NA
HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
ILIKUA
kama ndoto, kwa siku ya kwanza kati ya zile 360 zinazounda mwaka, kwa waalimu,
wanafunzi, wazazi, walezi wa Mwambe, kunawa uso mbele ya Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Sio tu kunawa uso, kwa maji kama ilivyozeeleka, wao
walinawa kwa kumalizika skuli ya msingi ya ghorofa mbili eneo hilo la Mwambe.
Hapa wazazi, walezi, wanafunzi na waalimu, maji kwenye
upindo wa kucha ya mtoto mchanga, yalitosha kuwakogesha mwili mzima.
Furaha yao, sio tu kuamka wakiwa wazima siku hiyo ya
Januari 1, mwaka 2023, lakini ni pale waliposhuhudia jengo la kwanza la ghorofa
katika eneo la Mwambe, na bahati nzuri sio la mtu binafsi, bali likiwa la
serikali.
WANANCHI
MWAMBE
Haji Omar Kheir, anasema aliposikia ahadi ya rais wa sasa
wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, juu ya ujenzi wa skuli ya ghorofa,
hakuamini akilini mwake.
‘’Si unajua baadhi ya wanasiasa wakitaka jambo lao,
watakuahidi jambo hata ambalo yeye hajawahi kuliona wala kuliskia,’’anasema.
Kisha kwa Januari mwaka huu, akasema sasa anakubali kuwa Dk.
Mwinyi, anachokiahidi anakitekeleza, akatolea mfano skuli hiyo ya ghorofa mbili
Mwambe.
Asha Muhsini Mohamed, anasema sasa baada ya kusimama kwa
jengo hilo, ni wajibu wao kuwahimiza watoto kusoma, badala ya kukimbilia
baharini kuchokoa pweza na kaa.
Is-mail Hamdu Mjaka, anasema jengo hilo, alitarajia
lijengwa mjini Chake chake au mjini Unguja, lakini kwa uungwana wa Rais wa sasa
Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewapelekea wao.
‘’Kwa hakika ile Mwambe wa miaka 50 iliyopita sasa
imeshatoweka, na hii ya sasa ni kama ilivyo mjini Chake chake au Unguja, kwa
kuwepo kwa jengo la kisasa,’’anasema.
WANAFUNZI
Kazija Omar Haji na mwenzake Asha Haji Ussi wanasema,
sasa ni kazi ya kamati, washirikiane na wazazi ili kutimiza ndoto zao za kupata
elimu.
Makame Mcha Kheir na Abubakar Mohamed Machano, wao
wanasema watasoma kwa ushindani na skuli nyingine, hasa baada ya kupatiwa jengo
la kisasa.
Wanafunzi wanakumbuka, wakati ule walipokuwa wakiingia
mikondo mitatu, wakisema hawakuwa na mtiririko mzuri wa kujifunza.
RAIS
WA ZANZIBAR
Januari hiyo 1, mwaka huu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alikwenda mwenyewe, kuifungua
skuli hiyo mpya ya ghorofa mbili.
Kwenye hutuba yake fupi na iliyojaa kila kitu, alianza na
kuipa agizo wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, ishirikiane kwa karibu na
Idara ya Utumishi, ili kuajiri waalimu nchini.
Akasema, changamoto ya uhaba wa waalimu anaijua kuwa ipo,
lakini ni vyema kwa wizara husika, kuongeza kasi ya kuajiri waalimu, na
kipaumbele, iwe ni wale ambao walishajitolea siku za nyingi.
Wakati serikali ikijenga skuli mpya zikiwemo za ghorofa,
na kuzifanyia ukarabati zile za zamani, lazima na suala la kuajiri waalimu,
nalo liangaliwe kwa haraka, alisisitiza Dk. Mwinyi.
‘’Kama walionesha moyo wa kujitolea kwa taifa lao, kwa
kuwatumikia wananchi wenzao, sasa wakati ukifika nao kuajiriwa, wapewe
kipaumbele kwa wenye sifa,’’akasisitiza.
