WAUMINI
wa dini ya kiislamu shehi za Wambaa na Chumbageni wilaya ya Mkoani Pemba, wamekutana
na kukubaliana kuanzisha mfuko maalum wa uchinjaji, kila ifikapo mfunguo tatu,
kwa ajili ya sadaka kwa wasiokua na uwezo.
Kwenye kikao
hicho, kilichofanyika skuli ya Wambaa, waumini hao walisema, imeonekana kuna
kundi kubwa kubwa la waumini wenzao, wamekuwa kikosa kitoweleo kwa siku za sikukuu,
jambo ambalo sio sahihi.
Akizungumza Mwenyekiti
wa muda wa mfuko huo Ali Abdi Mohamed, jana Juni 22, 2024 alisema wamekusudia kuwa mfuko huo
uwasaidie, wale ambao uwezo wao uko chini.
Alieleza kuwa,
mpango huo wa uchinjaji kila ifikapo mfunguo tatu, kwa hatua za awali
utahusisha kila watu saba, kutakiwa kumiliki Ng’ombe mmoja na kumuwasilisha kwa
kamati, kwa ajili ya uchinjaji.
Mwenyekiti
huyo alisema, kisha baada ya kukamilisha taratibu za uchinjaji, kutagawiwa mafungu
matatu, kama sheria ya dini ya kiislamu ilivyoelekeza, ambapo fungu moja
hutolewa kwa wasiokuwa na uwezo.
‘’Kamati hii
inaskusudia hasa kuwahamasisha wanawambaa na Chumbageni popote walipo, waungane
na sisi katika kukusanya Ng’ombe wengi zaidi, na kuchinja kwa pamoja, ili kila
mmoja apate kitoweleo siku ikifika,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine Mwenyekiti huyo huo wa muda, alisema kuanzia sasa, kila muumini wa
dini ya kiislamu anayetaka kuungana na mfuko huo, awasilishe jina lake mapema.
Kwa upande
wake Katibu wa muda wa mfuko Mwalimu Ali Ussi, alisema kwa kuanzia mwaka jana,
walichinja Ng’ombe watatu, kwa mpango wa kushirikiana.
‘’Mahitaji
yameonakana makubwa, maana kila mmoja alikuwa anahitaji kitoweleo, na ndio
maana sasa tunatoa taarifa mapema, kuelekea mwakani, ili tukusanyika tuwe wengi,’’alieleza.
Sheha wa
shehia ya Chumbageni Mgeni Othman, alisema wazo hilo ni zuri na ni jema mno, maana
litaongeza umoja na mshikamano wao.
‘’Suala la
kuanzisha mfuko wa uchinjaji, kwa lengo la kupata Ng’ombe wengi zaidi hapo
mwakani ni jambo jema, maana ni kweli wapo wasiokuwa na uwezo, hula hadi dagaa
siku ya sikukuu,’’alieleza.
Mjumbe wa
mfuko huo Mohamed Juma Khamis, alisema ni vyema jamii ya kiislamu kushajiishana,
ili mwakani walau wapatikane Ng’ombe 20, ili kila mmoja apate nyama siku ya
sikukuu.
Kwa upande
wake mjumbe Hadia Ramadhan, alisema changamoto aliyoiona kwa msimu uliomalizika,
ni kujitokeza kwa watu wengi wenye hali ngumu, wanaohitaji kusaidiwa.
Akizungumzia
umuhimu wa kuchinja kwa ajili ya Allah, sheikh Abdi Salim Khamis, alisema kila
unyoya mmoja ya mnyama aliyechinjwa, wahusika wanaandikiwa thawabu.
‘’Haipendezi
kuona siku ya sikukuu, wengine wanakula nyama na wengine wanakula dagaa, kwa
sababu ya kukosa sadaka, lazima hili waumini wa Wambaa na Chumbageni tulifikirie,’’alifafanua.
Wakichangia kwenye
mkutano huo, mshiriki Juma Abassi Ali, aliitaka kamati hiyo, kujipanga kutafuta
Ng’ombe mapema, ili kuepuha kupanda bei, hapo baadae.
Nao washiriki
Juma Ali Pandu, Juma Abdalla Jonga, Amini Haji Makame na Khamis Khatib Khamis,
walitaka mfuko huo, uwe wa kudumu hapo baadae.
Akifunga kikao
hicho, mjumbe wa mfuko huo Mohamed Abdi Mohamed, alisema kuanzia mwakani,
watahakikisha hakuna muumini wa dini ya kiislamu ndani ya shehia za Wambaa na Chumbageni,
atakaekosa kitoweleo.
Alifafanua kuwa,
hilo litawezekana iwapo watajitokeza wadau wengi zaidi kuunga nguvu kupitia
mfuko huo, au wafadhili wengine mbali mbali.
Mfuko huo wa
uchinjaji wa shehia za Wambaa na Chumbageni wilaya ya Mkoani, kwa mwaka jana
ulichinja Ng’ombe watatu na wastani wa waumini 56, walisambaaziwa sadaka hiyo,
kati yao 14 ndio waliokuwa wagawaji.
Mwisho
Comments
Post a Comment