NA AMRAT KOMBO, ZANZIBAR@@@@
KILA mwanadamu huwa na malengo katika maisha na huhitajika
mipango na ujasiri kuweza kuitekeleza.
Ujasiri ni silaha nzito kuibeba, lakini ina faida kama
utakuwa na sulubu ya kuibeba.
Neno ujasiri limebeba maana kubwa kwenye tafsiri ya mtu
aliefanikiwa katika maisha yake.
Mmoja wa wanawake aliyeweza kupata mafanikio kutokana na kuwa na ujasiri ni Zawadi Amour Nassor .
Mwana mama huyu, ambaye ni mtoto wa kwanza katika watoto tisa
wa familia yao,amezaliwa 1978 katika
kijiji cha Konde Pemba na kupata elimu yake ya msingi katika Skuli ya
Kinyasini, Unguja, mwaka 1991.
Aliendelea na elimu ya sekondari katika Skuli ya Konde mwaka
1994 na kupata elimu ya juu katika chuo cha Zanzibar Muslim College, Mazizini
hadi ngazi ya stashahada na shahada.
Vile vile amesomea uwalimu katika Chuo Kikuu Huria Tanzania
‘OUT’.
Alisomesha katika skuli ya msingi za Pangale na
Konde"A" kuanzia mwaka 2000 hadi 2020.
Jasiri huyu alianza kuwa mwalimu wa skuli ya msingi ya Konde
‘A’ na kuwa Msaidizi wa Mwalimu Mkuu katika mwaka 2015.
Kuanzia mwaka 2018
alikuwa karibu na chama cha Wandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) na kupata
mafunzo ya masomo mbali mbali, ikiwa pamoja na kupiga vita vitendo vya
udhalilishaji.
Vile vile alipata
mafunzo ya uongozi kwa mwanamke ambayo yalimjenga hadi kuingiwa
ushawishi wa kujiunga na siasa katika mwaka 2019.
" Nilikuwa mjumbe katika Chama Cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania –Zanzibar (TAMWA) katika kisiwa cha Pemba.
Nilipata mafunzo mengi, yakiwemo ya kuwa jasiri katika
kupigania vitendo vya udhalilishaji,’’ alisema.
Akiwa na TAMWA, Bi Zawadi ambae sasa ni Mwakilishi wa Jimbo
la Konde, alisema alipata mafunzo ya uongozi kuanzia mwaka 2019.
Malengo yake baada ya kuiva kiuongozi na kugombea nafasi ya
uwakilishi katika Jimbo la Konde, ingawa wapo waliomshawishi agombee viti
maalum.
Kwenye kinyang’anyiro hicho walikuwa wagombea 11, kati yao
wanawake watatu na katika harakati za kugombea na jina lake lilirudi kuwa
mgombea.
Alieleza kuwa wazazi wake hawakupenda aingie katika siasa
kwa sababu ya hofu angebadilika kitabia
na mwenendo wake wa maisha.
Hata hivyo, baba yake
alimridhia aingie kwenye siasa, lakini mama yake alikuwa na wasiwasi kwa
kuhofia tabia ya kujengeana uadui,"alisema
Hivi sasa Bi Zawadi yupo mstari wa mbele kupinga
udhalilishaji na upo wakati aliibua taharuki ya kudhalilishwa wanafunzi wa
darasa la sita wa Skuli ya Msingi ya
Konde.
‘’Niliifuatilia kesi ya mwalimu wa madrasa kuwaingia
wanafunzi na hapo mwanzo Polisi na baadhi ya wazazi hawakunielewa mpaka kesi
ilipofikishwa mahakamani,’’aliongeza.
Akiwa skuli, Bi. Zawadi alifundisha watoto jinsi ya
kujilinda na vitendo viovu na kujitambua.Alifanikiwa kuwapata watoto 35
waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Alipowaibua watoto hao, jamii iligawaika makundi. Wapo
waliomuona amefanya jambo jema, na wengine walimtenga na kumsema vibaya, kwa
kule kufanya kazi yake vizuri.
‘’Ukifuatilia jambo ovu ili liondoke, wao wataokuunga mkono
na wengine kukulalamikia, lakini hayo sikuwajali, maana nilishaelezwa na
mwalimu wa TAMWA-Zanzibar kuwa
yatajitokeza,’’ alisema.
