'JAMBO NIA PEMBA’ : USHIRIKA WA VIJANA WAFUGA NYUKI, WAMILIKI MIZINGA 40, NJIA YA KUKUZA PATO NYEUPE
NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
NI majira ya
saa 10: 00 jioni, katika pita pita zangu, niliangukia kijiji cha Fuuweni,
kilichomo ndani ya shehia ya Mfikiwa, wilaya ya Chake chake Pemba.
Pita pita
yangu, ilisikia harufu ya asali kwa mbali, kwa vile mramba asali harambi mara
moja, hata hiyo harufu nami sikutosheka kuisikia mara moja.
Nilipoangaza macho
juu, niliwaona nyuki wakitoka upande wa mashariki na kwenda magharibi mwa kijiji
hicho, hapo lakini ghafla niligundua kuwa, ni wale wanaofugwa.
Si nilishazoea
kila ninapoona nyuki, basi huwa ni wale wa msituni na kufua (kuvuna)
unajipangia mwenyewe, lakini kumbe hawa ni wale waliochini ya himaya ya vijana
wa kijiji cha Fuuweni shehiani hapo.
Sikutaka kuonekana
mwizi, la hashaa….nilimvuta kijana mmoja pembeni nikamuuliza, ikiwa wahusika wa
wanaofuga mizinga hiyo, wapo karibu ili nizungumze nao.
Walishasema wahenga
nyota njema huuonekana alfajiri, nami nilibahatika kuzungumza na Msaidizi
Katibu wa ushirika huo wa ‘Jambo nia’ Salum Msellem Salum.
HISTORIA YAO
Kabla ya
ufugaji huo wa nyuki, anasema walianza kukumbwa na changamoto ya ukosefu wa
fedha za ada kwa vijana hao, katika suala la elimu kwa wakati huo wa mwaka
2020.
Hivyo,
waliamua kuanzisha mpango wa kuweka na kukopa, ili sasa isiwe kikwazo kwa
wanachama wa ‘jambo nia’ anaetaka kujiendeleza kimasomo ama kulipia ada.
Ndipo ilipofika
Febuari 2, mwaka 2020 wakajikusanya vijana 23, wakiwemo wanawake watano (5), ili
kujiwekea fedha hizo na kisha kuzikopa, kwa ajili ya kujikwamua.
‘’Hasa hisa
yetu hii, ilikuja baada ya sisi kukosa fedha za kujiendeleza kielimu, iwe kwa
kujinunulia mitihani au vifaa vya masomo, maana familia zetu ni duni,’’anasimulia.
Akaenda mbali
zaidi, akisema kuwa hapo sasa kasi ikawa moja na kuanza kujiwekea shilingi 5,500
kwa kila mwanachama mmoja, na hivyo kwa wikim wakawa wanakukusanya shilingi 126,500
sawa na shilingi 5060,00kwa mwezi.
‘’Ilipotimia
miezi mitatu wakati huo tukiwa na shilingi milioni 1.5, kazi ya kuanza kukopa
kwa ajili ya elimu na changamoto nyingine, ilianza kwa wanachama,’’anaeleza.
Wapo waliofanikiwa
kujinunulia mitahani ya kidato cha nne, na wingine vifaa vya masomo kama viatu
na kamalu, ambapo hapo kabla hawakuwa na uwezo huo.
Ndio maana,
Mwenyekiti wa ushirika huo Hussein Khamis Salim, akasema ilipofika mwaka mmoja
tokea kuanzisha kwa hisa hiyo, na kufikia wastani wa shilingi milioni 18,
waligawana.
Wapo wanachama
waliopata shilingi 400,000 wengine shilingi milioni1 na hata wengine kujipatia
shilingi 700,000 kwani uwekaji wa hisa hutegemea nguvu na uwezo wa mwanachama.
Wanaushirika hao,
licha ya kugawana fedha hizo, lakini waliamua kuzaa mradi wa mboga mboga aina
za mchicha, bamia, bilingani na tungule, ingawa kisha walishindwa, kwa sababu
ya huduma ya maji.
