NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WATU wasiojulikana, wamevamia na
kuiba Kaa na Vitango bahari, waliyokuwa yakifugwa na wanaushirika wa
‘yashasemwa’ uliopo shehia ya Mtambwe kusini, wilaya ya Wete Pemba.
Watu hao kwa
nyakati tofauti, wanadaiwa kuiba Kaa 80 kati ya 120 waliyoyaingiza na Vitango
bahari kuibiwa yote 1,000 kwa nyakati za usiku.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi, viongozi wa ushirik huo, walisema wizi huo
umefanyika miezi mitano, baada ya kuweka vifaranga hivyo, kwa ajili ya ufugaji.
Msaidizi wa
Mwenyekiti wa ushirika huo Jabir Saleh Jabir, wamepatwa na mshangao mkubwa,
baada ya kupokea taarifa za kuibiwa, kwenye shamba lao.
Alisema,
walitumia gharama kubwa kuanzisha maeneo hayo husika, kwa ajili ya ufugaji wa vitango
bahari na Kaa, ingawa watu wasiowafahamu, waliwarejesha nyuma kwa kuwaibia.
‘’Na sisi ni
ushirika ambao tuna nia ya kuvuna matunda ya uchumi wa buluu, na
tulishajikusanya na kuunganisha nguvu zetu, lakini wengine waliamua kuturejesha
nyuma,’’alilalamika.
Mshika fedha
wa ushirika huo, Mafunda Abdalla Omar alisema, pamoja na kuibiwa kwa Vitango
vyao bahari 1,000 kwa sasa wameamua kuanzisha tena.
‘’Kwa sasa
tumeanzisha tena ufugaji wa Vitango bahari 50 baada ya vile vya awali kuibiwa, lakini
bado tunahofu na changamoto kama hiyo tena, ingawa hatuvunjiki moyo,’’alieleza.
Alieleza
kuwa, kwenye mradi wa ufuji Kaa, walianza na mtaji wa shilingi 600,000 ikiwa ni
mkopo maaluma kwa ajili ya wajasiriamali, kupitia sera ya uchumi wa buluu.
‘’Kwa wakati
huo, tulinunua vifaranga vya Kaa 100 kwa shilingi 400,000 na kununua Kaa
wakubwa 20, kwa shilingi 200,000 ili kuwawek kwenye ‘zoo’ malum, ingawa baada
muda waliibiwa,’’alifafanua.
Mshifa fedha
huyo alisema, kama sio kuibiwa kwa Kaa hao, wangepata wastani wa shilingi
milioni 1, kwani kila Kaa wawili hufikia kilo moja, ambapo ni shilingi 17,000.
Hata hivyo
Mshika fedha huyo alieleza kuwa, bado hawajavunjika moyo, na ndio maana
wameanzisha utaratibu wa kwenda kutafuta wenyewe vifaranga vya Kaa na vitangi,
ili kuongeza kipato chao.
Mwanachama
wa ushirika huo Neema Abdalla Omar, alisema amevutiwa mno na kazi ya ufugaji wa
Kaa na vitango, kwani anaufahamu kabla ya kuingia kwenye ushirika huo.
Aidha
mwanachama huyo alisema, bado hajavunjika moyo na wizi uliofanyika kwenye
shamba lao la ufugaji Kaa na Vitango habari, huku akiamini iko siku
watafanikiwa.
Sheha wa
shehia ya Mtambwe kusini Othman Ali Khamis, alikiri kuwepo kwa tabia ya wizi,
kwenye mashamba ya wafugaji wa samaki, kaa na vitango bahari.
Alieleza kuwa,
ni vyema kwa wanaushirika wote waliomo shehiani humo, kushirikiana kwa karibu,
ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi katika mashamba yao.
‘’Serikali
imeshajitahidi kutekeleza ahadi zake za kutoa mikopo na vifaa, kwa ajili ya
kuimarisha sera ya uchumi wa buluu, na changamoto nyingne wananchi wazimalize
wenyewe,’’alifafanua.
Ushirika huo
wa ‘Yashasemwa’ unaojishughulisha na ufugaji wa Kaa na Vitango bahari uliopo
shehia ya Mtambwe kusini, umeanzishwa miezi minane iliyopita, ukiwa na
wanachama 15, wanawake wakiwa saba.
Mwisho
Comments
Post a Comment