NA
MOZA SHAABAN, PEMBA
DUNIA
inapaswa ielewe kuwa, watu wenye ulemavu ni sawa na watu wingine katika jamii.
Wana haki ya
kunufaika na kupata haki zote za msingi ikiwemo ya afya.
Haki ya afya kwa watu wenye ulemavu
imetamkwa na kuelezwa kwenye sera na sheria za kimataifa, kikanda na kitaifa.
Hapa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za watu wenye
ulemavu wa mwaka 2006, ibara ya 25, imesisitiza watu wenye ulemavu wana haki ya
kupata huduma za afya bila ubaguzi.
Huku Sheria ya Watu wenye Ulemavu ya
Zanzibar nambari 8 ya mwaka 2022 nayo kwenye kifungu cha 28, kikisisitiza watu
wenye ulemavu wanastahiki kupata haki zote za msingi ikiwemo ya afya.
“Watu wenye ulemavu wanastahiki kupata huduma
za afya kama matibabu, matengenezo na marekebisho yanayohusiana na ulemavu,” kinafafanua
kifungu hicho.
Hii inaonyesha, jinsi gani ulimwengu umewazingatia
watu wenye ulemavu katika upatikanaji wa
haki zote za msingi ambao ndio haki za kibinaadamu.
Kwani watu wenye ulemavu ni kundi kubwa na
muhimu, ambalo halipaswi kudharauliwa kwa namna yeyote.
Izingatiwe kwamba matokeo ya sensa ya watu na
makaazi ya mwaka 2022, yameweka wazi kua asilimia 11.4 ya wazanzibari wote ni
wenye ulemavu.
Kwa muktadha huu wanastahili kupata haki
zote za msingi ikiwemo huduma za afya, kama ilivyoainishwa.
Na haya yote yanaweza kufikiwa iwapo kila
aina ya ulemavu itazingatiwa kwa kuwekewa namana bora ya kuzifikia na kuzipata
huduma za afya.
WATU WENYE ULEMAVU WANASEMAJE?
Mmoja wa watu wenye ulemavu wa viungo Said
Saleh Sultan wa Mtambile anasema, miundombinu wezeshi ya ufikiaji huduma iliopo, ndio ujumuishi wao.
Anasema asilimia kubwa ya vituo vya Afya
vinawawezesha wenye ulemavu wa viungo kuzifikia huduma, bila au wakiwa na viti
mwendo.
Rehema Juma wa Kukuu Kangaani Mkoani, mwenye
ulemavu wa uoni anasema, wamekua wakipata kipaumbele kupata huduma katika vituo vya afya
na hospitalini.
Anaona jambo hilo ni hatua muhimu, katika
ujumuishi wao kwenye haki hiyo ya msingi ya kiafya.
“Tunapofika vituo vya afya au hospitali
tunapewa kipaumbele, ni utaratibu mzuri kwetu, kwani unahakikisha upatikanaji
wa haki zetu,”anaeleza.
Pamoja na jitihada hizi bado changamoto
zipo kwa watu wenye ulemavu wa uziwi, kutokana na kutokuwepo kwa wataalamu wa
lugha ya alama.
Wenyewe wanasema, wasisahauliwe
wazingatiwe na watiliwe maanani kama ilivyo kwa wingine.
Nuru Faki Kombo mkaazi wa Kangani mwenye
ulemavu wa uziwi anaeleza, mawasiliano baina yao na watoa huduma za afya ni
changamoto.
Anasema wakati mwingine hulazimu kuwepo
mtu wa tatu wanapotaka huduma za afya, ili waipate ipasavyo haki yao hiyo ya
msingi.
Anafafanua kua, mara nyingi kunakua na
kutofahamiana baina yao na watoa huduma, kwani wengi wao hawana uwelewa wa
lugha ya alama.
Adinani Khamis wa Chake chake anasema,
mara nyingine hutumiza dawa madukani na kutumia, bila kuonana na wataalamu.
Anasema ni vyema Wizara ya Afya kuimarisha
mifumo ya mawasiliano, kwa kuweka wakalimani wa lugha ya alama hospitalini na
vituo vya afya.
