati hiyo kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao juu ya kuachana na matumizi ya kuni na mkaazi na badala yake watumie nishati ya gesi kwani ina manufaa mengi.
"Pia nawasisitiza mujipange kwa ajili ya kuendelea matumizi ya gesi hiyo pale tu itakapomalizika gesi ya mwanzo, hiyo ni kwa manufaa yenu zaidi," alisema Mkaguzi huyo.
Kwa upande wake sheha wa shehia ya Pandani Khamis Rashid Ali na sheha wa Mlindo Maryam Issa Omar walimpongeza Mkaguzi huyo kwa moyo wake wa kujitolea katika kuwasaidia wananchi wa shehia hizo ambazo anazisimamia.
"Tunashukuru sana kwa sababu anapita vijijini kwetu na kutafuta changamoto zilizopo, hivyo zile ambazo ana uwezo wa kuzitatua, hujitahidi kuzitafutia ufumbuzi unaofaa, tunamshukuru sana," walisema masheha hao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mara baada ya kukabidhiwa majiko hayo mwananchi Asya Hamad Haji alishukuru kupatiwa msaada huo wa majiko ya gesi na kuahidi kuendelea kujaza kila itakapomalizika, kwani tayari wamesharahisishiwa maisha.
MWISHO.
Comments
Post a Comment