Mwenyekiti
huyo anasema, kilimo hicho ambacho hakikudumu kutokana na ukosefu wa huduma ya maji,
msimu mmoja, walitumia nguvu kazi ya shilingi 100,000 na ununuzi wa mbolea
maalum kwa ghama kama hiyo.
‘’Pamoja na
hiyo wakati huku hisa ikiendelea, tulipovuna mboga zetu, tulipatia shilingi
400,000 ni sawa na faida ya shilingi 200,000 na kisha fedha hizi zilizaa mradi
wa ufugaji nyuki,’’anaeleza.
MRADI WA
UFUGAJI NYUKI
Mwenyekiti anaeleza
kuwa, mradi huu waliuzaa kwa malengo kadhaa, moja ni kujiongezea kipato cha
halali, pili kutunza mazingira na hasa baada ya kubaini wazazi wao, waliharibu
mazingira kwa ukataji miti kwa kutengenezea vinu na michi.
Kwa mara ya
kwanza, walizna na mizinga 10 ya nyuki, ambayo waliitengeneza wenyewe, kwa
kutumia vifaa vya asili na walibahatika kunasa nyuki kama walivyopanga.
Ushirika wa ‘Jambo
nia’ ulianza kufikia nia yake, baada ya kukabidhiwa mizinga 10 kwa njia ya mkopo,
ingawa kutokana na uchakavu wake mingine iliharibika.
‘’Mizinga
tuliambiwa tunakopeshwa, na nyuki wameshanasa na tukipokaribia kuvuna, wakati
wa kuihamisha ilikuwa inavunjika wenyewe, na mingine hata kuruhusu wadudu
kupita,’’anaeleza.
Hivyo, wakajikutana
wanayomizinga 14, ingawa mwanzoni mwa mwaka 2023, taasisi ya ‘PIRO’ baada ya
kuwapa mafunzo ya namna bora ya ufugaji nyuki, kisha waliwakabidhi mizinga
mitatu mikubwa na ya kisasa.
‘’Yale
tuliopewa na PIRO, ilikuwa mikubwa na mwanzoni mwa mwaka huu, tulitarajia
tuvune, ingawa tulighairisha kutokana na kuvuma kwa upepo mkali na mvua,’’anafafanua.
Walihofia kuwa
nyuki, wanaweza kutoroka ikiwa watavuna katika kipindi hicho, hivyo kwa sasa
wamejipanga kuvuna miezi minne ijayo kwa mizinga iliyobakia 13.
Wanasushirika
hao, wanasema kila mzinga mmoja, wanategemea kujipatia wastani wa chupa tano (5),
kama utanawiri kama walivyotegemea, hivyo kuwa na chupa 65.
Moja ya faida
ambayo ushirika huu wanaweza kuupata kuanzia mwezi August mwaka huu hadi Septemba
ni shilingi milioni 1.6, kwani kwa sasa chupu ya moja ya asali yenye ujazo wa
lita moja, ni shilingi 25,000 hadi shilingi 30,000.
Hapa mwanachama
wa ushirika huo Ali Thabiti Ali, anasema wakati hisa yao ikiendelea na uvunaji
huo wa usali ukifanyika, wanaweza kujipatia matunda mara mbili.
‘’Moja ni
faida ya fedha, lakini pili sasa kupata asali ambayo kiafya ni tiba kwa
magonjwa mbali mbali, ikiwemo mishipa,’’anasema.
MALENGO YAO
YA BAADAE
Msaidizi
Katibu Salum Msellem Salum, anasema malengo yao ya baadae kwanza ni kuhakikisha
wamejiimarisha kipato cha ushirika wao, na hata mwanachama mmoja mmoja.
Maana anasema,
wanatokea kwenye hali duni tena hasa ya kipato, ingawa tokea wakijusanye pamoja,
makali ya maisha yanaonekana kupungua kila siku zikisogea.
