NA AMRAT KOMBO, ZANZIBAR@@@@
Maisha ya binaadamu huwa
salama na ya afya njema kama mazingira yanayomzunguka yapo safi na
salama na yanapokuwa yameharibika huwa hatarishi kwake, wanyama, wadudu na
mimea.
Hali hii ndio inayopelekea kusikia kila kukicha wizara ya afya kwa kupitia wataalamu wake mbali mbali
inasisitiz umuhimu wa kuweka mazingira safi ndani na nje ya nyumba zetu,
mitaani, vijijini na katika maeneo ya biashara kama masoko au ya kuuza na kununua
chakula.
Mwanamke amekuwa akionesha uongozi mzuri kwenye jamii zetu
kwa kuanzia kwenye familia na kutokana na jamii yetu, katika miaka ya karibuni
kutotilia maanani sana usafi wa mazingira kumepelekea kujitokeza watu kuongoza
jamii kufanya marekebisho yanayohitajika.
Miongoni mwa wana jamii waliojitokeza kuwa mstari wa mbele kuongoza juhudi za
kutunza mazingira ni mwana mama anyeiingoza Kikundi cha Ulinzi wa Mazingira,
Siwema Mshenga Issa, kutoka Sheiha ya Bubwini Makoba.
Yeye na wenzake walianzisha kikundi hicho kwa lengo la
kuwaelimisha wanawake katika eneo hilo njia nzuri za kulinda mazingira na
kupambana na magonjwa ya mripuko ambayo chanzo chake ni kuruhusu kuzungukwa na
mazingira machafu.
Wakati huo magonjwa ya mripuko yalikuwa yameshamiri katika
eneo lao na yote hii kutokana na kuzungukwa na mazingira machafu.
"Tulianzisha kikundi kwa ajili ya kulinda familia zetu na jamii . Watoto
walikua hawawezi kwenda skuli sababu ya
magonjwa ya tumbo na saa hali kidogo imebadilika, " alisema.
Kikundi kilikuwa na kamati mbili, moja iliyoshughulikia
kufanya usafi maeneo ya juu na ya pili pwani.
‘’ Tulianza na
wanachama 30, lakini sasa tumebaki 26, wanawake 10 na wanaume 16. Upungufu huu
umesababishwa sababu mbali mbali ikiwemo
wengine kufariki ." anasema
Kikundi kilianza na kazi ya kusafisha maji machafu na mitaro
ya kwenye majaa kwa kushirikiana na
madaktari na wasimamizi wa afya.
Kazi za kwanza zilikuwa kuchimbia mashimo ili kuhakikisha
wananchi hawatupi taka ovyo na katika maeneo ya pwani, waliweka doria kwa
kushirikiana na wavuvi. Juhudi hizi zililenga kuzuia uharibifu wa mazingira ya
bahari.
NDOTO YAKE KUWA KIONGOZI WA MAZINGIRA
Tangu mdogo alipenda
kuongoza wenzake wakati akisoma skuli ya msingi kwa kuhakikisha anasimamia
wanafunzi wenzake katika kusafisha mazingira ya skuli. Ndoto yake ilikuwa kuwa
kiongozi katika serikali.
Katika kikundi chao wanakutana na changamoto nyingi, moja
wapo ikiwa kutopata mapokezi mazuri wanapokwenda majumbani kutoa elimu na mara
nyingi wanaowapa usumbufu ni wanaume.
"Bado wanajamii wengi wanamchukulia mtoto wa kike kama
chombo cha starehe.Hii ni changamoto kubwa
tunapo watuma mabinti zetu wa kazi watembee majumbani kutoa elimu."
Alieleza.
Vile vile wapo baadhi ya watu wanaoendelea kutupa taka na
kukata miti ovyo, lakini juu ya hivyo yamepatikana mafanikio, ikiwa pamoja na
kusaidia kuondokana na maradhi ya mripuko.
Aliviomba vyombo vya serikali kushirikiana nao kikamilifu na
kuwapa vitendea kazi vizuri ili kuzilinda afya zao wapofanya usafi.
Sheha wa eneo
hilo, Khamis Subuhi, alionesha
kufurahishwa na kazi ya kikundi hicho na zaidi kwa kumuona mwanamke anasimamia
kukiongoza vizuri katika kazi zake za kila siku.
Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuipa jamii
elimu juu ya umuhimu wa kuwa na mazingira safi ili kujiepusha na maradhi na
kupata mafanikio mazuri zaidi katika maisha ya kila siku.
Alisikitika kuona ufukwe wa pwani umegeuzwa eneo la kutupa
taka na jamii kusahau kuwa huko ndiko
watoto wao wanapopendelea kwenda kucheza na wazee huenda kufanya mazoezi.
Alisema inafurahisha
kuona maeneo yaliyo karibu na hoteli za kitalii yanawekwa katika hali ya usafi,
lakini wana wakijiji bado wapo nyuma katika kuweka mazingira safi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uvuvi Bumbwini Makoba ,Othman Ussi
Machano,ambaye ni mvuvi wa muda mrefu alifurahishwa na kuwepo kwa kikundi hicho
cha ulinzi wa mazingira ya pwani.
Mwakilishi wa Viti Maalumu Mkoa wa Kaskazini Unguja, Panya
Ali Abdallah, alisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira safi ya bahari kwani
mbali ya kusaidia upatkanaji wa samaki pia kutavutia watalii.
"Tukiimarisha fukwe zetu, itatusaidia kupata ongezeko
la wageni katika nchi yetu na itapelekea kupata maendeleo," aliongeza.
Mmoja wa wana kijiji wa hapo, Fatma Ali Kiroboto, alisema wanafurahi kuwepo kwa kiongozi
mwanamke ambae anahamasisha usafi, kwani mwanamke ndio anaetunza mazingira
ikiwa ya nyumbani hadi ya ufukweni.
Mkuu wa Idara Huduma
za Jamii Mazingira na Mipango Miji Baraza la Magharibi A, Tatu Hussein
Abdallah, alisema mwanamke anapaswa kuwa kiongozi kwani ndiye mlinzi mkubwa wa
mazingira.
Alisema anawajua viongozi wanaopambana kuhakikisha jamii inazingatia umuhimu wa kuwa na mazingira mazuri na Siwema ni mmoja kati yao wanaofanya kazi hio kwa uadilifu katika sheiha yake.
Aliitaka jamii kushirikiana naye kuendeleza juhudi za
kikundi chake cha kuwa na mazingira mazuri katika shehia yao.
MWISHO
Comments
Post a Comment