NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAFUNZI
wanaosomea uwalimu Chuo cha taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ kampasi ya Benjamin Wiliam
Mkapa Wete Pemba, wamependekeza adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa mtu atakaetiwa
hatiani, kwa kosa la dawa za kulevya.
Walisema,
haiingii akili kuona, mahkama imeshamtia hatiani mtu kwa kukutwa na dawa za kulevya,
ambazo huathiri nguvu kazi ya taifa na kisha, kupewa hukumu ya kifungo pekee.
Wakizungumza leo Juni 26, 2024 kwenye kongamano la vyuo vikuu, juu ya masuala ya msaada wa kisheria, kuelekea wiki
ya msaada wa kisheria Zanzibar, lililofanyika Chuoni hapo, walisema wakati
umefika sasa kutolewa kwa hukumu hiyo.
Walipendekeza
kuwa, ni vyema kwa mtu anayetiwa hatiani asibakie chuo cha Mafunzo pekee kuitia
tena hasara serikali kwa chakula na wakati mwingine matibabu, wakati tayari
ameshasababisha madhara, kwa vijana.
Mshiriki Juma
Nafasi Juma, alifafanua kuwa kama mtu ameamua kuliumiza taifa kwa kuingiza,
kusafirisha, kusambaaza dawa za kulevya, hivyo ni vyema anapotiwa hatiani, hukumu
yake ni kunyongwa hadi kufa.
Nae mshiriki
Sharif Hamad Iddi, alisema serikali iondoe fungu la huruma kwa wanaoingiza aina
yoyote ya dawa za kulevya, kwani madhara yake ni makubwa.
Nae Nasfa
Abdalla Abdi, alieleza kuwa kupitia kongamano hilo, amejifunza mambo kadhaa,
ikiwemo mbinu chafu za wasafirishaji dawa za kulevya na wajibu kama jamii.
Akilifungua kongamano
hilo, Afisa Mdhamini Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ
Pemba, Thabiti Abdalla, aliwataka wanafunzi hao, kuzitumia simu zao, ili kujifunza
masuala ya sheria.
‘’Kama
ambavyo ujumbe wa mwaka huu unaelezea, tumia teknologia kurahisisha upatikanaji
wa haki, hivyo nanyi msiwe nyuma, katika kufikia hilo,’’alieleza.
Aidha Afisa
Mdhamini huyo, ameisisitiza haja kwa jamii, kujifunza pole pole masuala ya sheria,
kupitia wasaidizi wa sheria waliomo majimboni mwao, ili kujua haki na wajibu wao.
‘’Suala la
kujifunza mambo ya kisheria ni wajibu wa kila mmoja, kwani hakuna kinga, kwa kisingizio
cha kutokujua sheria,’’alifafanua.
Akizungumza kwenye
kongamano hilo, Meneja Mawasiliano na Ushirikiano wa kutoka ‘LFS’ Jane Matinde,
alisema taasisi yao itaendelea kufanyakazi kwa karibu na Idara ya Katiba na
Msaada wa Kisheria, ili kuisaidia jamii kupata haki.
Alieleza kuwa,
wamekuwa wakiisaidia Idara hiyo, kusudi iwasaidie na kuwawezesha wasaidizi wa
sheria, ambao wanafanyakazi moja kwa moja na jamii husika.
Akizungumzia
wiki ya msaada wa kisheria, alisema ni siku maalum kabla ya kilele, ili taasisi
za watoa msaada wa kisheria, kukutana na makundi kuyaelimisha.
Mwanasheria kutoka
Afisi ya Mwanasheria mkuu Zanzibar ofisi ya Pemba Safia Saleh Sultan, alisema
dhana ya utoaji wa msaada wa kisheria, imo ndani ya katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984.
Kwa upande
wake Afisa Ustawi wa Jamii Rashid Said Nassor, aliwataka wanafunzi hao,
kuwafichua wanaoendesha vitendo vya usafirishaji haramu, wa binaadamu.
Akiwasilisha
mada ya athari za dawa za kulevya, afisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na dawa za Kulevya Pemba, Ahmed Khamis Kombo, alisema sheria mpya nambari
8 ya mwaka 2021 imeongeza makali zaidi.
‘’Kwa mfano dawa
za kulevya zikikutikana ndani ya nyumba, kisheria inataifisha, hata chombo
mfano gari, piki piki, mashua inakuwa mali ya taifa,’’alieleza.
Akilifunga kongamano
hilo, Afisa Dhamana wa Chuo cha taifa cha Zanzibar ‘SUZA’ tawi la Benjamin Walliam
Mkapa Pemba, Idrissa Khamis Sabour,
alisema kongamano hilo, limewaamsha walio wengi, kupata uwelewa wa kisheria.
Wiki ya
msaada wa kisheria Zanzibar ilizinduliwa Juni 24, 2024 na Waziri wa Nchi Afisi,
Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman.
Hii ni wiki
ya tano wa Msaada wa Kisheria Zanzibar, ambapo ujumbe wa mwaka huu ni ‘tumia teknologia kurahisisha upatikanaji wa haki’’ na mgeni
rasmi wa kilele hicho anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Mwisho
Comments
Post a Comment