NA MARYAM SALUM, PEMBA@@@@
UTAMADUNI wa uvaaji kanga ya shingoni,
ama kwa lugha Micheweni ‘kinje kuku’ umepotea kwa kasi.
Kizazi cha
sasa cha Micheweni, na hasa watoto wa kike ambao ndio walengwa wa utamaduni,
wameanza kuupa kisigo.
Wakionekana,
kuachana na vazi hilo, na sasa wakivaa nguo nyingine ambazo wanaona zinawastiri
hasa sehemu ya kifuani.
Hiyo ni kutokana na karne ya sasa na utandawazi
jinsi ulivyokua, ndipo watoto wa kike wa Micheweni takribani kwa asilimia kubwa
kuacha utamaduni huo.
Vazi hili
lilikua linavaliwa sana na watoto, wengi wao wanaishi vijijini, lengo hasa la
kinje kuku, ni kuwastiri watoto hao wa kike sehemu ya kifuani, hasa wakianza
kutanuka kifua.
Vipo vijiji
vyengine vingi katika Mkoa huo ambavyo
watoto wa kike walikua wanavaa vazi hilo kama utamaduni wao, lakini mwandishi
wa makala hii aliamua kwenda kwenye kijiji cha Kwale Wilaya ya Micheweni
kuzungumza na wazee.
Wilaya ya Micheweni ni Mkoa unaoongoza kwa
masuala mbali mbali ya utamaduni ikiwemo vazi la kanga ya shingo yani kinje kuku,
upishi wa maandazi ya kombo alawi na mengine mengi.
Hayo si
maneno ya mwandishi wa makala hii bali ni maneno ambayo yalitoka kinywani mwa
mama Saada Said Kombo miaka 70 mkaazi wa Kwale shehia ya Majenzi Wilayani humo.
Anasema kuhusu
suala la vazi la kanga ya shingo kwa jina jengine kwa baadhi ya vijiji ‘kinje
kuku’ ni miongoni mwa utamaduni wao ambao ulikua na kipaumbele kwa jamii ya Kwale
na Micheweni kwa ujumla.
VAZI HILI WALIPATA WAPI
Anasema
kwamba vazi la kanga ya shingo kwa mtoto wa kike ni urithi kutoka kwa wazazi
wao, na kwa wakati huo, ulikuja kutokana na kuwepo kwa uhaba wa nguo za kuvaa hapo
zamani.
Aneleza kuwa
kutokana na kulikua na uhaba wa mavazi (nguo) hapo zamani ndio maana,
ikapelekea wazazi kuwalazimisha watoto wao wa kike kuvaa vazi hilo ili waweze
kujistiri.
Maana hapo
zamani vazi hilo kwa watoto wa kike katika kijiji chao, lilikua ni vazi la
lazima na hakukua na mtoto yeyote aliyekuwa akithubutu kukataa kuvaa vazi hilo.
Kwani kwa
wakati huo, kije kuku lilikua ndilo vazi lenye stara zaidi kuliko vazi jingine lolote, kwa watoto
wa kike.
Aisha Makame
miaka 60 nae anasema kuwa zamani watoto wa Micheweni kwa ujumla vazi hilo ndio
vazi pekee ambalo likivaliwa na rika kwa watoto wa kike walio na umri mdogo.
Anaeleza
kuwa Micheweni na vijiji vyake vyengine jirani vya wilaya hiyo, anasema ilikuwa
lazima kumuona mtoto wa kike hakuvaa vazi hilo.
‘’Usipovaa
vazi hilo kwa wakati huo, ukionekana kama unatembea uchi, hata kama umevaa
kanga bei bui na vazi jingine, lakini vazi la heshima lilikuwa kanga ya
shingoni,’’anasimulia.
Anaeleza
kuwa lengo jengine katika uvaaji wa kanga ya shingo kwa mtoto wa kike jamii ya Micheweni,
ni pale tu anapoanza kuota maziwa (machuchu) kujistiri kwa vazi hilo, ili
kifuani wengine wasijue kinachoendelea.
“Mtoto wa
kike wa jamii yetu ya Micheweni hapo zamani, alikua hana hiari katika kuvaa
vazi hili, ilikua ni amri na sio ombi,’’anasimulia.
Anaeleza kuwa
kutokana na kuacha asili yao ya kuvaa vazi hilo na mambo mengine mbali mbali ya
utamaduni wa jamii zao ndipo kupelekea mambo mbali mbali ya ushawishi ambapo
mwisho wa siku hupelekea hata kubakwa.
“Vazi la kanga ya shingo kwa mtoto wa kike kwa
sasa vijana wanadai kwamba si vazi zuri la kuvaa, haliendani na hadhi iliyopo
sasa katika ulimwengu wetu tulionao wa kimtandao, sasa mambo yamekua ni tofauti
na hapo zamani,’’anasema.
