NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba, wametakiwa kuendelea kutilia mkazo, suala la upatikanaji wa sheria mpya na rafiki ya habari Zanzibar
Hayo yameelezwa Disemba 9, 2024 Afisa Program na mchechemuzi wa mpitio za sheria za habari Zanzibar, kutoka TAMWA-Zanzibar Zaina Abdulla Mzee, alipokuwa akifungua mafunzo ya ukumbusho wa sheria hizo, kwa waandishi wa habari wa Pemba, yaliofanyika ofisi ya TAMWA-Pemba.
Alieleza kuwa, waandishi wa habari ndio wahusika wakuu wa sheria hiyo, hivyo wanaowajibu wa kupigia debe na kuandika juu ya madhara yaliopo kwenye sheria zilizopo.
Alisema, mchakato wa upatikanaji wa sheria mpya, umekuwa ukionekana kwa mwendo wa kusua sua, hivyo waandishi wa habari, wanaweza kutumia kalamu zao, kuchapuza mchakato huo.
‘’Waandishi wa habari, mnaweza kuchapuza kwa haraka mchakato wa upatikanaji wa sheria mpya, kwa kutumia vipindi na makala mbali mbali, zinazoelezea changamoto za sheria zinazitumika sasa,’’alisema.
Akiwasilisha vifungu cha sheria ya Magazeti, Vitabu na Mawakala wa Habari nambari 5 ya mwaka 1988 na ile ya Tume ya Utangaazaji nambari 7 ya mwaka 1977, kwenye vifungu kandamizi, Mkufunzi mshauri Haura Shamte, alisema vinahitaji kupigiwa debe kwa haraka.
Alisema, kupitia vifungu hivyo, vimekuwa vikitishia uhuru wa kujieleza, ukusanyaji wa habari, uhuru wa habari jambo ambalo linatia shaka fani hiyo.
Akivitaja vifungu kandamizi kupitia sheria ya Magazeti, Vitabu, Mawakala wa Habari nambari 5 ya mwaka 1988, alisema ni pamoja na kifungu cha 27 kinachompa uwezo ofisa wa Polisi wa kukamata gazeti
Alikitaja kifungu cha 39, kinachoelezea sharti la kukusanya na kutoa habari na vifaa vya habari, ambapo uamuzi wa waziri wa kukataa kutoa kibali, haukatiwi rufaa.
Wakiwasilisha kazi za vikundi, waandishi hao walisema ipo haja ya kuchapuzwa kwa mchakato wa upatikanaji wa sheria mpya na rafiki ya habari Zanzibar.
Mwandishi wa kituo cha redio cha sauti ya Istqama, Bakar Khamis Juma, alisema uwezo wa ofisa wa Polisi kuweza kuingia na kupekura katika jengo la habari, ni uminywaji wa uhuru wa habari.
Nae Cicilia Mkini kutoka Redio Jamii Micheweni, alisema wakati umefika sasa kwa sheria mpya ya habari kupatikana hapa Zanzibar, ili kumarisha utawala wa kisheria.
TAMWA Zanzibar kwa sasa imo kwenye hatua nyingine ya kukutana na vyombo vya habari, ili kuvijengea uwezo, ili kuandika makala na kutengeneza vipindi, vya mwekeleo wa kuchapuza upatikanaji wa sheria mpya Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment