NA ZUHURA JUMA, PEMBA
“NILIAMBIWA mahkamani kua, mtoto wangu atalipwa
shilingi milioni 1 ya fidia, tangu mwaka jana, mshitakiwa alipotiwa hatiani, lakini
sasa ni miaka miwili hajapewa, mpaka mshitakiwa alipoondolewa hukumu kwa madai
ya ugonjwa wa akili,’’anasema mzazi mmoja.
Mama huyo mkaazi
wa Wingwi Wilaya ya Micheweni ambae mtoto wake wa miaka mitatu (3) alifanyiwa
kitendo cha ubakaji na kijana wa miaka zaidi ya 28.
Anaeleza
kuwa, alitegemea fedha hizo zitamsaidia kumshughulikia mtoto wake ambae
aliathirika kisaikologia na kimwili, ingawa hajaulizwa chochote tangu kesi hiyo
ilipopata hukumu mwaka jana.
“Kinachoniumiza
zaidi ni kuona yule mshitakiwa alitakiwa kutumikia chuo cha mafunzo miaka 30,
lakini haijatimia mwaka, ameshatolewa eti kwa madai kuwa ni mgonjwa wa akili,
na amekwenda Unguja Mental”, anaeleza.
Anasema
kijana huyo hajawahi kumuona wala kusikia kwamba ana ugonjwa wa akili,
isipokuwa wanafanya hivyo ili asifungwe wala alimlipe fidia.
Mama huyo sio
peke yake ambae hajapata fidia bali, kuna baba ambae mtoto wake wa miaka 11 alibakwa
na hukumu kutolewa mwaka jana, ingawa hajaona fidia iliyotakiwa kulipwa.
Baba huyo mkaazi
wa Madungu Wilaya ya Chake Chake anasema, mshitakiwa huyo alitakiwa atumikie
chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka saba, na alipe fidia ya shilingi milioni 2, ingawa
bado hajalipwa na ameshakata tamaa.
“Sina tamaa
ya kulipwa, lakini familia ya kijana huyu huko mtaani wanasema kuwa, hawalipi
chochote kwa sababu wanajua kuwa, kitakapomalizika kifungo, ataongezwa tu miezi
mitatu ya adhabu kwa kutolipa fidia”, anasema.
Anaiomba
Serikali uwepo mfuko maalumu wa fidia ambao utawasaidia waathiriwa wa vitendo
vya udhalilishaji, katika kutatua changamoto zinazowakuba watoto wao.
‘’Sio kwamba
tunataka watoto wetu wabakwe ili tulipwe fidia, lakini wakati limeshatokea, ni
vyema na hawa watoto waliodhalilishwa wakafikiriwa, kwa sababu ningezipata ningemuendeleza
kielemu katika eneo jengine’’, anasema.
Wakili wa
Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (PP) Ali Amour Makame anasema, katika sheria ya Adhabu nambari 6 ya
mwaka 2018, imeweka adhabu ya kifungo pamoja na fidia, ingawa hakuna fidia
iliyowahi kutolewa.
Anasema, hiyo
ni kwa sababu washitakiwa wengi wanaotiwa hatiani hawana uwezo wala vyanzo vya
kulipia fidia na hatimae waathirika, kukosa haki yao hiyo.
‘’Waathiriwa
wengi baada ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wanapata matatizo ya kiafya
au kiakili, hivyo ni muhimu wapatiwe hii fidia yao ili zipate kuwasaidia’’,
anafafanua.
Wakili huyo
anaeleza, kuna haja ya waandishi wa habari kuzisemea sheria zenye kasoro, ili Serikali
kuzijua na kuzirekebisha sambamba na jamii kuzifahamu.
Sheria ya
Kanuni ya Adhabu Zanzibar nambari 6 ya mwaka 2018, ni Sheria ambayo yamo makosa
mengi ya udhalilishaji.
Kifungu cha 3
cha Sheria hiyo kimeeleza makosa ya udhalilishaji kuwa, ni yale yote yalipo
katika sehemu ya 14 kwenye vifungu vya 146, 147 na 148 vya Sheria hiyo.
“Kwa kiasi
kikubwa Sheria hiyo imekidhi matakwa ya Haki Jinai na Jamii kwa ujumla, ingawa
zipo kasoro ambazo zinahitaji kufanyiwa mabaoresho”, anafafanua.