“Sisi wenye ulemavu wa uziwi tunapata
shida sana kuwasiliana na watoa huduma wa afya, kwani hua hatuelewani, hivyo tunaomba
tuzingatiwe,”anasisitiza.
Wafanya kazi wa vituo vya afya na
hospitali wakiwemo madaktari na wauguzi, kazi yao kuhakikisha mtu anaefika
hospitali anapata huduma stahili, bila kujali hali ya mtu.
WATOA HUDUMA ZA AFYA
Abdullah Ali Juma Daktari wa kituo cha
afya Michenzani Mkoani Pemba anasema, utoaji huduma za kitabibu kituoni hapo, unatoa kipaumbele kwa watu wenye
ulemavu.
Anasema huweka umakini wa hali ya juu
zaidi kwa wenye ulemavu wa uziwi, ili mawasiliano baina yao yasiwe kikwazo.
Kwa kuepusha hili, Afisa watu wenye
ulemavu kutoka Umoja wa watu wenye Ulemavu ‘UWZ’ Pemba Maryam Mohamed Salum anasema,
watu wenye ulemavu wanapaswa kuzingatiwa, katika utoaji wa huduma za afya.
Anaeleza changamoto yeyote ile katika
vituo vya utoaji huduma hizo, inaweza kuzorotesha ustawi wa watu wenye ulemavu.
Mratibu
Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Pemba Mashavu Juma Mabrouk anasema, kuna
haja ya kuboresha mawasiliano kwa watoa huduma za afya.
Anaeleza kua, hili litasaidia kuimarisha
upatikanaji wa huduma bora kwa watu wenye ulemavu, hasa wale wa uziwi.
Anasisitiza wataalamu wa afya wanapaswa
kupewa mafunzo maalum ya kushughulikia mahitaji ya kundi hili.
Anaongeza kua watu wenye ulemavu wanapaswa
kushirikishwa katika kutathmini mipango na bajeti za afya, kama ilivyoelekezwa
kwenye sera na miongozo ya nchi kwa ujumla.
Kwa kuona umuhimu wa afya kwa watu wenye
ulemavu jitahada mbali mbali zinafanyika kutoka serikalini na
asasi za kiraia.
Huku lengo likiwa ni kuhakikisha ujumuishi
wao na upatikanaji wa haki hii ya msingi ya afya.
Moja ya asasi ni Chama cha waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar, ambao wanatoa mafunzo kuwajengea uwezo
waandishi wa habari, juu ya utetezi wa
haki za watu wenye ulemavu.
Masaidizi mkuu wa kitengo cha elimu ya afya Ghalib Hassan Hamad anasema, watoa huduma za afya wameshajengewa
uwezo ili kutoa huduma bora kwa watu wenye ulemavu.
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis
Bilali Ali anasema, wizara inaendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma na
upatikanaji wake kwa watu wenye ulemavu.
Anaongeza kuna kanuni zinazowataka watoa
huduma kutoa kipaumbele kwa wenye
ulemavu, katika utoaji wao wa huduma na wizara, inasimamia kwa karibu suala hilo.
Anasisitiza ingawa suala la wakalimani wa
lugha ya alama hospitalini ni changamoto, lakini kuna umakini mkubwa wa
kimawasiliano baina ya watoa huduma na watu wenye ulemavu wa uziwi.
“Ili wenye ulemavu kupata huduma stahili
za afya, wizara inajenga miundombinu yenye kufikika kwa kila mmoja, wahudumu
wetu wanatoa kipaumbele kwa wenye ulemavu na wanaumakini mkubwa wa kuwasiliana
nao,”anaeleza.
Wizara ya Afya itaendelea kuweka
miundombinu rafiki ya utoaji huduma bora kwa watu wenye ulemavu, kwani ni haki
ya msingi ya kila mmoja.
Aidha Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali
Mwinyi katika hutuba yake ya ufunguzi wa baraza la wawakilishi Zanzibar Novemba
10 mwaka huu, aliahidi kulinda na kuimarisha haki za watu wenye ulemavu.
MWISHO
Comments
Post a Comment