NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia ya Mfikiwa wilaya ya Chake
chake, wamesema kupooza kwa ulinzi shirikishi katika shehia yao, kumesababisha
kurudi upya vitendo vya kihalifu, ikiwemo wizi wa mifugo.
Walisema, kwa sasa wapo wafugaji wanaolazimika kulala na
mifugo yao majumbani kama vile Ng’ombe kutokana na kuhofia wizi ulioshamiri
shehiani hapo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, Juni 22, 2024 walisema, kwa sasa hali ya vitendo vya kihalifu imeibuka upya, kufuatia ulinzi
shirikishi kutoonekana.
Walieleza kuwa, kwa sasa ndani ya shehia yao hakuna
ndizi, muhogo, fenesi, chungwa wala mifugo ya kuku, Ng’ombe na Mbuzi wanaonawiri
kwa wizi ulivyokithiri.
Mmoja kati ya wananchi hao Mohamed Khamis Ali, alieleza
kuwa, kwa miaka zaidi ya sita sasa, hakuna tena ulinzi shirikishi ambao
uliondoa vitendo vya uhalifu.
‘’Sasa hakuna mkulima wala mfugaji anaefaidika na mazao yake, kutokana na wizi uliokithiri ambao ni watu kutoka ndani ya shehia yetu,’’alieleza.
Nae Mkubwa Ali Khatib alisema, ijapokuwa haupo kama zamani,
lakini kutokana na ulinzi shirikishi kupooza, kwa sasa wizi umejitokeza.
Kwa upande wake Mzee wa nasaha katika ulinzi shirikishi jamii
shehiani humo, Khamis Ali Khamis alisema, wananchi baada ya kulinda na kutokomea
kwa vitendo hivyo, walijisahau na sasa kurudi upya.
Alifahamisha kuwa, hapo zamani kulikuwa na wizi wa Ng’ombe
kati ya 10 hadi 25 kwa mwaka, ingawa kisha ulipotea na sasa wizi huo, kurejea
tena kwa kasi.
‘’Ulinzi ushirikishi kwa sasa hauna tena nguvu kama
zamani, hali inayosababisha wizi wa mifugo na mazao, kurejea na kuwaumiza wakulima
na wafugaji,’’alieleza.
Kwa upande wake mwananchi Mkasi Mohamed Ali, alisema
kupooza kwa ulinzi shirikishi, kumesababisha hata kuibuka kwa watumiaji wa dawa
za kulevya.
‘’Imekuwa kama vile mji wetu wa Mfikiwa hauna mwenyewe,
vijana wanazurura ovyo, hukaa vijiweni hadi usiku wa manane, hapo huzaliwa
mashauri ya wizi na utumiaji dawa za kulevya,’’alieleza.
Kwa upande wake Sheha wa Mfikiwa Bimkubwa Rajab Tangwi,
alikiri kuwepo kwa wizi uliopindukia shehiani mwake, kutokana na wananchi
kukataa kuendeleza ulinzi shirikishi.
Alieleza kuwa, wananchi kama waliovunjika moyo, juu ya kuendeleza
ulinzi shirikishi, kwani husaidia kukoa mazao na mifugo na vijana waliojipanga
kwa wizi.
‘’Kwa sasa shehia ya Mfikiwa, wizi wa mazao na mifugo upo
kama kawaida, maana jamii imeacha ulinzi shirikishi, tofauti na zamani,’’alieleza.
Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Abdalla Hussein Mussa,
ameikumbusha jamii ya Mfikiwa, kuurejesha ulinzi shirikishi, ili kukabiliana na
uhalifu.
Alieleza, kuwa serikali iliupelekea ulinzi kwa jamii husika,
ili kutumia mbinu na mikakati ya kienyeji kuzuia uhalifu na kuona kila mmoja,
anaishi kwa amani.
Shehia ya Mfikiwa ipo wastani wa meli sita kutoka katikati
ya mji wa Chake chake, ipo karibu na uwanja wa ndege wa Pemba, ikizungurukwa na
shehia za Pujini, Chanjaani, Mgogoni na Vitongoji wilaya ya Chake chake.
Mwisho
Comments
Post a Comment