MICHUANO ya soka
ya ligi daraja la kwanza kanda ya Pemba, imendelea tena jana, kwa timu ya Wawi
star, kuwafariji washabiki wake, baada ya kuiadabisha timu ya Fufuni Sports Club
‘FFC’ kwa mabao 3-0.
Mchezo huo
uliohudhuria na washabiki wengi kiasi, ulipigwa uwanja wa Ngere ngere Jeshini,
majira ya saa 10:30 jioni, huku kila timu ikisaka alama tatu muhimu, katika
michuano hiyo.
Wawi star,
ilishuka dimbani humo ikiwa na njaa la alama, baada ya mchezo uliopita,
kutandikwa mabao 2-0 na timu ya Mila, huku FFC ikiwa na kumbu kumbu ya kushinda,
mchezo uliopita mbele ya Mgogoni star.
Wawi star, ambayo
ilionekana na hamu ya ushindi, nusura dakika 29, ilijipatie bao la kuongoza,
baada ya kutokezea piga nikupige langoni mwa FFC, na kisha shuti la nahoza wao
Azhar Mbarouk, kuokolewa na mlinda mlango.
FFC, walijibu
shambulizi hilo dakika nne baadae, baada ya mpira aliounza mlinda mlango wao na
kumfikia mshambuliaji Habib Said, nae kugawa pasi kwa Yassiri Seif, na kuachia
shuti, lililokuwa chakula mbele ya mlinda mlango wa Wawi star, Omar Mzee.
Dakika 37,
Wawi star walijipatia bao la kuongozwa lililowekwa wavuni kwa njia ya tuta na nahoza
Azhar Mbarouk, baada ya walinzi wa FFC kucheza madhambi ndani ya eneo la 18,
Zikiwa zimebaki
dakika tano kabla ya mchezo kwenda mapunziko, Wawi star waliongeza mtaji wa
mabao, safari hii likifungwa na mshambuliaji machachari Suleiman Seif Madeo,
baada ya kuachia fataki katikati ya walinzi na kujaa wavuni.
Kipindi cha
pili, kilianza kwa kasi ya aina yake, huku FFC wakitafuta namna ya kusawazisha
mabao hayo, na Wawi star kuongeza bao, ili kujihakikishia ushindi.
Waliofanikiwa,
walikuwa ni wenyeji wa uwanja huo Wawi star, walioongeza mtaji wa bao la tatu, mnano
dakika ya 83, baada ya mfungaji wao Abdull-nassir Ali, kuambaa ambaa na mpira,
na kisha kuachia kombora, lililotikisha nyavu.
Kwa ushindi
huo, bado timu ya Junguni, ndio inayoongoza ligi daraja la kwanza kanda ya
Pemba, kwa kujikusanyia alama 59, nafasi ya pili ikishikiliwa kwa karibu na na Tekeleza,
yenye alama 58 na wakongwe wa soka Mwenge kwa alama 57.
Kwenye msimamo
huo, ambapo kila timu tayari imeshacheza michezo 27, timu ya Tibirinzi star, inashika
mkia kwa alama 20, ikifuatiwa na Mila FC yenye alama 23 na Dyanoo FC alama 24.
Mwisho
Comments
Post a Comment