Lakini, kubwa na la kufurahisha kwa eneo hilo la Mwambe,
ni pale Dk. Mwinyi, alipoahidi kujenga skuli nyingine ya ghorofa, ili
kukabiliana na uwingi wa wanafunzi uliopo.
Akaeleza kuwa, ameshtushwa na idadi ya wanafunzi
wanaoendelea kuandikishwa wa darasa la kwanza kwa mwaka huu, ambapo walifikia 970
kwa wakati huo.
‘’Kwa hili, lazima niwaahidi wananchi wa Mwambe na vijiji
jirani kuwa, serikali itajengwa tena skuli nyingine ya ghorofa, ili kuondoa
hata mikondo miwili,’’anaeleza.
Tena hapa akagongomelea msumari kuwa, bado serikali ya
awamu ya nane, itaendelea kuona kuwa, elimu ndio kipaumbele cha kwanza, na azma
ya kujenga skuli za kisasa na vifaa vya kufundishia ipo.
‘’Ndio maana zipo skuli 24 za zamani kwa Unguja na Pemba,
zinaendelea kufanyiwa matengenezo makubwa, ambapo kwa wilaya ya Mkoani, ni skuli
za Mauwani Kiwani, Chambani na Maendeleao Ngwachani.
Kumbe ndani kipindi cha mwaka mmoja, serikali imeshajenga
madarasa 143, kati ya hao 95 yalianzishwa kwa nguvu za wananchi na 48 ndio mapya,
samba mba na ujenzi wa vyoo 318 kwa skuli za maandalizi, msingi na sekondari
mkoani humo.
WIZARA
YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI
Mwenye dhamana kuu ya elimu ya Zanzibar Leila Mohamed
Mussa ambae ni Waziri wa wizara hiyo, anasema, kwanza amevutiwa mno na kasi ya
Dk. Mwinyi ndani ya wizara hiyo, akisema imesaidiai kutatua changamoto tofauti,
zikiwemo za maakazi kwa wanafunzi.
Kumbe, sio Mwambe pekee, lakini kila wilaya ya Unguja na
Pemba, ameshaacha alama, kwa kuhakikisha kunajengwa skuli za kisasa na za
ghorofa, kuingiza na samani zake kamili.
Waziri huyo wa Elimu akaenda mbali zaidi, pale alimpongeza
Dk. Hussein kwa kuwapatia fedha shilingi bilioni 68, kwa ujenzi wa skuli na
kutia samani.
Hata ununuzi wa vitabu, sambamba na kukamilisha ujenzi
skuli 25 za maandalizi Unguja na Pemba, ikiwa ndio msingi wa elimu ya sekondari.
Kwake anaona, kukamilika kwa skuli hiyo ya ghorofa mbili
Mwambe, kama vile amemalizka changamoto kubwa hasa eneo hilo.
Katibu Mkuu wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis
Abdalla Said, akiutaja ujenzi wa skuli ya ghorofa ya Mwambe, akasema baada ya
kumalizika, sasa umejumuisha madarasa 46, yakiwemo 25 ya zamani.
Lakini pia, akazigeukia fedha za sherehe ya Mapinduzi ya
Zanzibar za miaka 59, shilingi milioni 450, zitawasaidia kwa ununuzi wa samani na
vitabu katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.
‘’Skuli hii yenye
ghorofa mbili na moja ya chini (ground)
ni ya kwanza kwa Zanzibar, ambayo itapunguza changamoto ya makaazi kwa
wanafunzi wa Mwambe,’’alieleza.
Wizara, tayari imeshaingiza viti, meza mpya na za kisasa
ndani ya skuli hiyo, na sasa iko tayari kwa ajili ya kuhamiwa.
Afisa Mdhamini wizara ya elimu na mafunzo ya Amali Pemba
Mohamed Nassor Salim, anasema matayarisho ya kuongoeza idadi ya waalimu skulini
hapo, yameshakaa vyema.
