Skip to main content

HATIMAE BARABARA MELI TANO- WETE YAANZA KUTIWA LAMI, WANANCHI HAWAAMINI MACHO YAO

 

NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WANANCHI na waendesha vyombo vya moto wanaotumia barabara ya Meli tano- Wete, wamesema zoezi la utiaji wa lami wa barabara hiyo, ndio wameanza kujenga matumiani ya kuitumia barabara hiyo bila ya usumbufu.

Walisema, sasa wanaamini na kuanza kusahau machungu waliyodumu nayo kwa miaka zaidi ya 20, kufuatia kuharibika kwa miundombinu ya barabara hiyo bila ya kufanyiwa matengenezo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema kwa sasa hawana shaka ten ana nia ya serikali ya kuwatengenezea barabara hiyo, hasa baada ya kuanza kwa zoezi la utiaji wa lami wiki tatu zilizopita.

Walisema, kwa sasa hawana wasi wasi na kuwataka wenzao wanaoitumia kutoa ushirikiano wa karibu na mafundi hao, ili zoezi hili liwe rahisi kwao.

Mmoja katia ya wananchi hao Mwanajuma Haji Nassor ‘anti mwaju’ alisema zaidi ya miaka 30, barabara hiyo ilikuwa ikitajwa kuuanza ujenzi wake bila ya mafanikio.

Alieleza kuwa, walifika pahala walishindwa kuamini nia thabiti ya serikali kwamba barabara hiyo yengenjwa kwa kiwango la lami.

‘’Maana ahadi zilishakuwa nyingi mno kwetu, sasa ilifika pahala hata tukielezwa hakuna anayeamini, maana tulishakula dhiki na usumbufu kwa miaka mingi,’’alieleza.


Nae Khamis Omar Khamis, alisema zoezi linaloendelea la utiaji wa lami ndio limewapa uhakika kwamba, sasa serikali inataka kutimiza ahadai zake kwetu.

Dereva wa gari ya abiria aliyejitambulisha kwa jina la Khamis Haji, anayefanyakazi Chake chake-Wete kupitia barabara hiyo, alisema walishapata usumbufu kwa muda mrefu.

‘’Hata wakati ujenzi unaaza wa kuisafisha barabara hii, mimi na wenzangu hatukuamini kwamba, itafika pahala iwekee lami, maana ahadi zilishakuwa nyingi,’’alieleza.

Hata hivyo, alisema kwa kasi ya uwekaji lami kwa sasa, wanayomatumaini ya kweli, kwamba sasa dhiki inaweza kuandoka wakati wowote.

Dereva wa piki piki ‘boda boda’ anayechukua abiria eneo la Meli tano, alisema sasa wanafurahishwa na kazi ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.

‘’Mwinyi naamini ametumia nguvu nyingi kuhakikisha barabara hii haikuwami tena, na leo zoezi la uwekaji limeshaanza na sasa naamini juu ya kukamilisha ahadi hii,’’alisema.

Mkubwa Haji Kassim mwenye ulemavu wa viungo, alisema sasa wataisahau dhiki ya kupita kwa dhiki na baiskeli zao za magaurudumu matatu.

Mkuu wa wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar, alisema kasi ya Dk. Mwinyi ndio iliyosababisha barabara hiyo na nyingine kuendelea kwa kasi ujenzi wake.

Akitembelea ujenzi wa barabara hiyo, Julai 30, mwaka huu Makamu wa Pili war ais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, aliitaka kampuni ya Mecoo inayojenga barabara hiyo kuongeza kasi zaid.

Alisema, anajua kuwa kwa mujibu wa mkataba wake, ilitakiwa barabara hiyo ikamilike tokea mwezi Augost mwaka huu, ingawa kutokana na sababu mbali, wakaongezewa tena miezi mitano mbele.

Akizungumzia kusua sua kwa ujenzi wa barabara hiyo Mkandarasi wa kampuni hiyo Nassor Kolowa, alisema moja ni kucheleweshewa kwa malipo na kuondoa udongo mwingi usiohitajika kwenye barabara hiyo.

Hata hivyo, Afisa Mdhamini wa wizara ya Ujenzi, Usafirishaji na Uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma, alisema hadi juzi, tayari kilomita 2.2 zimeshaweka lami moto.

Alieleza kuwa, zipo kilomita 7.3 nazo tayari zimeshawekea rojo ‘primer’ tayari kwa maandalizi ya uwekaji wa lami moto, ambapo zoezi hilo halitarajiwei kusita tena tokea lilipoanza wiki tatu zilizopita.

Barabara hiyo ya Chake chake -Wete yenye urefu wa kilomita 22, ujenzi wake unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 26.6, ambapo mkataba wa ujenzi ulisainiwa mwaka 2022 na ilitakiwa kukamilika Agosti 2024.

                      mwisho

Comments