ALIPOINGIA KWENYE SIASA
Alipoingia kwenye siasa aliwafuata watu maarufu na magwiji
wa siasa kuwaomba wamsaidie na kupata mapokezi tafauti.
‘’Yuko mzee ambae sasa ni marehemu ndio mtu pekee
aliyonionesha njia na kuniambia niwe makini kwenye siasa,’’alisisitiza Bi.
Zawadi.
ALisema aligundua ni kwamba
wakati mwengine adui wa mwanasiasa ni mwanasia mwenzake, wakati mwengine
wa chama, shehia , wadi, jimbo au mkoa mmoja.
Kilichompa nguvu Bi. Zawadi, mbali ya familia yake ni kuona
baadhi ya ya marafiki zake wapo pamoja.
ZAWADI NA UWAKILISHI
Alisema mfuko wa jimbo
haukidhi matakwa ya wananchi na hili halieleweki vizuru na jamii.
Alisema anaamini mambo aliyoyafanya katika jimbo lake ni
karibu kwa asilimia 90 ya mambo aliyoahidi wakati wa kampeni ya uchaguzi.
Ahadi hizi ni pamoja na kuwapatia waanchi maji safi na
salama kwa kuwajengea visima nane.
Vile vile alisambaza huduma ya nishati ya
umeme,ameshajihisha wanafunzi kuweka kipaumbele katika sekta ya elimu na
kuwasaidia kwa kuwapelekea vifaa vya kusomea, kama vitabu kompyuta.
"Nilikuja na mradi unaosema ‘tokomeza ziro na kuengeza
ufaulu kwa kidato cha sita.Nikawapatia mafunzo ya ujasiria mali vijana wa kike
10 katika sekta ya ushoni,’’alieleza.
Aliwapatia vijana 43 mafunzo ya udereva katika chuo cha
‘KST’ Pemba kwa lengo la kuja madereva wazuri, wapo vijana 70 waliopewa mbinu
za kujiajiri, kupitia fursa zilizopo
Pemba.
Kwenye afya, Mwakilishi huyo
aliwapelekea daktari wa magonjwa wa moyo katika hospital ya Konde pamoja
na gari ya kubeba wagonjwa.
Katika michezo alisaidia kusajili timu 26 katika ligi ya
Shirikisho la Kanda Zanzibar (ZFA) na kutumia shilingi milioni 4.4 na kuendelea
na matengenezo ya uwanja wa mpira wa Konde.
Bi. Zawadi alisema kinachowakwaza wanawake kutoingia
majimboni na kukimbilia viti maalum ni pamoja na hofu ya moyo na kuamini
mwanamke akiwa kiongozi anapotosha maadili yake.
Alisema bado dunia imetawaliwa na mifumo dume, ambayo
humtenga mwanamke au wakati mwingine kujiona hana haki ya kuingia kwenye safu
ya uongozi.
WANAOMFAHAMU ZAWADI
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi. Salama Mbarouk Khatib,
alisema mkoa huo umebahatika kupata mafanikio makubwa kwa sababu ya kuongozwa
na watu kama Bi. Zawadi.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, alisema
mwakilishi wa Konde ni mmoja wa viongozi anaowafuatilia kwa utendaji na
kujiamini kwao.
Mbunge wa viti maalum kwa mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi. Asia
Sharif Omar, alisema Mwakilishi wa Jimbo la Konde, Zawadi Amour Nassor, ni
shujaa na jasiri kwenye uongozi.
Maray Haji Khamis wa Vilima Vitatu Konde, alisema sasa
wanaendelea kunufaika na huduma ya maji safi na salama, baada ya Jimbo lao
kumpata Mwakilishi makini.
‘’Ametusaidia kwenye ujasiriamali, kwanza kwa mafunzo pili kutupatia mtaalamu kutuelekeza namna ya kuzalisha bidhaa bora na zinazokubalika katika soko,’’alisema.
Hivi karibuni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, DK. Hussein Ali,wakati alipokuwa na ziara mkoa wa kaskazini Pemba,
aliwataka wananchi kuendelea kuwaamini viongozi wao.
‘’Tunao wawakilishi na madiwani wachapakazi, sasa hatuna
sababu ya kutokuwarejesha tena madarakani kwenye kila uchaguzi,’’alisema Dk.
Mwinyi.
MWISHO
Comments
Post a Comment