NA HAJI NASSOR,
PEMBA:::::
WAJUMBE wa kamati
ya kuelekea kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kisiwani
Pemba, wameombwa kuacha dharura zisizo za msingi, na kushiriki kikamilifu
katika vikao vya matayarisho.
Kauli hiyo, imetolewa Oktoba 20, mwaka 2022 na Katibu wa muda wa kamati hiyo, Safia Saleh
Sultan kwenye kikao kazi cha kupanga mikakati na namna ya kufanikisha kilele
hicho, kilichofanyika Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar ‘ZLSC’ tawi la Pemba.
Alisema jambo hilo ni jepesi mno
kulifanikisha, ikiwa wajumbe waliojikubalisha kuingia kwenye kamati hiyo,
watahudhuria kwenye vikao vinavyoitwishwa.
Alieleza kuwa, kutokana na mpangilio walivyofikiria
kufanikisha siku 16 za kupinga udhalilishaji, unaweza kufanikiwa ikiwa wajumbe
hawatokatisha vikao vinavyoitwisha kila muda.
‘’Moja ya changamoto kubwa ni wajumbe kujaa
dharura wakati tunapoendesha vikao vyetu, sasa kwanza waje kisha tuone
tunafanikisha shughuli yetu kwa wepesi,’’alieleza.
Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa muda,
alisema wanakusudia kuonana na mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, ili kuona wanapata
baraka na ushauri kwa baadhi ya mambo waliokwisha yapanga.
‘’Siku zote tunapokuwa na shughuli zetu mbali
mbali, mkuu wa Mkoa amekuwa sehemu ya ufanikishaji, sasa tunakusudia kumfuata,
baada ya kumaliza kupanga kwa hatu za awali sisi kamati,’’alifafanua.
Akizungumzia kuhusu muelekea wa shughuli hiyo,
alipendekeza kuwa, kinachoweza kupunguza gharama ndio kiangaliwe, ingawa lengo
ni kufikisha ujumbe wa jamii.
Nae mshika fedha wa kamati hiyo Siti Habib
Mohamed, alisema bado bajeti rasmi ya shughuli haijapitishwa kutokana na baadhi
ya wajumbe kutohudhuria.
Kwa upande wake mjumbe kutoka ‘KUKHAWA’ Hafidh
Abdi Said, alisema ni vyema wakaangalia zaidi kutoa elimu ya kujiepusha na
udhalilishaji kwa wanafunzi wa skuli na madrassa.
‘’Tukielekea siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia,
tusisahau kuwa watoto ndio waathirika wakubwa, hivyo hata kama kuna mabonanza,
lakini utoaji elimu skuli na madrassa upewe kipaumbele,’’alipendekeza.
Wiki iliyopita kamati hiyo, tayari imeshaonana
na Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, ambae alitaka kuona vile
vijiji vyenye matukio mengi ya udhalilishaji, kufikiwa kielimu.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya, alipongeza
wazo la kamati hiyo, kutaka kusaidiana na serikali, katika azma yake ya
kupunguza na kuondoa kabisa matendo hayo.
Hadi Oktoba 20, mwaka huu ratiba pendekezwa ni
kuanza shughuli hizo Novemba 24, kwa wajumbe kuzungumza na wananchi kupitia vyombo
vya habari.
Novemba 26, kuwepo kwa matembezi ya uzinduzi
wilaya ya Mkoani, kutoa elimu kwa wananchi kupitia redio Jamii Mkoani, Novemba 27,
kuanza kuruka kwa vipindi vya redio na tv.
Aidha ratiba hiyo ya awali, ilipendekezwa
kuwa, kuanzia Novemba 28 ni kutoa elimu ngazi ya skuli na madrassa za kur-an, Novemba
29 hadi Disemba 3 kufanyike makongamano kwa wilaya zote nne za Pemba.
Aidha wajumbe hao walipendekeza kuwa, Disemba
4, mwaka 2022 iwe ni siku ya bonaza la mpira wa miguu eneo la Tumbe, na michezo
mengine kwa ajili ya watu wenye ulemavu, katika viwanja hivyo.
Vipindi vya redio na tv, vitarudi tena kuanzia
Disemba 5 hadi 9, na Disemba 10, ndio siku ya kilele kinachotarajiwa kufanyika
kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake.
Hadi sasa taasisi zinazounda kamati hiyo na
kuhudhuria kwenye kikao cha mwisho ni ZLSC, CHAPO, My hope Foundation, KUKHAWA,
blog ya Pemba today, ZAPDD, PEGAO ambazo zote na nyingine zimetakiwa
kuwasilisha nembo (logo zao) kwa
kamati.
Siku 16
za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake, ambapo kampeni hii hufanyika kuanzia tarehe 25 Novemba na kumalizika tarehe 10 Desemba ya kila mwaka.
Siku hiyo ilianza kuadhimishwa
rasmi mwaka 1991, siku hii inaongozwa na Kituo cha kimataifa cha Wanawake tarehe 10 ilichaguliwa
rasmi kuwa siku ya kilele cha maadhimisho haya ikiambatana na siku ya haki za binadamu
duniani.
MWISHO
Comments
Post a Comment