WANANCHI
kisiwani Pemba, wamesema fedha za ahuweni ya UVIKO 19, zilizoelekezwa kwenye
miradi ya wizara ya Afya kisiwani humo, zimetumika vyema, na sasa wanaendelea
kunufaika nazo.
Walisema,
serikali iliweka wazi mgao wa fedha hizo na matumizi yake, ambapo kwa upande wa
Wizara ya Afya na hasa kisiwani Pemba, zilizitumia kwa ujenzi wa hospitali za
kisasa.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi, juu ya kumalizika na kuanza kazi kwa hospitali hizo,
walisema majengo hayo yamekuwa ya kiwango cha juu, ujenzi wake.
Walieleza kuwa,
sasa wameshaachana na majengo ya zamani, ambayo hayakuwa na nafasi, kwa ajili
yao na madaktari wanapotoa huduma kwa wagonjwa.
Maryam Himid
Mjaka wa Micheweni, alisema sasa wamekuwa na nafasi kubwa ya kukaa kumsubiri
daktari, ikilinganishwa na hospitali yao ya zamani.
Kazija Haji Mshamata
wa Konde, alisema sasa wamekuwa na hamu ya kwenda kutafuta huduma kwenye
hospitali ya Micheweni ama Kinyasini, kutokana na ubora wake.
Mwananchi
Haji Vuai Shella wa Wawi, alisema sasa amekuwa akienda kila anapopata hitifalu
ya afya yake, kwani pamoja na uwepo wa majengo ya kisasa, lakini hata huduma
zimeimarika.
‘’Sasa dawa unweza
kupata zote hata kama ni tano ulizoandikiwa, na ukifika kuna sehemu maalum ya
kumsubiri daktari, kwa aina ya ugonjwa unaokusumbua hamchanganyiki kama zamani,’’alifafanua.
Kwa upande
wake Thuwaiba Haji Khamis, alisema hata wodi za wazazi sasa zimeimarisha,
ambapo kuna vitanda zaidi ya vitatu ambavyo vinaweza kutumika kwa wakati mmoja.
‘’Majengo
yale ya zamani, kulikuwa na vitanda viwili, mkiwa wajawazito kuanzia watatu
msubiriane, au wakati mwingine, ilikuwa lazima waazime chumba kisichokuwa na kitanda,
kwa ajili yao,’’alieleza.
Akizungumza na
waandishi wa habari hivi karibuni, Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis
Bilali Ali, alisema wizara hiyo kwa Zanzibar nzima, ilipewa shilingi bilioni
80.1 kwa ajili ya uimarishaji wa huduma za afya.
Alisema, kupitia
fedha hizo pamoja na miradi mingine, kulijengwa hospitali za kisasa za Kinyasini
wilaya ya Wete, Micheweni na Vitongoji kwa wilaya ya Chake chake.
‘’Ujenzi wa
hospitali hizi, ambazo kwa sasa zinaendelea kutumiwa na wananchi, ni miongoni
mwa juhudi za maksudi, za Rais wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi, ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Afisa Mdhamini huyo, alisema wizara pia, imejipanga kuhakikisha inajenga
hospitali za rufaa kila mkoa na kisha kujenga moja ya rufaa kwa Zanzibar.
Baadhi ya
wananchi akiwemo Muhidin Juma Sharifu wa Kinyasini Mkoani, alisema kasi ya Dk.
Mwinyi itawasaidia wao, kupata huduma bora katika vituo vya afya na hospitali
kadhaa.
Aisha Mohamed
Juma wa Tironi, alisema hata wanawake walioko maeneo hayo, sasa wamepata faraja,
baada ya kukabidhiwa kituo kipya cha mama na mtoto.
Akizungumza
hivi karibuni, wakati akiweka jiwe la msingi la nyumba za madaktari zilizopo
Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema anakusudia kuona wananchi wanatapa
matibabu bora.
Alisema, havutiwi
kusikia kuna vifo vya mama na mtoto, vinavyosababishwa na huduma duni za afya,
na ndio maana amekuwa akiongeza idadi ya wataalamu, ili kukabiliana na
changamoto hiyo.
Mwisho
Comments
Post a Comment