WANANCHI WANASEMAJE
Bakar
Suleiman Juma mkaazi wa shehia ya Kambini anasema, kitu kinachosababisha waathiriwa
wa vitendo vya udhalilishaji wasipate fidia, ni kukosa uwelewa wa sheria, hivyo wanashindwa kujua waipate wapi kudai
haki yao.
“Wao wanajua
hukumu ni ile moja tu ya adhabu ya kifungo na hajui haki yake nyengine, hivyo
fursa hiyo wanaitumia wengine kwa maslahi yao, jambo ambalo sio sahihi”,
anaeleza.
Asha Ali
Hamad mkaazi wa shehia ya Mchanga mdogo anasema, ni vyema kwa Serikali
kusimamia hilo, ili kuhakikisha fidia inatolewa na inawafikia walengwa.
“Hili suala
la fidia sio la kufumbiwa macho, kwa sababu mtoto akishafanyiwa vitendo vya
ukatili anakuwa ameshaathirika kiakili, kisaikologia na kimwili, hivyo
atakapopewa haki yake ya fidia itamsaidia”, anafahamisha.
Mkaazi wa
shehia ya Shengejuu Fatma Saleh Yussuf anaishauri Serikali kupitia mahakama,
itunze kumbukumbu vizuri za mshitakiwa, ili atakapomaliza muda wa kutumikia
adhabu ikiwa hajalipa fidia alazimishwe kuilipa.
WARATIBU WA WANAWAKE NA WATOTO WA SHEHIA
Awena Salim
Kombo ambae ni Mratibu wa shehia ya Kangagani Wilaya ya Wete anasema kuwa, ni
kwamba mahakimu wanapotoa hukumu hawashughulikii tena suala la fidia na ndio
maana washtakiwa hawatoi.
“Ingekuwa
hili jambo la fidia linashughulikiwa na kufuatiliwa basi naamini washtakiwa na
familia zao wangezitoa, lakini kwa vile linakaliwa kimnya ndo maana hawalipi”,
alisema .
Anashauri kuwa,
mshitakiwa atakapomaliza kifungo chake na ikawa hajalipa fidia, asitolewa mpaka
ailipe hata kama atakaa chuo cha mafunzo kwa miaka mengine kumi.
Mratibu wa
shehia ya Mzambarao Takao Fatma Hamad Nassor anaeleza kuwa, sababu ya
washtakiwa kutolipa fidia ni kwamba familia zao ni masikini na wakati mwengine
wao ndio watafutaji.
“Wanasema
kuwa hali zao ni za umasikini lakini wengine hawatoi hata kama wanazo, kwa
sababu hakuna usimamizi wowote, hii inawaumiza sana waathiriwa wa vitendo vya
udhalilishaji”, anasema.
Mratibu huyo
anashauri kwamba, ikiwa mshitakiwa atakuwa na kitu chochote cha thamani
kitaifishwe, ili ipatikane fedha alipwe fidia muathiriwa.
Mchanga Said
Hamad ambae ni Mratibu wa shehia ya Kiungoni Wilaya ya Wete anasema, ili
waathiriwa wanufaike na fidia kuna haja ya kuwa itolewe mwanzo kabla ya
mshitakiwa kutumikia adhabu.
“Itakapofanywa
hivyo atapungua huzuni kwa sababu kwa vile ameshafanyiwa ukatili itakuwa muda
wote anafikiria mambo mengi, lakini fidia itamsaidia kutatua baadhi ya
changamoto zilizomkumba”, anaeleza.
Sheha wa
shehia ya Piki Assaa Khamis Mussa anaishauri Mahakama kusimamia fidia mara tu
inapomalizika kesi na kuhakikisha inawafikia walengwa.
“Ni kweli
fidia hazitolewi na wakati mwengine eti unatakiwa ufungue kesi ya madai, jambo
ambalo ni vigumu kwa sababu umeshapoteza nauli nyingi kufuatilia kesi ya mwanzo
na ndio maana familia za wahanga zinabaki njia panda”, anaeleza.
ASASI ZA KIRAIA
Hafidh Abdi
Said Mkurugenzi wa ‘KUKHAWA Pemba anasema, kwa vile ipo Wizara ya Ustawi wa
Jamii ni vyema iweke utaratibu wa kuwasaidia waathiriwa wa vitendo vya
udhalilishaji.
“Hii ni
muhimu kwa waathiriwa wa vitendo vya udhalilishaji, kwa sababu ameshaathirika kisaikologia
na maisha yake yanaharibika, hivyo Wizara ijipange kuwasaidia wahanga hawa”,
anaeleza.
