NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘’WATU wenye ulemavu wanastahiki haki zote za
msingi za binaadamu, sawa na watu wingine, ikiwemo michezo na burudani,’’inaeleza
sheria yao.
Sheria hiyo nambari 8 ya mwaka 2022, ikazidi kufafanua kwenye
kifungu cha 28 (1) (f), kwamba kundi hilo linastahiki haki zote za msingi, bila
ya ubaguzi.
Tena uzuri zaidi kifungu cha 29 (1), kikamtamka kuwa,
Baraza la Taifa la Watu wenye ulemavu, katika kuiendea haki hiyo, litahakikisha
ufikiaji wa maeneo hayo.
Kikafafanua kuwa, lazima pawepo na miundombinu rafiki ya
kuyafikia majengo ama maeneo kwa watu wenye ulemevu, wanapoziendea haki zao
michezo na burudani.
Kifungu cha 30, kikasisitiza kuwa, kila mmoja anawajibu
wa kutekeleza, kulinda na kutetea haki za watu wenye ulemavu, kwa kutoa taarifa
za uvujifu wa haki hizo.
Eneo jingine sera ya maendeleo ya taifa ya watu wenye
ulemavu ya mwaka 2004, Ibara yake 3.15 ikazitaka nchi, kuhakikisha wanawekewa
utaratibu utakaohakikisha watu wenye ulemavu, wanashiriki kikamilifu, michezo
na burudani.
Sera, ikataka kuaandaliwe utaratibu utakaoshirikisha
vyama vya michezo na wadau wingine, kuhakikisha sehemu za michezo kwa watu
wenye ulemavu, zinakuwa mpango wa kuendeleza michezo kitaifa.
Mkataba wa kimataifa wa haki za watu ulemavu wa mwaka
2006, Ibara ya 30, ikazitaka nchi, zinachukua hatua kadhaa, ili kuhakikisha
watu wenye ulemavu, wanaushiriki sawa kwenye michezo.
Kwenye kifungu cha 30 (b) ukafafanua kuwa, kundi hilo
linaakuwa na fursa ya kuandaa, kuendeleza na kushiriki kwenye riadha na
burudani, mahsusi kwa ajili yao.
‘’Kuhakikisha kuwa,
kundi hilo linapata huduma sawa kutoka kwa wanaoandaa shughuli za michezo na burudani,
bila ya vikawazo,’’ulifafanua mkatana huo.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 20, kinatoa
kinga kwa uhuru wa watu kujikusanya na kujiunga, kupitia vikundi mbali mbali.
Hapa mikataba, sheria, kanuni, katiba na maandiko,
haijawabagua watu wenye ulemavu, kushiriki michezo na burudani.
HALI HALISI IKOJE?
Hidaya Mjaka Ali, kutoka Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar ‘UWZ’
Pemba, anasema bado ni kaa la moto, kwao kushirikishwa kwenye michezo.
Anasema, kuanzia viwanja, gharama, vifaa na ushajiishaji,
umekuwa haupo, kama ilivyo kwenye mikata na sheria ilivyoelekeza.
‘’Kwa sasa tunayosheria mpya ya watu wenye ulemavu ya mwaka
2022, lakini bado vifungu vinavyolazimisha sisi kushiriki michezo, havijatekelezwa,’’analalamikia.
Omar Shaibu Omar wa Wawi, mwenye ulemavu wa viungo,
anasema hakumbuki hata shindano moja la michezo, kwa ajili ya watu wenye ulemavu,
lililowahi kuandaliwa Pemba.
‘’Kwa hakika kwenye michezo sisi hatujatekelezewa hata
kidogo, na tunatamani sana kama mpira wa miguu tuwe na ligi yetu, lakini wapi,’’anasikitika.
Ali Ussi Hakim wa Mwambe mwenye ulemavu wa usikivu, anasema
vipaji vyao vinazidi kudidimizwa, maana hata timu za mitaani hawashirikishi.
‘’Nilikuwa na rafiki yangu alikuwa akicheza mpira vizuri,
lakini kwa vile alikuwa kiziwi, timu ya Mtambile ilimkataa, na kwa vile hakuna
ligi yetu maalum, aliachana na michezo,’’anasema.
Mohamed Haji Khamis wa Makoongwe Mkoani, anasema hakuna ligi iliyoandaliwa
na wizara ya michezo, iwe ya mpira wa miguu, mikono, kikapo, pete, kuogelea na
riadha, kwa ajili yao.
Massoud Khamis Haji wa Mchanga mdogo na Aisha Omar
Othmna, wanasema wanamebakia kuwaangalia timu za wenzao, kwao wakikosa haki hiyo.
Bahati Khamis Haji, anasema kwa mara ya mwisho alishiriki
kwenye michezo ya kuruka juu, Disemba 3, mwaka 2020 kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya
watu wenye ulemavu Wete.
‘Kwa hakika sheria na mikataba haijatekelezwa kwenye
michezo, imekuwa maadhimisho hadi sherehe, ndio pingine tunaweza kuigusa michezo,’’analalamika.