Sharif Massoud Hamad mkaazi wa Majenzi
Micheweni mwenye miaka 60 anaeleza kuwa kutokana na kupotea kwa vazi hilo
kumekuwa na utofauti mkubwa kwenye suala la kujistiri.
“Utofauti
upo baada ya vazi la kanga ya shingo kupotea, moja ni kutokana na vijana wetu
wa kike kuonekana kirahisi kwa baadhi ya maungo yao ikiwemo kifua baada ya
kutoa chuchu (maziwa),’’anasema.
“Ingawa
kulikua na uhaba wa upatikanaji wa nguo kwa kizazi cha zamani, lakini hata kwa
wale waliokuwa wakipata nguo hakuna aliyekua akithubutu kuvaa kanga ya kiuno,
kutokana na kuonekana kua ni tabia mbaya,”anaeleza sharif.
Kama
hujaolewa mtoto wa kike yoyote wa jamii ya Micheweni hakithubutu kuvaa kanga
kiunoni, hadi pale atakapofika kwa mume wake.
Anasema kuwa
kwa sasa vazi hilo limepotea kabisa, sasa mtoto akiachishwa tu huanza kuvaa
kanga ya kiuno ncha kabisa na hakuna ambae ataweza kumrejesha ama kumrekebisha.
SABABU
YA KUPOTEA KWA UTAMADUNI HUO
Mayasa Haji Hamad anasema kupotea kwa uvaaji
wa kanga ya shingo, kama utamaduni wa wazaliwa wa wilaya ya Micheweni, kwanza ni
vijana wenyewe kujenga dhana mbaya juu ya vazi hilo.
Anasema
wazazi wa sasa kushindwa kusimamia utamaduni huo kama ilivyo kwa maeneo mengine
mbali mbali, jambo ambalo linasabisha athari.
“Sasa hivi kumeonekana kabisa kupotea kwa
amlezi ya pamoja kwa watoto kama ambavyo yalikuwepo zamani, sasa hivi kila mtu
na mwanawe hakuna kusaidiana ulezi,” anasema.
NINI KIFANYIKE KUREJESHA UTAMADUNI
HUO?
Wazazi na
walezi wa Micheweni wanasema kwanza kuwepo na ushirikiano wa pamoja katika
suala la malezi, hapo ndipo jamii itaweza kubaki na kuendeleza yale mambo yao mengi
ya asili ikiwemo mavazi.
Wanasema wazazi
wakubali kuwa, malezi ya pamoja yana umuhimu wake katika kuwalea vijana wao,
kwani hapo zamani kulikua na malezi ya ushirikiano na ndio maana hata wao
wakafikia pahala pazuri.
Hamad Mbwana Shaame mkaazi wa Kwale shehia ya
Majenzi Wilaya Micheweni miaka 60, anasema wazazi wawaelezea vijana wa sasa
umuhimu wa vazi hilo.
‘’Inawezekana
vijana wa leo hawajui, faida kama vile stara, sasa tukichukua nafasi ya
kuwaelisha huwenda uatamduni huo ukarejea Micheweni,’’anashauri.
VIJANA
WANAZUNGUMZIAJE JUU YA VAZI HILI
Fatma Juma na
Time Khamis Mwinyi wa Micheweni wanasema kuwa vazi hilo lilikua linavaliwa hapo
zamani, kutokana na uhaba wa nguo.
Kwa sasa
wanasema, wamelipa kisogo maana nguo na mavazi mengine yamekuwa mengi, mno na suala
la kujistiria inategemea na mtu mwenyewe.
Wanaeleza lakini kwa sasa vazi hilo limeonekana
kupotea kabisa hii ni kutokana mambo yalivyokuwa, kwani sasa hivi hakuna mzazi
anaeweza kumwambia kijana wake avae vazi hilo
WIZARA YA HABARI
Waziri wa Habari,
Vijana na Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita, wakati akiwasilisha
bajeti ya fedha ya mwaka 2022/2023, Baraza
la Wawakilishi, anaeleza kuwa wizara inaendelea kuhifadhi, uendelezaji na
ukuzaji wa utamaduni.
Upande
mwengine anaeleza kuwa, miongoni mwa vipaumbele kwa mwaka ujao wa fedha ni
pamoja na utoaji mafunzo kwa watendaji, wajasiriamali wa shughuli za
kiutamaduni na wasanii.
Katika
kukuza na kuendeleza utamaduni, wizara imefanikiwa kuandaa tamasha la 26 la utamaduni
wa mzanzibari kwa Unguja na Pemba.
Eneo jingine
ni kuimarisha huduma za utamaduni na sanaa kwa kujenga nyumba ya Sanaa kwa
lengo la kutoa mafunzo, kuongeza ajira, kukuza, kuhifadhi na kuendeleza
utamaduni, Sanaa na ubunifu kwa jamii ya Zanzibar.
MWISHO.
Comments
Post a Comment