NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WATUHUMIWA wa kesi ya kuua kwa
makusdi, inayowakabili vijana wanne akiwemo Ali Mussa Omar ‘Mkapa’ na wenzake,
wote wakaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake, wamerejeshwa tena rumande, baada ya
Jaji anayesikiliza kesi yao kutokuwepo mahkamani.
Watuhumiwa wingine waliorejeshwa
rumande hadi Januari 23, 2024 ni Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari
Mussa Omar miaka 30 na Yassir Mussa Omar ‘Makababu’ miaka 29, ambao wanatuhumiwa
kumuua kwa maksudi kijana Said Seif Kombo.
Mara baada ya kuwasili mahakamani
hapo wakitokea rumande, walitulia tuli wakisubiri taratibu za mahakama kuu
ziendelee, ingawa Mwanasheria wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka Awamu Zubeir Awamu, alidai kuwa Jaji husika hayupo mahakamani hapo.
Wakili huyo wa serikali,
alimueleza hakimu wa mahkama ya mkoa Chake chake anayeshughulikia makosa ya udhalilishaji
Ziredi Abdull-kadir Msanifu, juu ya dharura ya Jaji husika wa kesi hiyo.
‘’Mheshimiwa Hakimu, ilikuwa
kesi hii leo, inawasilishwa mambo kadhaa ikiwemo ushahidi wa maandishi na idadi
ya mashahidi, lakini kutokana na Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim kutokuwepo mahakamani,
naomba ighairishwe,’’alidai.
Baada ya maelezo hayo, Hakim
Ziredi, alikubaliana na uamuzi wa Mwanasheria huyo wa serikali, na kisha kuamua
shauri hilo litarudi mahkama kuu Januari 23, mwakani.
‘’Mahkama hii kisheria haina
uwezo wa kusikiliza shauri lenu, kwani ni kesi za mahkama kuu, na jaji wenu hayupo,
itabiudi murudi rumande hadi Januari 23 mwaka 2024,’’alisema Hakimu
huyo.
Kwa mara ya kwanza kesi hiyo, ilisomwa
mahakama kuu, Novemba 14, ambapo siku hiyo ikaghairishwa tena hadi Novemba 30,
kabla ya kutakiwa kurudi tena mahakama kuu, Januari 23, mwaka 2024.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka
kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa
kufanya mauwaji hayo ya maksudi.
Ilidai kuwa, wote kwa pamoja,
walitenda kosa hilo Oktoba 16 mwaka 2023, baina ya majira ya saa 7:00 mchana na
saa 11:00 jioni, katika eneo la Machomane wilaya ya Chake chake.
Ilidaiwa kuwa, kufanya hivyo ni
kosa kinyume na vifungu vya 189 na 190 vya sheria nambari 6 ya mwaka 2018
sheria ya Zanzibar, iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi.
Hata hivyo watuhumiwa hao,
waliieleza mahakama hiyo kuu kuwa, wanaewakili katika kesi yao hiyo, ingawa kwa
siku ya kwanza, hakuweza kufika mahakamani, kutokana na sababu mbali mbali.
Wakati huo huo, Jaji Ibrahim
Mzee Ibrahim, aliwaambia watuhumiwa hao kuwa, kwa mujibu wa sheria za Zanzibar,
kama watatiwa hatiani, adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.
Mwisho
Comments
Post a Comment