CHUO cha Utawala wa Umma Zanzibar ‘IPA’
kimegundua sababu mbali mbali, zinazowafanya watumishi wa umma, kuhama sehemu moja
kwenda nyingine, ikiwemo mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
IPA imegundua sababu nyingine kuwa ni,
miundo ya kiutumishi, maslahi na ndoa kwa watumishi wanawake na wanaume, kwa
kumfuata mwenzake sehmu alipo kimakaazi.
Hayo yameelezwa leo Disemba 8, 2023, na Mkuu wa Divisheni ya
Utafiti na Ushauri Elekezi kutoka ‘IPA’ Haji Jumbe Haji, wakati akizungumza
kwenye uwasilishaji wa matokeo ya awali wa tafiti nne walizozifanya, kwenye
hafla iliyofanyika ukumbi wa Chuo, hicho mjini Chake chake.
Alisema, sababu hizo na nyingine, zinazowafanya
watumishi wahame kutoka sehemu moja kwenda nyingine, wakati mwingine huathiri
mtiririko mzuri wa kazi za sekta ya umma.
Alisema, tafiti hizo ambazo walizifanya katika
mwaka wa fedha wa 2020/2021, zilichukua takriban miezi sita hadi kukamilika kwake,
ambapo watendaji mbali mbali wa sekta za umma za Unguja na Pemba, walihojiwa.
‘’Hama hama ya watumishi wa umma, imekuwa
ikijitokeza kwa kasi kadiri pia mabadiliko ya kiutendaji yanavyowekwa mazingira
rafiki, ikiwemo vifaa vya kisasa,’’alifafanua.
Alizitaja tafiti hizo kuwa ni ‘uanzishwaji na
utekelezwaji wa mifumo ya kielektroniki katika utumishi wa umma, usalama na
utunzaji kumbu kumbu za serikali, uwezo wa serikali za mitaa, katika kutoa huduma
kwa jamii na kuangalia sababu za watumishi wa umma kuhama kutoka sehemu moja
kwenda nyingine.
Akifungua hafla hiyo, Afisa Mdhamini wizara
ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba, Halima Khamis Ali, alisema
hakuna kitu ambacho, kinaweza kuleta mageuzi pasi na kufanyika utafiti.
Alisema, kikao hicho ni muhimu kwa wadau
hao wa Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar ‘IPA’ kupata kusikiliza utafiti huo na
matokeo ya awali na kisha, kutoa maoni yao, kwa ajili ya kuimarisha zaidi.
Alieleza kuwa, moja ya kazi kubwa ya IPA,
ni kuishauri serikali kuu, juu ya uimarishaji katika sekta ya umma, ili kuhakikisha
mifumo iliyopo inakuwa rafiki, kwa watumishi wa umma wa kada zote.
‘’Utumishi wa umma ni rasiliamali muhimu
ndani nchi yetu, na ndio maana IPA, kimepewa jukumu la kuhakikisha wanachoona
hakiendi sawa, ni kuishauri serika na kufanyiwa mapitio ya haraka,’’alieleza.
Alifahamisha kuwa, mifumo ya serikali kama
ya ukusanyaji mapato, uendeshaji wa shughuli za kila siku ‘e-government’,
zan-malipo, uhifadhi wa kumbu kumbu, zinahitajika kuangaliwa kila baada ya
muda.
Hata hivyo, Afisa Mdhamini huyo, aliupongeza
uongozi wa IPA, kwa kutekeleza majukumu yao mbali mbali, licha ya changamoto zinazowakabili.
Aidha aliwataka wadau hao, kutoa maoni yao
ambayo yatasaidia kuimarisha utafiti huo, ambao baadae utawasilishwa serikali kuu
kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo cha
Utawala wa Umma Zanzibar ‘IPA’ tawi la Pemba Juma Haji Juma, alisema uwasilishaji
wa matokeo hayo ya awali, na maoni ya wadau hao, yatasaidia kuongeza ufanisi
katika utafiti wao.
Mwisho
Comments
Post a Comment