Na Muhammed Khamis,TAMWA-ZNZ
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Wanawake (UN Women) Bi. Sima Sami Bahous amesema kazi inayofanywa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kuhamasisha wanawake wengi zaidi kushiriki kwenye nafasi za uongozi ni ya kupongezwa na kuthaminiwa na kila mmoja kwa lengo la kufikia usawa wa kijinsia baina ya wanaume na wanawake.
Bi Sima, ameyasaema hayo katika ofisi za TAMWA-ZNZ zilizopo Tunguu Wilaya ya kati Unguja aipofanya ziara maalumu kuzungumza na uongozi wa chama hicho pamoja na baadhi ya wawakilishi wa asasi za kiraia,viongozi wa dini na wawakilishi wa vyama vya siasa kufuatia utekelezaji mradi wa wanawake na uongozi.
Amesema amefurahishwa na mbinu mbalimbali zilizotumiwa na TAMWA-ZNZ katika kutekeleza mradi huo kwa kushirikisha makundi mbalimbali yaliyopo katika jamii ikiwemo viongozi wa dini ambao wamefafanua misingi ya dini na nafasi ya Mwanamke kushika uongozi hali ambayo imesaidia kuleta ulewa kwa jamii na kuonedokana na mitazamo potofu iliyojengeka.
Sambamba na hilo kiongozi huyo wa Umoja wa mataifa alionesha kufurahishwa kwake na ubunifu mkubwa uliofanywa na TAMWA-ZNZ kuwashirikisha wanaume kwenye uhamasishaji jamii jambo ambalo kwa kiasia kikubwa lilichangia kuibadili jamii na kuona umuhimu wa wanawake kuwa viongozi jambo ambalo awali halikua likipewa nguvu kwenye maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Aidha Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambae pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Wanawake (UN Women) Bi. Sima ameelezea adhma ya shirika lake ni kuendelea kufanya kazi na taasisi mbalimbali ikiwemo TAMWA- ZNZ katika kuleta maendelo endelevu kwa wanawake abayo yanaenda sambamba na Malengo ya Milenia ya 2030 yanayosisitiza usawa wa wanawake na wanaume katika vyombo vya maamuzi.
Awali akimkaribisha Bi Sima, Mkurugezi wa TAMWA –ZNZ Dkt Mzuri Issa amesema mradi wa wanawake na uongozi umeleta mabadiliko chanya katika jamii kwani wanawake wengi wameweza kuwa na uthubutu na kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu uliopita.
Mradi wa Wanawake na Uongozi uliokuwa ukitekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ulilenga kuwajegea uwezo wanawake kushiriki harakati za siasa na uongozi ili kuhakikisha wanawake wanapata fursa kwenye uongozi katika ngazi zote za maamuzi na kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake ikiwemo mifumo kandamizi, tafsiri potofu ya baadhi ya misingi ya dini, udhalilishaji katika siasa na rushwa.
Akieleza ushuhuda mmoja miongoni mwa waliowahi kuwa wagombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 jimbo la Malindi kupitia chama cha ACT Wazalendo Halima Ibrahim alisema asingeweza kuwa mgombea na kunadi sera mbele za watu kama sio ujasiri aliojengewa na TAMWA-ZNZ.
Alisema kupitia mradi huo ulimfanya yeye binafsi na wengi kuwa miongoni mwa wanawake wanaojiamini kwa kusimama mbele za watu na ndio maana haikua shida kwake kugombea jimbo kama la Malindi ambalo linatambulika kuwa miongoni mwa kitovu cha siasa kwa miaka mingi.
Hata hivyo alimuomba kiongozi huyo kufikiria kuendeleza tena mradi huo kwa kuwa bado anaamini kuna idadi kubwa ya wanawake wanahitaji kujengewa uwezo zaidi ambao awali hawakubahatika kupata fursa hiyo.
Kwa upande wake kiongozi wa dini, Khamis Abdulrahman, alisema kuwa dini haijakata wanawake kuwa viongozi bali wanatakiwa kufuata taratibu zilizipo katika imani za dini.
Alisema wakati wakitoa elimu kupitia mahubiri yao kuhusu nafasi ya mwanamke katika ungozi walipitia changamoto nyingi ikiwemo maneno mazito kutoka kwa jamii kutokana na mfumo dume uliojengeka kuwa mwanamke ni mlezi wa familia.
Alisema mradi huo umesaidia kubadilisha mitazamo hasi ya jamii kuhusu nafasi za uongozi kwa wanawake na kusema ipo haja ya mradi huo kuendelea ili kufikia asilimia ya 50 kwa 50 ya wanawake katika vyombo vya maamuzi ikiwemo Baraza la wawakilishi na Bunge.
Comments
Post a Comment