ZFF
Khamis Hamad, Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar 'ZFF' ofisi ya Pemba, anakiri kuwa, hakujawahi kuandaliwa ligi ya mpira wa miguu wala
michezo mingine, kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Anasema, hilo linachangiwa na mambo kadhaa, ikiwemo
miundombinu ya viwanja kwao sio rafiki, mifumo ya mpira wa miguu kwa Pemba,
bado ni changamoto.
‘’Huwa nasikia tu huko Tanzania bara, ipo timu ya mpira
wa miguu ya watu wenye ulemavu, na imefanya vizuri, lakini kwa Pemba bado
sana,’’anasema.
JUMUIAYA ZA WATU WENYE ULEMAVU
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wasioona Zanzibar ‘ZANAB’ Ofisi ya
Pemba Suleiman Mansour, anasema watu wa kundi lao, bado halijazingatiwa kwenye
michezo.
‘’Inawezekana kwa sababu anaeshughulikia michezo hana
ulemavu, na ndio maana hata sisi wenye ulemavu hautuna ligi ya michezo wowote,’’anasema.
Maratibu wa Baraza la Taifa la Watu wenye ulemavu Pemba Mashavu Juma Mabrouk, anasema lazima jitahada za kupaza sauti zifanywe, ili kundi la watu wenye ulemavu, lishirikishwe michezo.
‘’Tunataka michezo jumuishwi, viwanja jumuishi, ili kusiwe na mtu kwa sababu ya ulemavu wake, anakosa kushiriki michezo, hii itakuwa sio sahihi,’’analalamika.
WIZARA INAYOSHUGHULIKIA WATU WENYE ULEMAVU INAFANYA
NINI?
Aliyekuwa Waziri wa Afisi ya Makamu wa Kwanza Harusi Said
Suleiman, anasema kwa mwaka 2024/2025, waliandaa bonanza la michezo kwa watoto 100
wenye ulemavu na wasiokuwa na ulemavu, wakiwemo wanawake 51 na wanaume 49.
Anasema ilikuwa ni sehemu ya shamrashamra za kilele cha
maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani Disemba 3.
Akafafanua kuwa, kwenye kilele cha siku hiyo, michezo
kadhaa ilifanyika, ukiwemo wa kuruka kamba, mbio za magunia, kuvuta kamba,
kukalia viti na mchezo wa kuvuka vikwazo.
Eneo jingine ilifahamika
kuwa, hakuna shabaha ya moja kwa moja, inayozungumzia uimarishaji wa michezo,
kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kati ya shabaha kadhaa.
MITANDAO YA KIJAMII IMERIPOTI NINI?
Disemba
2021, blog ya Idara ya Habari Maelezo ya Tanzania bara, imeripoti, aliyekuuwa
waziri wa Michezo, Innocent Bashungwa, aliwaongoza watanzania kuishangilia timu
ya Tanzania ‘Tembo Warriors’ baada ya kufuzu nusu fainali ya soka ya bara la
Afrika, kwa wenye ulemavu ‘CANAF’.
Hivyo,
kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo huo yaliyofanyika Uturuki
mwaka 2022, ni baada ya kuichapa timu ya Cameroon mabao 5-0.
Tena timu hiyo baada ya kuingia kwenye michuano hiyo, ilipata
ushindi wake wa kwanza, kwa kuifunga Uzbekistan mabao 2-0.
Nayo Dost Media,
iliripoti kuwa, Emmanuel Mrefu kijana mtanzania mwenye ulemavu wa viungo, anacheza
soka la kulipwa kwa sasa.
Kulingana
na kituo cha kudhibiti magonjwa, mmoja kati ya watu wazima wanne wa Marekani,
wana ulemavu unaoathiri, shughuli kuu za maisha yao.
Kwa Tanzania sensa ya
mwaka 2022 imebaini asilimia 11.2 ya watanzania ni walemavu na wanaohitaji mahitaji
muhimu, ili waweze kuendesha maisha yao.
NINI ATHARI YAKE?
Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Watu weye ulemavu
Zanzibar Ussi Salim Debe, amenukuliwa akisema, ni kukosa kuwaendeleza watu wenye ulemavu.
‘’Michezo ni afya, na wakiwanayo watu wenye ulemavu
hupunguza ukakasi na ufinyu wa kiakili na mwili, na wakiiokosa huzidi kudumaa,’’anasema.
Khamis Hamad kutoka ‘ZFF’ anasema, ni kuwanyima haki zao
za kushiriki michezo, kama walivyo watu wingine.
NINI KIFANYIKE?
Maulid Ali Hamad mwenye ulemavu wa Viungo, anasema ni
kutekelezwa kwa sheria yao, ambayo inalazimisha michezo kama walivyo makundi
mingine.
Aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar
Tabia Maulid Mwita, akayomba mashirika kuungana na serikali, katika kuanzisha ligi
maalum kwa watu wenye ulemavu.
Mwanaharakati wa haki za watu wenye ulemavu Khalfan Amour
Mohamed, anasema ni kuhakikisha, wizara inayosimamia michezo, inaweka bajeti
maalumm kwa ajili ya kundi hilo.
Mwisho



Comments
Post a Comment