VIONGOZI
WENGINE
Mattar Zahor Massoud ndie mwenye mkoa wa kusini Pemba, baada
ya kulishuhudia ghorofa likiwa limesimama wima, akawakumbusha wananchi wa
Mwambe, kuilinda miundo mbinu ya skuli hiyo.
‘’Hii ni hazina ya urithi wa elim na shilingi bilioni
zaidi 3.5 zimeshatumika hadi kukamilika, sasa lazima na sisi wananchi tuthamini
jambo hili,’’anasema.
Kumbe ndani ya mkoa huo, vipo vyumba vya madarasa 1,116
ikijumuisha hivyo 42 vya skuli ya ghorofa ya Mwambe.
Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani ilipo skuli hiyo ya Mwambe,
Mussa Foum Mussa, akaigeukia serikali kuhakikisha kuwa, inaongeza idadi ya
waalimu, ili kwenda sambamba na idadi ya wanafunzi.
‘’Hapa pana waalimu 49 tu, kwa wanafunzi 4,234 sasa
lazima tuone hiyo changamoto, baada ya kupata makaazi sasa ni ajira kwa
waalimu,’’alikumbusha.
Hata Mwalimu mkuu
wa skuli hiyo, Ali Mohamed Omar, anasema ujenzi wa skuli hiyo, umetoa mwanga
mpya wa kupata elimu.
Anaona kuwa, sasa kilichobakia ni jukumu la wazazi na
walezi, kuwahimiza wanafunzi wao ili, uwepo wa jengo hilo la ghorofa mbili,
thamani yake iaendane na kasi ya kupata elimu.
ILIKOTOKA
SKULI YA MWAMBE NA SASA
Skuli ya msingi Mwambe, iliasisi mwaka 1973 ambapo kwa
wakati huo, ikiwa na wanafunzi wasiozidi 100, na ilianza ikiwa na madarasa ya
kusomea 25.
Kisha skuli hiyo katika miaka ya 2000, baada ya idadi ya
wanafunzi kuongezeka, mtindo wa kuingia mikondo mitatu skulini hapo, ulianza.
Hadi mwaka 2022, ndipo ilipoanza ujenzi wa skuli ya
kisasa ya ghorofa moja ya chini (ground) na ghorofa mbili za juu.
Sasa zikijumuisha vyumba 21, na ukijumlisha vyumba vya
zamani, skuli hiyo itakuwa na vyumba 46, vikibeba wastani wa wanafunzi 45 kwa
chumba kimoka kutoka 86 kwa zamani.
Skuli hiyo kwa sasa, ina jumla ya vyoo 30, na kila
ghorofa kuwepo kwa ofisi tatu za waalimu, achia mbali ile ya mwalimu mkuu.
Lakini wapo wanafunzi 4,234 ikijumuisha na ile skuli kwa
madarasa ya zamani, huku ile mpya pekee, ikiwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 1,890
kwa mikondo miwili.
Ambapo hapo wanafunzi 945, wataingia asubuhi na wengine
mchana, wakitumia vyumba 21 kwa wastani wa wanafunzi 45 kila darasala moja.
Kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo, skuli ya msingi
Mwambe, wapo wanafunzi 820 walifanya mitihani ya taifa, lakini ni wanafunzi
sita tu wa michepuo na wawili wa kipawa maalum.
Na ile ya sekondari, nao kwa kipindi hicho hadi mwaka
2021, hawajapata mwanafunzi aliyepata ufaulu wa daraja la kwanza ‘division
one’.
Skuli hiyo ya ghorofa mbili ya msingi ya Mwambe wilaya ya
Mkoani Pemba, ujenzi wake umechukua mwaka mmoja, umejengwa na kampuni na Mwamba
kwa shilingi bilioni 3.571 fedha za UVIKO 19, kupitia Shirika la Fedha Duniani
‘IFM’.
Mwisho
Comments
Post a Comment