NA SALMA LUSANGI, ZANZIBAR
WAKAAZI wa kijiji cha Kinooni Shehia ya Kiboje Mkoa wa Kusini Unguja wameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji Nishati na Maadini Zanzibar kwa kutimiza ahadi ya kuwafikishia huduma ya umeme ndani ya wiki moja ili waondokane na gharama za kutumia umeme wa jenereta.
Wakizungumza mara baada ya kupatiwa huduma hiyo wananchi hao walisema hawana budi kutoa shukrani zao hizo kutokana na sasa watapata unafuu mkubwa wa utumiaji wa huduma hiyo ya umeme kwa kutumia jenereta ambapo gharama zake ilikuwa ni kubwa.
Bi Yusta Clauzi alisema jitihada ambazo zinafanywa na Serikali kama wananchi wanapasawa kuunga mkono kutokana na viongozi wao kuonesha utayari wa kuwatumikia wananchi wake.
“Hatuna budi kutoa shukrani zetu kwa Serikari na pia tumpongeze Naibu Waziri wa Maji Nishati na Madini Shaaban Ali Othman ambaye alituahidi kutufikishia umeme katika eneo letu na leo tumeshuhudia ukeli wake’’, alisema.
Alisema Naibu waziri huyo alifika kusikiliza malalamiko siku ya Oktoba 13, mwaka huu na kuwaahidi October 19 huduma hiyo itafikishwa kupitia taasisi yake ya Shirika la Umeme Zanzibar ( ZECO) ndani ya siku tano za kazi jambo ambalo limefanywa kweli.
Hivyo ahadi hiyo alisema baada ya kupatiwa huduma hiyo ambapo waliteseka kwa kipindi kikubwa na shida hiyo.
Naye Naibu waziri wa wizara hiyo Shaaban alisema wizara yake inatekeleza ahadi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi ya kuwafikishia wananchi huduma karibu.
Hivyo wizara yake itaendelea kufikisha umeme maeneo yote ya Zanzibar ambayo hayajafikiwa na yale ambayo yana matatizo.
Alisema kabla ya mwaka huu 2022 kumalizika ZECO itafikisha nguvu za umeme maeneo yote ya Kinooni, Ili kutimiza ahadi za Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Mwinyi kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Aidha Naibu waziri huyo alitembelea tangi la maji la Serikali katika eneo hilo, ambalo wakaazi hao walieleza kwamba linavuja na kuangiza watalaam wa Mamlaka ya Maji Zanzibar ( ZAWA) kulipatia ufumbuzi.
Comments
Post a Comment