NA
HAJI NASSOR, PEMBA
WAJAWAZITO
wa shehia za Mwambe, Kengeja, Wambaa na Chumbageni wilaya ya Mkoani Pemba,
wameomba kufanyiwa matengenezo ya dharura barabara zao, ili zipitike kwa
utulivu wakati wote.
Walisema, wamekuwa na changamoto ya usafiri kwa salama, kutokana
na barabara zao kuharibika kwa kuwepo mashimo yenye kina kirefu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti,
walisema wakati umefika sasa kwa mamlaka husika kuwaonea huruma, kutokana na
barabara wanazozitumia kuchakaa.
Asha Amini Hilali wa Mwambe alisema, baarabara yao, sasa imekuwa
tishio hata kwa garia ya aina gani, kwa kuwepo mashimo yanayohatarisha usalama
wao.
‘’Wakati mwengine sisi wajawazito tunalazimika kwenda hospitali ya
rufaa ya Abdalla Mzee, lakini wasisi ni kupata mitikisiko kwa ubovu wa
barabara,’’alisema.
Nae Hamida Machano Makame, alisema mwanzoni mwa mwaka huu,
alijifungulia ndani ya gari eneo la Mahuduthi, baada ya gari aliyokuwa
akipelekewa hospitali kuingia shimoni na kukatika.
Alieleza kuwa, baada ya kufika kituo cha uzazi cha Mwambe kesi
yake ilikuwa kubwa na usiku huo was aa 7:00 alitakiwa kwenda hospitali ya
Abdalla Mzee ingawa hakufika alijifungulia njiani.
‘’Bara bara yetu sio rafiki kwa sisi wananchi na hasa wajawazito,
baada hupata mitikisiko na mihangaiko, ambayo wakati mwengine huzidisha
maumivu,’’alieleza.
Kwa upande wake Hadia Juma Khamis wa Wambaa, alisema mtoto wake,
aliharibu mimba ya miezi mitatu njiani, baada gari aliyopanda kuserereka na
kuingia msingini.
‘’Ilikuwa ni siku ya mvua mashimo yamejaa maji, dereva haoni
vizuri, lakini wakati analikimbia shimo, ili ndio chanzo cha ajali ndogo na
mtoto wangu kumwagida damu papo hapo,’’alieleza.
Muume wa mwanamke huyo Khamis Issa Khamis alisema, wameguwa
wakitoleshwa fedha kati ya shilingi 50,000 hadi shilingi 40,000 kutoka Wambaa
hadi hospitali ya Abdalla Mzee.
‘’Madereva ukienda kuwataka usafiri wanaifikiria mara mbili
barabara ya Wambaa- Mzingani, hivyo wanapiga fedha kubwa, ili ajihakikishie
mafuta na matengenezo,’’alieleza.
Ali Mkubwa Khamis ambae ni dereva, alisema wamekuwa wazito kuzitoa
gari zao hasa nyakati za usiku kutokana na ubovu uliokithiri wa barabara yao.
Sheha wa shehia ya Chumbageni Mgeni Othman Shaame, alisema kila
anapoandika ripoti, kwenye eneo la changamoto ubovu wa barabara yao huingiza.
‘’Ukieleza wilayani tunaelezwa kuwa barabara zote zimo kwenye
mpango wa ujenzi, na sisi tunaamini itajengwa na wananchi waendelee
kustahamili,’’alieleza.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, alisema anaelewa vyema
kuwa zipo barabara kadhaa ikiwemo ya Mizingani –Wambaa, Mtambile- Mwambe,
Mtambile- Kangani na Kenya –Chambani kuwa zimeshachakaa.
Alisema, mpango wa serikali kuu ni kuzijenga upya kwa kiwango cha
lami, kama ambayo imekuwa ikiahidiwa na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzim Mawasiliano na Usafirishaji Pemba
Ibrahim Saleh Juma, alisema barabara hizo zimo kwenye mpango mkuu wenye zaidi
ya kilomita 300 ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
‘’Kwa sasa hatutumii kifusi tena kujenga barabara za aina yoyote,
bali mpango wa serikali ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami, ili
zidumu,’’alieleza.
Barabara hizo sita za Mzingani- Wambaa, Mtambile- Mwambe,
Mtambile- Kangani, Kenya –Chambani, Chanjamjawiri- Tundanua na Chanjaani –
Pujini zilifunguliwa mwaka 2012 na aliyekuwa rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed
Shein.
Mradi huo wa ujenzi wa barabara hizo,
zilijengwa kwa msaada wa Serikali ya Norway, kupitia Shirika lake la Norad kwa
ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Barabara hizo zilijengwa kwa aina yake, ambapo
zilitumia mfumo wa kuwashirikisha wananchi kwa njia ya nguvu kazi na kutumia
teknolojia ya lami baridi, na kugharimu dola za Marekani milini 11.4
zilizotolewa na Norway na serikali ilichangia dola milioni moja.
Mwisho
Comments
Post a Comment