NA HAJI NASSOR, ALIPOKUWA UNGUJA
TUME ya taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzanian imesema iliguswa mno na ajali ya moto iliyoteketeza nyumba za familia 19 mwezi August mwaka huu eneno la mji Mkongwe Zanzibar na mtu mmoja kufariki.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu mtendaji wa tume hiyo katika hatuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Katibu Aboud Idd Khamis kwenye hafla ya kukabidhi ubani wa fedha taslim kwa wahanga hao hafla iliyofanyika nyumba za wazee Sebleni mjini Zanzibar.
Alisema UNESCO ni sehemu ya familia ya mji Mkongwe na jamii kwa ujumla hivyo iliguswa na kuhuzunishwa mno na ajali hiyo ambayo pia mtu mmoja alifariki dunia.
Kaimu Katibu huyo mtendaji alieleza kuwa ajali hiyo ilipoteza pia mali za wakaazi wa shehia ya Kiponda kufuatia kukosa muda wa kuziokoa ingawa hilo ni mipango ya Muumba.
'"Sisi tulipopata taarifa hii kwa kweli tulikosa amani na kuwakumbuka mno binadamu wenzetu na hasa kwa vile kulikuwa na kifo na majeruhi,"alisema.
Katika hatua nyingine Kaimu Katibu huyo mtendaji wa tume ya taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aboud Idd Khamis aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchukua tahadhari katika majanga kama hayo.
Kwa upande wake Katibu mkuu ofisi ya Makamu wa Pili wa rais Zanzibar Thabiti Idarus Faina alisema wakati umefika sasa kwa wananchi kujiunga na mashirika ya bima.
Alisema wananchi kujiunga na mashirika hayo kunasaidia kwa kiwango kikubwa pale inapotokezea majanga kupata usaidizi wa kureresha mauimivu ya awali.
Aidha alieleza kuwa serikali haitomuacha mtu nyuma na kudhalilika na hasa ikiwa amekumbwa na majanga.
"Kama tulivyowaahidi mara baada ya kutokezea ajali hii kuwa serikali itawasaidia lakini pia tutawatafuta na wenzetu na leo wapo tume ya taifa ya UNESCO itawapatia chochote alisema,""alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu mkuu wizara ya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee wanawake na watoto Zanzibar Maryam Juma Sadala aliipongeza tume hiyo kwa kuwakumbuka wahanga hao.
Alisema tume hiyo pamoja na kwamba ni mdau wa Mjimkongwe lakini imekuwa karibu mno na makundi mbali mbali katika jamii.
Baadhi ya wahanga wa ajali hiyo akiwemo Riziki Idd Mwalim alisema msaada huo wa fedha ni faraja kwao.
Nae Amina Rashid Abass na mwenzake Abass Rajab Issa walisema hasara walioipata ni kubwa ikiwa ni pamoja kuyahama makaazi yao.
Ajali hiyo ya moto iliyotokezea shehia ya Kiponda eneo la Mjimkongwe wilaya ya mjini Unguja August 30 mwaka huu familia 19 zilikosa makaazi na mtu mmoja kufariki dunia.
Mwisho.........
Comments
Post a Comment