Mratibu wa
TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, hakuna Sheria malumu zinazosimamia
upatikanaji wa fidia kwa waathiriwa na vitendo vya udhalilishaji, bali kuna Sheria
tu inayomtaka mshitakiwa alipe fidia au akishindwa atumikie kifungo.
“Na jamii
imejijenga kuwa, mshitakiwa akishapelekwa chuo cha mafunzo hana sehemu ya
kuipata fidia ya kumlipa muathiriwa hasa kwa vile yeye ndie alitenda lile kosa”,
anaelezea.
Anasema,
lakini kuna haja ya kuangalia Sheria upya na kuzifanyia marekebisho, ili
kuhakikisha kwamba muathirika anafaidika na fidia hiyo na inamsaidia katika kurudisha
hali yake ya kisaikologia ambayo imeathirika.
“Mimi nadhani
kuwe na utaratibu wa kutolewe fidia ya lazima, kutoka kwa mshitakiwa, kwa sababu
hata wakaidai hawaipati na wakati mwengine wanatakiwa wafungue kesi ya madai,
jambo ambalo ni changamoto,” anafafanua.
Anashauri kuwepo
utaratibu maalum wa kuwalipa wahanga fidia au kuwepo kwa darasa maalumu la
saikolojia kwa watoto hao, ambalo litagharimiwa na serikali na wafadhili.
Anasema kuwa
kupitia wanamtandao wao wa kupambana na masuala ya udhalilishaji katika Wilaya
ya Wete na Mkoani mwaka jana walifuatilia kesi 90, ambazo 16 zipo mahakamani
Kesi nyingine
43 zinaendelea na upelezi, kesi saba (7) zimepata hukumu na 17 ziliondolewa
mahakamani kutokana na kukosa ushahidi.
MAHAKAMA
Naibu Mrajis
Mahakama Kuu Pemba Faraji Shomari Juma anafafanua, kuna kifungu cha sheria
kimeeleza kwamba washtakiwa walipe fidia, ambapo humpa mtu adhabu na kumtaka
alipe fidia hiyo sambamba na kumpa adhabu.
“Kwa hivyo
inakuwa sio lazima alipe kwa sababu imeweka kwamba akishindwa kulipa fidia,
anatakiwa atumikie adhabu ya kifungo kwa muda atakaopangiwa, hivyo
akishatumikia hicho kifungo hakuna sababu ya kulipa tena fidia”, anaeleza.
Akitoa mfano
alisema, pengine amefungwa miaka 30 na akishindwa kulipa fidia atumikie mwaka
mmoja, hivyo anapomaliza adhabu yake ya kifungo anaulizwa kuhusu fidia, ikiwa
hana ndo anamalizia adhabu.
“Ile kusema
tu utamlipa fidia milioni 1ukishasimama hapo tu, inakuwa katika Sheria kuna
shida kidogo, kwa sababu ikiwa hakumlipa je utafanya nini”, anahoji.
Na ndio maana
anawashauri mahakimu wao, wanapotoa fidia waseme kuwa, akishindwa kulipa fidia
itatokea hivi…, jambo ambalo linasaidia kwani anapoambiwa hivyo, wazee wake
watazitafuta.
Anaeleza kuwa,
kuhusu ufuatilia wa fidia ni kuhakikisha mshitakiwa analipa, kwani katika hati
ya kifungo wanaeleza kuwa… mshitakiwa atatumikia miaka kadhaa na fidia kiasi fulani.
Kwa hiyo kule
chuo cha mafunzo wanamlazimisha mshitakiwa alipe na baadae zinafikishwa
mahakamani kwa ajili ya kukabidhiwa muathiriwa.
Anataja kuwa,
mwaka 2022 mahakama maalumu za kupambana na udhalilishaji Pemba, zilifikishwa
kesi 94, ambapo kesi 48 za mkoa wa kusini na kutolewa hukumu kesi 40, huku kesi
za mkoa wa kaskazini Pemba zikiwa ni 46 na kutolewa hukumu 33.
Kutokana na
mapungufu yaliyomo kwenye sheria za kupamba na udhalilishaji, Chama cha
Waandishi wa Habari Tanzania TAMWA -Zanzibar wameona kuna haja ya kuorodhesha Sheria
hizo na kuonyesha kasoro za msingi kutokana na mazingira yaliypo sasa.
Lengo la
kuainisha mapunfu katika Sheria hizo ni kuisaidia Serikali na jamii kwa ujumla
katika upatikanaji wa haki.
MWISHO.
Comments
Post a Comment