NA SALMA LUSANGI,
NAIBU waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shabaan Ali Othman amewaahidi wakaazi wa eneo la Kinooni, Shehia ya Kiboje, Unguja kuwa ndani ya wiki moja Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) litafikisha umeme katika eneo hilo ili waondokane na gharama za kupandisha maji kwa kutumia umeme wa jenereta.
Kauli hiyo ameitoa alipofanya ziara ya kikazi katika jimbo la Uzini, Unguja kufuatia malalamiko ya Mwakilishi wa jimbo hilo kwamba waakazi wa eneo hilo hawana huduma ya umeme wala maji safi na salama.
Shabaani alisema atahakikisha kuanzi tarehe 13 hadi tarehe 19, mwezi huu umeme utafikishwa katika maeneo hayo ili waakaazi wa eneo hilo waandokane na gharama za kutia mafuta kwenye jenereta kwa ajili ya kupandisha maji kutoka kwenye kisima hadi tangi la maji la juu.
Alisema wizara yake kupitia ZECO inatoa nguzo za umeme bure ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi hivyo atahakikisha Shirika hilo linafikisha umeme haraka eneo hilo.
Aidha aliwaomba wakaanzi wa maeneo mengine ya shehia hiyo kuwa na subra wakati wataalamu wa ZECO wakifanya upembuzi yakinifu, kwani muda sio mrefu huduma ya umeme itafikishwa maeneo yote ya jimbo la Uzini.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri huyo alitembea maeneo mengine ya jimbo hilo la Uzini ikiwemo Kwambani na Kidimni ambapo waakazi wengi wamekabiliwa na changamoto ya maji safi ya salama, wengine wakiyapata kwa mgao huku wengine wakiyakosa kabisa.
Alieleza kwamba wizara yake inatekeleza miradi ya maji kwaajili ya kuwaondolea shida wananchi sio muda mrefu miradi hiyo itakamilika kwani kuna visima vingi vimechimbwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Mapema Mkaazi wa Kinooni bi Mastura Mgeni Hamadi alisema wanawake wa eneo hilo wamekuwa wakichangishana shilingi 3,000 kwa ajili ya kutia mafua ya dizeli kwenye jenereta ili wapandishie maji kwenye tangi kutoka katika kisima chake alichokichimba.
“Naiomba Serikali iwafikiria wanawake hii shida ya maji kwani wamekuwa wakiteseka sana, hali duni ya maisha wakati mwengini mtu anakua anakosa pesa elfu tatu,” alisema Mastura.
Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Uzini, Haji Shabaani Waziri, alimshukuru Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika jimbo hilo kusikiliza kero za wananchi ambao kwa muda mrefu wamekua wakilalamikia ukosefu wa upatikanaji wa huduma za maji na umeme.
Comments
Post a Comment