NA ZUHURA
JUMA, PEMBA::::
MKUU wa
Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali amesema, jamii inapaswa kuweka mifumo
na mipango imara ya kuondoa huzuni za watoto yatima kwa kuwapatia haki zao za
msingi.
Alisema kuwa, watoto hao wamekuwa wakikumbana na kadhia mbali
mbali ikiwepo kufanyiwa udhalilishaji, hivyo kuna haja ya kushirikiana pamoja
katika kuhakikisha wanapata haki stahiki kama watoto wengine wanaoishi na
wazazi wao.
Akikabidhi msaada wa mcehele kwa watoto 320 uliotolewa na
taasisi ya kusaidia mayatima, wajane, watu wenye ulemavu na wasiojiweza (The
Future Life Foundation), Mkuu huyo alisema, watoto yatima wanahitaji
kusaidiwa kwa hali na mali ili wasiwe na huzuni katika maisha yao ya kila siku.
“Mara nyingi watoto yatima wanadhalilishwa katika familia zile
wanazoishi, hivyo ili kuona hawaishi na huzuni, tuwasaidie wajihisi kama wapo
sawa na watoto wenzao”, alieleza Mkuu huyo.
Aliishukuru taasisi hiyo kwa mambo wanayoyafanya kusaidia
jamii na kusema kuwa atahakikisha anasaidia kutatua changamoto zinazowakabili,
ikiwa ni pamoja na ukosefu wa umeme katika shamba lao la mboga mboga.
“Tutafanya mpango kuona kwamba umeme unafika katika shamba
hili, ili uweze kuwarahisishia kupata maji ya uhakika na muweze kupata faida
ambayo ndio mnayowapatia mayatima wetu”, alisema.
Aliwaomba wawazi na walezi wenye watoto yatima wajitahidi kuwalea
vizuri watoto hao, kwani ni mkombozi wao hapa nduniani na kesho akhera.
Akisoma risala, Rais wa Jumuiya hiyo Sheikh Mbarouk Seif Salum
alisema, katika taasisi yao wanasaidia watoto yatima, wajane, watu wenye
ulemavu na wasiojiweza, kujenga visima, misikiti na kusaidia maskulini.
Alisema kuwa, watoto yatima ni watu wanaopata mitihani mikubwa
katika jamii, hivyo kuna ulazima wa kushirikiana pamoja katika kuwatunza na
kuwasaidia kwa kila hali.
“Wako ambao kwa makusudi wanafukuzwa, wananyanyaswa na
kudhulumiwa haki zao ambazo zimewekwa kwa sheria za kiislamu, hivyo ni vyema na
wao tukawajengea mazingira mazuri”, alieleza.
Alisema kuwa, katika juhudi zao za kusaidia watoto hao
wameanzisha kilimo cha mboga mboga katika shehia ya Mjiniole, ingawa wamekuwa
wakipata hasara kutokana na kukosa umeme ambao ungewasaidia kupandisha maji na
kumwagilia.
“Tunatumia jenereta kupandishia maji, jambo ambalo ni hasara
kubwa kwa sababu kwa siku tunatumia mafuta ya shilingi 30,000, hivyo inapofika
mavuno hatupati faida kubwa na kushindwa kuwasaidia mayatima wetu”, alisema.
Alieleza kuwa, lengo la kuanzisha kilimo hicho ni kuhakikisha
wanasaidia makundi hayo wakiwemo watoto yatima, ambapo katika shamba hilo
waliekeza kiasi cha shilingi milioni 45, ingawa gharama zao bado hazijarudi,
hivyo aliiomba Serikali kuiwasaidia zaidi ili malengo yao yafanikiwe.
Kwa upande wake sheikh Abdalla Mohamed Abdalla alisema, watoto
yatima wamekuwa wakikumbwa na udhalilishaji wa aina mbali mbali katika jamii,
kuna haja ya kulindwa na kusaidiwa.
“Baadhi ya walezi wa watoto hawa, wamekuwa wakiwatesa sana
kiasi kwamba muda wote wanajisikia unyonge, kwa hiyo iwapo tutashirikiana
kuwasaidia tutafanikiwa”, alifafanua.
Nae mshughulikiaji wa shamba hilo Ali Msanifu alieleza kuwa,
shamba hilo wamelianzisha kwa ajili ya kupata fedha za kuwasaidia watoto
yatima, hivyo wanahitaji kusaidiwa kutatuliwa changamoto zinazowakabili, ili
waweze kuendesha shughuli zao za kila siku.
Mmoja wa wazazi wa watoto hao Maryam Mohamed Muhene
aliishukuru taasisi hiyo kwa kuwapatia misaada mbali mbali, ambayo inawasaidia katika
kutatua changamoto zao ndogo ndogo.
“Tulichokipata sio kidogo kwa kweli, tunawashukuru sana, Allah
awawezeshe zaidi ili watupe misaada mara kwa mara, kwa sababu watoto yatima
wana mahitaji kama watoto wengine”, alisema mama huyo.
Hafla hiyo ya kukabidhi msaada kwa watoto yatima ulifanyika
katika ukumbi wa Judo Gombani Chake Chake Pemba.
MWISHO.
Comments
Post a Comment