Skip to main content

WANAKONGAMANO: ‘’TUITUMIENI TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUTOA MAONI KWA SHERIA MUITAKAYO’

NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@

WANANCHI kisiwani Pemba, wameshauriwa kuitumia Tume ya Kurekebisha sheria wanapokuwa na vikao vyao vya kupokea maoni, ya kutaka kurekebishwa sheria, ili kuwa na sheria zinazoendana na dunia ya sasa.

Ushauri huo umetolewa na wanakongamano la siku moja, la kuelekea siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, lililoandaliwa na Jumuiya ya wasaidizi wa sheria, wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’, na kufanyika ukumbi wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba.

Walisema, ni vyema wananchi wanapokutana na Tume hiyo, kuacha jazba na kuzitolea maoni sheria, ambazo zimeshapitwa na wakati, ili kueleza wanavyotaka ziwe, kwa mujibu wa mazingira ya sasa.

Mjumbe wa Jumuiya ya TUJIPE Pemba, Sheikh Abdalla Nassor Maulid, alisema utoaji wa maoni katika tume hiyo, ni njia muhimu kwa jamii kuwa na sheria rafiki.

‘’Tume ya kurekebisha, hupita katika maeneo yetu, sasa sisi wananchi tuitumieni ili kutoa maoni, juu ya sheria ambayo tunaihisi imeshapitwa na wakati,’’alieleza.

Kwa upande wake Abdull-atif Abdalla Salim kutoka ofisi ya Mufti Mkuu, alisema moja ya eneo ambalo, linaendelea kuwakosesha haki wanawake na ucheleweshaji wa mirathi.



‘’Ijapokuwa hata sheikh, aliyepo mtaani anaweza kurithisha, lakini ni vizuri zaidi kuitumia Kamisheni ya Wakfu, kwa ajili ya kurithishwa maana huko hupata waraka ambao unaondoa migogoro,’’alieleza.

Kiongozi wa dini ya kikiristo Robart Migua Ndalami, alisema ili uhalifu ukiwemo wa wizi na udhalilishaji upunguwe, wanaobainika wakijirejea kufanya makosa, waadhibiwe mara mbili.

Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba, Bakari Omar Ali, alisema CHAPO imo katika kuelekae siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, kwa kukutana na viongozi wa dini na wanaharakati wiengine.

Alieleza kuwa, siku hizi ni muhimu kwa jamii na wadau wingine kuangalia mafanikio na changamoto, katika kutomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji.



‘’Kongamano hili ni muhimu mno kwetu, kuona wapi tumefanikiwa na wapi tunahitaji kuongeza nguvu, ili kuhakikisha kundi la wanawake na watoto, linabaki salama bila ya vitendo hivyo,’’alieleza.

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alisema nguvu za pamoja bado zinahitajika katika jamii, ili kuona matendo hayo yanakoma.

Hata hivyo ameikumbusha jamii, kuendelea kuwatumia wasaidizi wa sheria wanapokuwa na changamoto za kisheria, ikiwemo kukwama kwa kesi Polisi, kuchelewa kuchukuliwa maelezo baada ya tukio kutokea.




Alieleza kuwa, zipo taarifa kuwa, huwenda sheria ya Mila inayohusu mavazi ya hapa Zanzibar ya tokea miaka ya 60, kufanyiwa marekebisho, ili kuona inaendana na mazingira ya sasa.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa CHAPO Kassim Ali Omar, alisema malezi ya pamoja kwa jamii, ndio msingi mkubwa wa kurejesha heshima na nidhamu kwa watoto.

Hata hivyo, aliwakumbusha wananchi kila mmoja kuwa mlinzi kwa mwenzake, juu ya mjanga yaliomo ndani ya jamii, ikiwa ni pamoja na dawa za kulevya na vitendo vya ukatili na udhalilishaji.

Mapema Masaidizi wa sheria Jimbo la Chake chake Riziki Ali Hamad, alisema wakati umefike sasa, kuwepo kwa kamati maalum ya kuhamasisha urithishwaji mara baada ya kifo kutokezea.

Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Chake chake Pemba CHAPO, inaendelea na mikutano na makongamano yake, ya kuelekea siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, ambapo inakutana na makundi mbali mbali.

                                    Mwisho   

Comments