Na Nusra Shaaban
Ushiriki wa wanawake katika siasa ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu.
Lakini Zanzibar, ambapo wanawake wanaunda zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura, idadi yao kwenye nafasi za uongozi bado ni ndogo. Takwimu za mwaka 2020 zinaonyesha kwamba wanawake walichangia asilimia 22 tu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Je, sheria za uchaguzi zina mchango gani katika hali hii?
Changamoto Zinazowakabili Wanawake Katika Siasa
Mifumo ya uchaguzi Zanzibar imekuwa ikibeba changamoto mbalimbali kwa wanawake wanaotaka kushiriki siasa. Kwa mujibu wa Hidaya Yussuph Ali, Katibu wa Ngome ya Wanawake wa ACT Wazalendo, mfumo wa kura ya mapema umekuwa ni kikwazo kikubwa. "Wanawake wanakata tamaa kwa sababu mfumo huu unatoa mianya ya rushwa na udanganyifu, huku ukiongeza gharama kwa wagombea wanawake," anasema.
Gharama za kugombea pia zimekuwa mzigo mkubwa kwa wanawake wengi. Mtumwa Faiz Sadiki, Naibu Katibu Mkuu wa ADC, anaeleza kwamba gharama za uchaguzi zinawaondoa wanawake wengi, hasa wale wanaotoka vyama vidogo.
"Tunahitaji sheria inayowapa nafasi wanawake wote, bila kujali chama wanachotoka," anasisitiza.
Jitihada za Kurekebisha Mfumo
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imechukua hatua kadhaa za kuboresha usawa wa kijinsia. Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa ZEC, Maulid Ame Muhammed, anasema kwamba sera maalum ya jinsia ya mwaka 2020 inalenga kuwahamasisha wanawake kushiriki katika siasa.
"Tumepunguza ada ya kugombea kwa asilimia 50 kwa wanawake ili kuwapa nafasi zaidi ya kushiriki uchaguzi," anaeleza.
Hata hivyo, hatua hizi bado hazitoshi kwa wanawake wengi. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, asilimia 30 ya wanawake wanaotaka kugombea huchukizwa na changamoto za kiuchumi na kijamii, huku mifumo ya uchaguzi ikionekana kuwa haina uwazi wa kutosha.
Suluhisho na Mapendekezo
Wadau wengi wanasema kwamba sheria za uchaguzi zinapaswa kufanyiwa mabadiliko makubwa. Miongoni mwa mapendekezo ni pamoja na :
1. Kufuta au kurekebisha kura ya mapema* : Mfumo huu umelaumiwa kwa kuathiri uadilifu wa uchaguzi, hasa kwa wanawake.
2. Kuhakikisha viti maalum vinapatikana kwa vyama vyote : Hii itatoa nafasi kwa wanawake wa vyama vidogo kushiriki kikamilifu.
3. Kupunguza zaidi gharama za uchaguzi* : Hatua hii inaweza kuongeza ushiriki wa wanawake, hasa wale kutoka familia za kipato cha chini.
Je, 2025 Itakuwa Mwaka wa Mabadiliko ?
Licha ya changamoto zilizopo, wanawake wa Zanzibar wameendelea kupigania nafasi zao kwenye siasa. Kampeni za kuhamasisha ushiriki wa wanawake zimeanza kuonyesha matunda, lakini bado safari ni ndefu.
Kama alivyosema Tunu Juma Kondo, Naibu Katibu Mkuu wa UWT, "Ni jukumu letu kuhakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi sawa na wanaume kwenye siasa. Hii sio tu kuhusu usawa wa kijinsia, bali pia maendeleo ya taifa letu."
Sheria za uchaguzi zina nafasi kubwa katika kufanikisha au kukwamisha malengo haya. Zanzibar iko kwenye njia panda, je, itaamua kurekebisha mfumo huu na kuwapa wanawake nafasi wanayostahili? Jibu lipo mikononi mwa wanasiasa, watunga sheria, na jamii kwa ujumla.
Mwisho
Comments
Post a Comment