NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MASHEHA wa shehia za Wawi na Wesha wilaya ya Chake
chake Pemba, wamesema tayari wameshapata maeneo, kwa ajili ya ujenzi wa ofisi
za masheha, kama agizo la serikali kuu, lilivyowataka kutafuta ardhi kwa kazi
hiyo.
Walisema, kwa sasa wanachosubiri ni serikali kuanza upelekaji
vifaa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo, hasa baada ya maeneo hayo, kuyamiliki
kisheria.
Wakizungumza na mwandishi habari hizi Juni 8, 2024 kwa nyakati tofauti, walisema
tayari maeneo hayo yameshapimwa na taasisi husika, na sasa yako tayari kwa
ajili ya ujenzi wa ofisi hizo.
Sheha wa shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, alisema eneo ambalo
wameshakubaliana na wananchi kwamba lijengwe ofisi, ni milki ya serikali tokea
asili.
Alisema, eneo hilo kwa muda mrefu, wananchi waliamua
kulihifadhi kwa upandaji wa miti mbali mbali, hivyo wakati wowote likitakiwa
kutumika litasafishwa.
‘’Sisi wananchi wa shehia Wesha, eneo la kujenga ofisi kwa
ajili ya sheha tunalo, kilichobakia tunaisubiri serikali kuu, ili ianze
harakati za ujenzi huo,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, sheha huyo wa shehia ya Wesha Haji Mohamed
Ali, alisema ameshapanga siku maalum, kwa ajili ya kuwaita wananchi, kwa kulifanyia
usafi eneo hilo.
‘’Wananchi tumeshapanga siku moja, tufike ili kulifanyia
usafi, kwani tayari wapimaji wameshamaliza kazi yao, na iliyobakia sasa ni kusubiri
ujenzi,’’alifafanua.
Nae sheha wa shehia ya Wawi Sharifa Waziri Abdalla, alisema kwa
sasa eneo la ujenzi wa ofisi, limechaguliwa kuwa ni kijiji cha Vikutani shehiani
humo.
Alifahamisha kuwa, wamebahatika kupata eneo la kutosha kando
ya barabara, ambapo awali wananchi walitaka kuanza harakati, ingawa baada ya
kutoka tamko la serikali, ujenzi ulisita.
‘’Ni kweli wananchi kupitia kamati yangu, walishaanza harakati
za kuomba muongozo wa ujenzi wa ofisi, lakini tukaelezwa kuwa kuna ramani
maalum, kwa ofisi zote za masheha, zinavyotakiwa kujengwa,’’alifafanua.
Aidha sheha huyo, alieleza kuwa anafurahishwa na wazo la Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, la
kutaka kila sheha, kuwa na ofisi ya kisasa.
Alieleza kuwa, anatamani siku ifike na ujenzi huo uanze, ili
iwepo ofisi ya msaidizi wa sheria, mratibu wa wanawake na watoto, kwani
wamekuwa na msaada mkubwa, katika utekelezaji wa majukumu yake.
Msaidizi wa sheria shehia ya Wesha Khadija Said Khalfan,
alisema wazo la ujenzi wa ofisi za masheha ni jema, kwani wamekuwa wakiwahudumia
wananchi barazani au chini ya miti kwa ukosefu wa ofisi.
Mwananchi wa shehia ya Wawi Juma Khamis Omar na mwenzake Maisara
Khamis Juma, waliiomba serikali kuaharakisha ujenzi huo, kwani wamekuwa
wakipata shida, wanapotaka huduma.
Masaidizi wa sheria shehia ya Wawi Fatma Hilali Salim, alisema
ni vyema ukarakishwa ili wawahudumie wananchi wakiwa kwenye sehemu za faragha
zaidi.
Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, akizungumza
hivi karibuni na kamati ya ufuatiliaji wa ujenzi huo, kutoka shehia ya Wawi,
alisema ujenzi wa ofisi hizo utafanywa kwa awamu tofauti.
Mwisho
Comments
Post a Comment