‘’Lakini pia
malengo yetu ni kuhakikisha vijana waliopo kijijini kwetu hapa Fuuweni shehia
ya Mfikiwa wilaya ya Chake chake, wanakua sehemu yetu kwa kuwapa ajira za mashamba
yetu ya nyuki,’’anaelezea.
Mwenyekiti
wao Hussein Khamis Salum, anasema kisha kuona kila mwanachama anajitegemea
katika kujiajiri mwenyewe, ili nao waone wanawaajiri vijana wingine.
Hapa anakazia
kamba, kuwa kwa vile hakuna serikali yenye uwezo wa kuwaajiri watu wote, ndio
maana wao 23, wakaamua wakijusanye ili kujiajiri wenyewe na wenzao hapo baadae.
CHANGAMOTO
Moja ya changamoto
iliyotaja na mwanachama wa ushirika huo Mustafa Thabiti Ali ni elimu duni ya
ufugaji nyuki, jambo ambalo haliwapi raha kwa hofu ya kukimbiwa na nyuki.
Mwenyekiti
anasema uhaba wa mizinga 13 ya sasa waliyonayo, na kama kuna mfadhili
wanahitajia tena ili 27, ili ifikie 40, kwa ujumla katika kazi yao hiyo.
Akaelezea kuwa,
hata suala la masharti ya mikopo iliyoko serikali, huwakwaza na kuachana nayo, ingawa
wanaendelea kuumia kwa udogo wa mtaji wao.
SHEHA
Sheha wa shehia
ya Mfikiwa Bimkubwa Rajab Tangwi, anasema ushirika huo amekuwa akiupigania, ili
kupata elimu na vifaa, kwani wamekuwa mstari wa mbele, kutafuta riziki ya halali.
Kila
anaposikia pana fursa ya kwa ajili yao, huwasiliana nao, akiamini kuwa mafunzo
na vifaa wanaopewa, havipotei.
WANANCHI
Mmoja kati ya
wananchi Khamis Ali Khamis, anasema vijana hao wamekuwa wapambanaji kwa vitendo,
katika kujiajiri, maana wameanza na hisa, kilimo cha mboga na sasa wameshaingia
kwenye kilimo cha nyuki.
Mkubwa Ali Khatib,
anasema kama ushirika huo utawezeshwa kivifaa, mtaji na mafunzo na kisha
kusimamiwa kidogo, unaweza kuwa mfano kwa Pemba nzima,
Mwananchi Masika
Mohamed Ali na mwenzake Kheriyangu Mohamed Ali, wanawapongeza vijana hao, kwa
moyo wao kujitolea na kujituma ambapo matunda yake yameanza kujitokeza.
SERIKALI KUU
Waziri wa
Nchi Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Sharif Ali Sharif, wakati akiwasilisha
hutuba ya bajeti ya mwaka 2024/2025, anasema serikali, inaimarisha sekta ya ushirika,
ili kuleta ufanisi wa kutoa ajira, kunyanyua pato la mwananchi na uchumi wa nchi.
Sekta hiyo
inashajiisha uundaji wa vyama vya ushirika, kwa lengo la kuwaweka pamoja, ili
kupata huduma kadhaa ikiwemo mafunzo ya ujuzi na mitaji.
Ndio maana, akasema
kwa mwaka wa fedha 2023/2024 wizara imesajili vyama vya ushirika 1, 560
ikilinganishwa na vyama 1,822 kwa mwaka 2022/2023.
Waziri Sharif
anasema, wamepiga hatua katika utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali, katika
maeneo ya ufugaji wa nyuki, usarifu wa matunda na mboga, utengenezaji wa vifaa
vya sola, masoko, ujasiriamali na mafunzo ya uokaji.
Hili linatajwa
kuongezeka kutoka wajasiriamali 1,239 kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia 3,979,
ambapo Unguja ni 1963 na Pemba 2,016, kwa mwaka 2023/2024.
Mwisho
Comments
Post a Comment