NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAVUVI wa dagaa wa shehia ya Wesha wilaya
ya Chake chake Pemba, wamekumbushwa kujiwekea mazingira ya usafi, kuanzia nguo
wanazovaa, madau yao pamoja na vyombo vyingine wanavyotumia, ili kuliongezea
thamani dagaa lao.
Ushauri huo umetolewa leo Disemba 6, 2023 na Mratibu wa Mradi
wa Kuimarisha Jamii kwa kuzingatia Ikolojia na shughuli za kijipatia kipato,
kwa wavuvi wadogo katika eneo la hifadhi ya mkondo wa Pemba ‘’SAPPHIRE’ Aisha
Abdalla Rashid, alipokuwa akifungua mafunzo, kwa wavuvi hao, yaliyofanyika
ukumbi wa Manispaa ya Chake chake.
Alisema, kwa sasa ofisi ya Makamu wa Kwanza
wa Rais Zanzibar kupitia Idara ya Mazingira, chini ya mradi huo wa ‘SAPPHIRE’
imeamua kukutana na wavuvi na waanika dagaa, ili kujengea uwezo kwa lengo la
kuongeza thamani.
Alieleza kuwa, moja ya jambo hilo ni usafi
wa wavuvi, kuanzia nguo wanazovaa wakati wanapokwenda kwenye shughuli zao za
uvuvi, madau yao na ndoo wanazotumia.
‘’Usafi wa bidhaa ya dagaa kavu au bichi,
huanzia kwa mvuvi mwenyewe, na kisha usafi huo, uendelee kwa mkaushaji ama
mchemshaji wa dagaa kabla ya kulipelekea sokoni,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Mratibu huyo wa
mradi wa ‘SAPPIRE’ alisema mradi huo, ambao unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa
Mataifa na Uhifadhi wa Mazingira ‘UNEP’ moja ya malengo yake, ni kuandaa mpango
shirikishi wa rasilimali bahari.
‘’Lengo jingine ni kuendeleza uhifadhi wa
eneo la Mkondao wa Pemba PECCA, pamoja na kusaidia shughuli mbadala za
kujipatia kipato kwa waanikaji na wavuvi wa dagaa,’’alifafanua.
Mapema Kaimu Afisa Mkuu Idara ya Maendeleo ya
Uvuvi na Mazao ya Baharini Pemba Mayasa Hamad Ali, wakati akitoa mada ya njia ya
bora za uanikaji dagaa, alisema ziko njia mbali mbali, moja wapo ni utumiaji wa
moshi.
Alisema, njia hii hutumia magamba ya miti
isiyokuwa na sumu, ambayo dagaa huwekwa juu, na moshi mwepesi mwepesi kupenya
kwenye dagaa, na kukauka taratibu.
‘’Na njia hii hasa wakati mwingine, hutumika
sana kipindi cha mvua, kwa kuhofia dagaa lisiharibike kwa kukosa jua, tena wapo
wateja wanalipenda zaidi hili, kuliko la kukausha kwa jua,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, mtoa mada huyo
alieleza kuwa, njia nyingine ambazo zinakubalika katika uanikaji wa dagaa, ni
kuchemsha kwa maji na chumvi na kisha kulianika kwa jua.
‘’Njia hii ni nzuri, lakini lazima
waanikaji wazingitie usafi, ikiwemo kabla kulikosha vyema na kuondoa taka taka
na chango za wadudu, ili likishakauka, lipendeze kwa mlaji,’’alieleza.
Hata hivyo alifafanua kuwa, haishariwi
kulianika dagaa kwenye sakafu chafu na inayongia mavumbi na kuruhusu wanyama
waharibifu, kwani hupoteza thamani kwa wateja.
‘’Hakuna uhusiano wowote, kati ya dagaa
kavu na kujaa mavumbi mavumbi kwani, baadhi ya wateja hupendelea kula kama
lilivyo, hivyo lazima tuwalinde wateja wetu,’’alifafanua.
Mwanikaji dagaa Salim Juma Omar, alisema moja
ya sababu za dagaa kuanza kuharibika na kupoteza thamani, ni wavuvi kulichelewesha
kulipeleka sokoni.
‘’Wakati mwingine, baadhi ya wavuvi
hilichanya dagaa walilolivua saa kadhaa zilizopita na jipya, hapo ndio athari
huanza kujitokeza na kusababisha athari kwa wateja,’’alieleza.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa dagaa Sabra
Massoud Ali, alisema changamoto kubwa inayowakabili, ni ukosefu wa wateja wa
uhakika, ambapo wakati mwingine, hukaa na dagaa zaidi ya miezi mitano bila ya
kuliuza.
Mafunzo kama hayo, tayari wameshapewa wavuvi na waanikaji dagaa wa shehia ya Ndagoni wilaya ya Chake chake, pamoja na kukabidhiwa vifaa kama vile chanja za kisasa za kuanikia dagaa, ndoo na vyombo maalum ya kuchemshia dagaa.
Mwisho
Comments
Post a Comment