WAZAZI wa shehia ya Mgogoni Wilaya ya Wete Pemba wamelalamikia tabia ya walimu wa skuli ya Kinyasini kuwarudisha watoto wao skuli kwa ajili ya kuchukua pesa ya kufanyia mitihani, hali ambayo inarudisha nyuma maendeleo yao ya elimu.
Walisema kuwa, hawajakataa kulipa fedha kwa ajili ya mitihani ya watoto wao kwani ni jambo zuri, ingawa kinachowauma ni vile kutolewa wakati masomo, hali ambayo inawakosesha vipindi vinavyoendelea skuli.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wazazi hao walisema, wakati mwengine hawana pesa kutokana na hali ngumu ya maisha, hivyo huwapa pesa nusu kupeleka skuli ingawa hurejeshwa tena kwa vile hawajakamilisha, jambo ambalo linawauma sana.
āāHatujakataa kulipia kwa sababu tunapenda wafanye mitihani, lakini linalotusikitisha ni hili la kuwatoa watoto skuli waje nyumbani kuchukua pesa, kwa sababu wanakosa masomo na jengine wanaweza kufanyiwa udhalilishaji njiani kwani ni masafa marefu,āā walisema wazazi hao.
Walisema kuwa, ni kilio kikubwa kwa skuli hiyo, kwani iwapo hawakulipa hawaruhusiwi kufanya mitihani, hiyo hali ambayo inawadhalilisha wanafunzi hao ambao hawajalipa.
Mwananchi Ramadhan Khamis Juma na Maryam Khamis Sharif awalieleza kuwa, kufanya hivyo kunarudisha nyuma maendeleo ya watoto kielimu ambao wanapenda kusoma, hivyo ni vyema wakawaonea huruma kutokana na uwezo wao mdogo kifedha katika familia zao.
āāTunapenda sana watoto wasome na wafanyiwe mitihani kwa ajili ya kupimwa lakini hali zetu ni duni na hata tukiwapa pesa nusu basi wanarudishwa na ikiwa hatujaipata haturuhusiwi kufanya mitihani,āā walieleza.
Bikombo Abdalla Ali na Asha Bakar Omar walisema, watoto wao wanasikitika sana kufanyiwa hivyo na kuwaomba walimu kufanya subra pale ambapo mtoto hajalipa, kwani hilo ni jukumu la wazazi, wao waachwe wasome.
āāTunawaomba watuite sisi wazazi japo kwa kuwapa barua watoto au kutupigia simu kwa sababu masafa wanayorudi nyumbani sio madogo wanaweza kukumbana na vishawishi njiani wakadhalilishwa na pia wanakosa masomo mengine,āā alieleza.
Nae Hanifa Khamis Said aliomba walimu hao inapofanyika mitihani waruhusiwe wanafunzi wote, ili na wale ambao wana hali ngumu katika familia zao wasijisikie vibaya.
Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim alisema kuwa, Wizara ya Elimu inatoa huduma zote za kielimu bila ya malipo na ndio utaratibu, ingawa wameanzisha Kamati za skuli ambazo miongoni mwa majukumu yake ni kuimarisha ufaulu kwa wanafunzi na kusimamia maendeleo katika skuli zao.
āāHivyo zinakuwa na mamlaka ya ndani na wanakaa kujadili vipi tunaweza kuongeza ufaulu wa alama za juu, ukipitia ripoti mbali mbali za ziara zangu changamoto inayowakuta wanakamati ambayo inasababisha kutokufikia malengo ni utoro wa wanafunzi na tunashirikiana kupambana nalo,āā, alisema.
āāLakini mkakati mwengine ambao wanautumia sana kuimarisha ufaulu ni mitihani ya mara kwa mara na ni suala la gharama, sisi tunapeleka pesa za uwendeshaji maskulini lakini wanakamati wanaamua kila wiki wanafunzi wafanye mitihani, hivyo hufanya utaratibu wa kuchangisha wazazi na wanakubaliana pamoja,āā alifafanua.
Alisema pamoja na hayo, Wizara imetoa angalizo kwamba michango yote ambayo kamati na wazazi watakubaliana isimuathiri mtoto, hivyo alikumbusha na kupiga marufuku aina yeyote ya mchango kumuhusisha mwanafunzi.
āāNimekuwa nikiyakemea kila wakati kwa sababu pesa ile waliyokubaliana wanakamati na wazazi ni dhima na mzazi sio mwanafunzi na tunakataza hata iyo pesa asipewe mtoto kuipeleka bali aipeleke mzazi mwenyewe au waweke utaratibu wa kuifikisha,āā alikemea Mdhamini huyo.
Alisema kuwa, Wizara ya Elimu haikubaliani na kumuhukumu mtoto kwa sababu mzazi wake hakulipa fedha na hakuna skuli ambayo wataibani ikifanya hivyo na kuiachia salama, bali itachukuliwa hatua stahiki kwani pia inasababisha kumuathiri mtoto kisaikolojia.
Aliwasisitiza makatibu wa Kamati za skuli kuendelea kusimamia hayo kwa kutengeneza kamati ndogo ndogo, ikiwemo ya fedha, itakayosimamia kambi, ya kusimamia maadili ili walimu na wanafunzi wawe na muda mzuri wa kutekeleza majukumu yao ya kielimu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment