NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MWENGE wa uhuru umewasili kisiwani
Pemba, ukitokea Mkoa wa kaskazini Unguja, tayari kwa ajili ya kukimbizwa katika
wilaya nne za Pemba, samba mba na ufunguzi wa miradi kadhaa, ikiwemo ya
maendeleo kisiwani humo.
Mwenge huo
umepokelewa jana, katika uwanja wa ndege wa Karume Pemba, ambapo wananchi wa
mikoa miwili ya Pemba, wakiongozwa na Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama
Mbarouk Khatib, wamejumuika.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahamoud,
alisema mwenge huo ukiwa mkoa mwake, ulizindua miradi minane ya maendeleo na
program nne, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 14.4.
Alisema
wakimbiza mwenge, walitoa ujumbe kwa wananchi, ukiwemo suala la uhifadhi na
utunzaji wa mazingira, lishe na kupinga rushwa na kisha kuchunguza afya kwa
wananchi.
Mkuu huyo wa
Mkoa, alisema katika kipindi hichi, walipanda miti 120,000, ingawa katika
shamra shamra za mwenge wamepanda miti 2,500.
‘’Mkuu wa
mkoa wa kaskazini Pemba, napenda nikukabidhi mwenge wa uhuru ukiwa unang’ara,
na wakimbiza mwenge wakiwa na afya njema,’’alieleza.
Akizungumza
kwenye hafla hiyo, kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Abdalla Shaib
Kaimu, alisema wameridhishwa na usimamizi wa miradi ya maendeleo, katika mkoa
wa kaskazini Unguja.
Alieleza
kuwa, umoja uliopo, mshikamano na upendo ndani ya mkoa wa kaskazini, umesaidia
kuwepo kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, na kuwepo kwa
miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha
aliwataka wakuu wa wilaya, kuwepo kwa nyaraka mahasusi ya miradi, vipimo vya
kupimia ubora wa baadhi ya miradi pamoja uwepo wa wataalamu husika kwenye miradi
itakayopitiwa na mwenge.
Mara baada
ya kupokea mwenge huo, mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib,
alisema mwenge utayapitia miradi 10 na program 10, yenye thamani ya shilingi
bilioni 18.428.
Alieleza
kuwa, miradi hiyo ipo katika wilaya ya Micheweni na Wete, ambapo imo ile ya
maendeleo, kama ya kiwanda cha kusarifu mwani Chamanagwe, upandaji miti eneo la
Kangagani.
Akisoma risala kabla ya zoezi la uzinduzi wa
upandaji miti, katika kambi za chuo cha Mafunzo Kangagani eneo la Mashindeni,
mpiganaji Abrahman Mwinyi Chumu, alisema ekari 792.05 zimetengwa kwa shughuli
mbali mbali, ikiwemo upandaji miti.
Alisema,
wameamua kupanda miti hapo, ili kulirejeshea hadhi yake eneo hilo, kufuatia
uharibifu uliofanyika kwa muda mrefu, hali iliyopelekea, kuwepo kwa jangwa.
Alieleza
katika eneo hilo, wanatarajia kupanda miti aina ya Mivinje 1,500 na kufanya
idadai ya miti yote ambayo wataipanda hapo baadae kufikia 9,000.
‘’Katika
zoezi hilo, shilingi milioni 14.175 zilikadiriwa kutumika, lakini zimeokolewa,
kwa kule wapiganaji kujitolea na kutumika shilingi 13.5 kwa ununuzi wa
miche,’’alieleza.
Mkuu wa
wilaya ya Wete Dk. Hamad Omar Bakar, alisema mikono ya wananchi, isitumike
kupelekea athari kwa jamii, kwa kule kukata miti ovyo.
Alieleza
kuwa, ujio wa mwenge huo katika eneo hilo, limesababisha upandaji wa miti 9000,
ya aina mbali mbali ikiwemo mivinje na mikeshia.
‘’Hata baada
ya kuondoka mwenge, zoezi la upandaji miti katika kambi za Chuo cha mafunzo,
litakuwa endelevu, kwani tayari pameshaharibika,’’alieleza.
Mapema mkimbiza
mwenge wa uhuru Zinab Hemed Mbetu, akitoa ujumbe wa mwenge, aliwataka wananchi
kuendelea kutunza mazingira, hasa eneo la vyanzo vya maji.
Akisoma
taarifa ya kitaalamu, Mkurugenzi mkuu Kampuni ya mwani Zanzibar Massoud Mohamed
Rashid, wakati mwenge huo wa uhuru ulipofika, kwenye kiwanda cha kusarifia
mwani Chamanangwe, alisema ujenzi wa kiwanda hicho umefikia hatua nzuri.
Alisema
ujenzi huo ambao unajengwa na Kikosi maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar ‘KMKM’
uko katika awamu ya kwanza, kati ya zile tatu hadi kukamilika kwake.
Alifafanua
kuwa, awamu ya kwanza inajumuisha ujenzi wa jengo kuu la kiwanda, ujenzi wa
ghala pamoja na uzio maalum kwa ajili ya kulihifadhi eneo hilo.
‘’Awamu pili
utajumuisha ujenzi wa maeneo ya bustani, ufungaji wa mitambo husika na awamu ya
tatu ni kuanza uzalishaji bidhaa zitokanazo na mwani,’’alifafanua Mkurugenzi
huyo.
Aidha
alieleza kuwa, hadi sasa tayari ujenzi huo wa awamu ya kwanza umeshafikia
asilimia 86, na ukitarajiwa kutumika shilingi bilioni 8.2 ingawa wameshatumia shilingi
bilioni 4.024 na utakapomalizika wote, utagharimu shilingi bilioni 13.
‘’Mradi huu
wa kiwanda, utakapomalizika utakuwa na uwezo wa kusarifu mwani tani 30,000 kwa
mwaka, ambapo umiliki wake kwa asilimia 55 utakuwa serikalini na asilimi 45
utakuwa wa kampuni ya Nutri-san.
Mwenge wa
uhuru leo, utakuwa wilaya ya Micheweni kwa kuzindua miradi mbali mbali, kisha
kukabidhiwa kwa uongozi wa wilaya ya Chake chake na Mkoani, ambapo ujumbe wa
mwaka huu ‘Tunza mazingira ukoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe na uchumi
wa taifa’.
Mwisho
Comments
Post a Comment