NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, limekiri kupokea malalamiko ya mwanamke mmoja, akimtuhumu mtendaji wa Jeshi hilo, kumbaka ndani ya kituo cha Polisi.
Jeshi hilo limesema, ni kweli walipokea lalalamiko hilo, ingawa lilisema ili kukamilisha na kutoa taarifa rasmi, wamo kwenye upelelezi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu Disemba 6 mwaka huu majira ya saa 8: 17, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo Mussa Mwakasula, alisema kwa sasa hawana taarifa pana juu ya tukio hilo.
Alieleza kuwa, kwa sasa wanaendelea na uchunguuzi wa tukio hilo, na hasa baada ya kuzipata taarifa hizo, kutoka kwa mlalamikaji.
‘’Ni kweli tumepokea lalamiko la mwanamke mmoja, akimtaja askari wetu, kwamba ndie aliyembaka, ingawa kwa sasa taarifa rasmi itatolewa baada ya uchunguuzi wetu kukamilika,’’alisema Kaimu Kamanda huyo.
Baadhi ya wananchi waliokataa kutaja majina yao , walisema mwanamke huyo kabla ya kudai kutendewa kosa hilo, alifika kituo cha Polisi cha Mchanga mdogo wilaya ya Wete, ili kuhojiwa kwa tukio jingine.
‘’Unajua yule mwanamke awali alikuwa na ugomvi na muume wake, sasa hiyo siku ya tukio, aliitwa kwenda kuhojiwa Polisi, ndio kisha wakati anatoka alilalamikia kubakwa,’’walidai wananchi hao.
Aidha wananchi hao walisema, baada ya tukio hilo na muume wake kupigiwa simu, alimueleza kwamba ikiwa amlimpeleka kituo cha Polisi cha Mchanga mdogo, ili abakwe na kukataa.
‘’Mwanamke alimuuliza muume wake, kwamba alimtaka afike kituo cha Polisi ili abakwe, na muume kukataa na hapo ndio taarifa zilipoanza kutolewa na mimi kusikia,’’alisema
Sheha wa Mchanga mdogo Asaa Makame Said, alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi, ikiwa anataarifa hizo ndani ya shehia yake, alijibu hana.
Upande mwingine wa taarifa zikaeleza kuwa, mlalamikaji huyo anatokea nje ya shehia ya Mchanga mdogo, ambae alikwenda kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano.
Mratibu wa wanawake na watoto Awena Salim Kombo, shehia anayotoka mlalamikaji huyo wilaya ya Wete, alikiri kuwa, mlalamikaji huyo anatokea ndani ya shehia yake.
‘’Ingawa mlalamikaji huyo hakuja kuripoti kwangu moja kwa moja, lakini baada ya kufuatilia nilibaini kuwa, mhanga huyo anatokea shehia yangu,’’alifafanua.
Hata hivyo Mratibu huyo, alisema baada yakufuatilia alijiridhisha kuwa, mtuhumiwa anashikiliwa kituo cha Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, kwa mahojiano zaidi.
Mwanamke aliyedai kubakwa, alikiri kutokezewa na tukio hilo, na kusema alikuchukuliwa ndani ya chumba cha kituo cha Polisi, kwa ajili ya kuhojiwa.
‘’Ni kweli askari alinibaka nikiwa ndani ya kituo cha Polisi Mchanga mdogo, tukiwa ndani ya chumba, ambacho aliniita kwa nia ya kutaka kunihoji, ingawa alinigeuzia kibao,’’alilalamika.
Hata hivyo, alisema atahakikisha haki yake inapatikana, na hatokuwa tayari kuchukua hongo ili kesi hiyo imalizike, kienyeji.
Muume wa mwanamke huyo , alithibitisha kupokea lalamiko la mke wake, juu ya kubakwa ndani ya kituo cha Polisi cha Mchanga mdogo, kwa njia simu akiwa kazini.
Alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa, tukio hilo lilitokea Novemba 24, mwaka huu majira ya saa 3:15 asubuhi wakati mke wake, alipokwenda kituoni hapo, kwa ajili ya mahojiano ya tukio jingine.
‘’Ni kweli juzi mke wangu alinilalamikia kuwa, alitendewa tendo la ubakaji na askari, ambae alikuwa anamuhoji kwa tukio jingine, lililotokezea baina yangu na yeye,’’alifafanua.
Alipoulizwa hatua alizochukua, anasema hajafanya jambo lolote, kwa vile mke wake huyo, hampi ushirikiano baada ya tukio hilo kwa kumficha ficha.
Akizungumza na mwandishi hizi akiwa Kamisha wa Polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad (sasa Balozi), alipopigiwa simu majira ya 9:18 Disemba 6, mwaka huu alaasiri, alimtaka mwandishi wa habari, kufuatilia tukio makao makuu ya Jeshi la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba.
‘’Wewe mwandishi wa habari si uko Pemba, basi wasiliana na Kamanda wa Polisi mkoa husika, maana mimi naweza kukupa taarifa, ambazo sio za uhakika,’’alisema.
Baadhi ya wanaharakati wa haki za binaadamu, walisema wana hofu ya kutotenda haki, kwa vile mtendaji ni Polisi na wanaolifanyia uchunguuzi ni muajiri wake.
Upande mwingine, taarifa ya Ofisi ya Mtakwimu mkuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaoneshwa uwepo wa matukio 147 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia, yalioripotiwa kwa mwezi Oktoba, 2024.
Ambapo ikafahamika kuwa, waathirika walikuwa 147, wengi wao walikuwa ni watoto sawa na asilimia 83.0, wanawake asilimia 11.6 na wanaume asilimia 5.4.
Miongoni mwa watoto (waathirika 122), wasichana walikuwa 101 (asilimia 82.8) na wavulana walikuwa 21 sawa na (asilimia 17.2).
Ikafahamika kuwa, idadi ya matukio kwa mwezi, yamepungua kwa asilimia 0.7 kufikia matukio 147 mwezi wa Oktoba, 2024
Mwisho
Comments
Post a Comment