NA HAJI
NASSOR, PEMBA::::
MOJA ya
mashirika ya serikali yaliotajwa kuongeza mapato yake, kupitia ripoti ya
Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, ni Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’
lililongeza mapato yake, kutoka zaidi ya shilingi bilioni 33.579 mwaka
2019/2020, hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 34.344 mwaka 2020/201.
Hayo yamebainika, kwenye ripoti hiyo ya mwaka 2020/2012, ambayo
iliwasilishwa mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Hussein Ali Mwinyi, na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali, Dk.
Othman Abass Ali.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa, kwa upande wa ZECO kulikuwa na ongezeko
la zaidi ya shilingi milioni 764.207 sawa na asilimia 2, huku kwa mwaka
2020/2021, shirika hilo limepata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 16.171,
ikilinganishwa na faida iliyopatikana mwaka 2019/2021, ambayo ni zaidi ya shilingi
bilioni 19.863 na upungufu ikiwa ni shilingi bilioni 3.692 sawa na asilimia 19.
Shirika jengine ambalo mapato yake yametajwa kuimarika ni kupitia
ripoti hiyo, Shirika la Bima Zazibara ‘ZIC’ ambapo yameongezeka, kutoka zaidi
ya shilingi bilioni 19.853 kwa mwaka ulioishia disemba 2019, hadi kufikia shilingi
bilioni 20.020 kwa mwaka 2020.
Ripoti hiyo ikafafanua kuwa, ZIC kwa kipindi hicho, imepata faida ya
shilingi bilioni 2.358 ikilinganishwa na faida iliyopatikana, kwa mwaka
ulioishia 2019 ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni 2.939 kukiwa na upungufu wa
shilingi milioni 580.078 sawa na asilimia 19.7.
Kwa upande wa Shirika la Bandari Zanzibar ‘ZPC’ mwaka fedha 2020/2021,
limepata mapato ya shilingi bilioni 39.897 kutokana vyanzo vya mapato,
ikilinganishwa na makusanyo ya zaidi ya shilingi billion 34.848 kwa mwaka 2019/2020
kukiwa na ongezeko la shilingi bilioni 5.048.
Aidha ripoti hiyo ya Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za serikali imeitaja
Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar ‘ZSTC’ katika kipindi cha mwaka
2020/2021, limepata shilingi bilioni 11.217 ikilinganishwa na makusanyo ya
shilingi bilioni 56.795 kwa mwaka 2019/2020, sawa na upungufu wa shilingi
bilioni 45.577 sawa na asilimia 80.
Aidha shirika hilo linadai wakulima wa zao la karafuu shilingi milioni
7.005 kwa ajili ya mkopo wa zao hilo, ambapo ilikuwa kinyume na mkataba ya
ukopeshaji uliofanyika.
Ambapo wa wilaya ya Chake chake ‘ZSTC’ wanawadai wakulima shilingi
milioni 4,050,000, Wete shilingi 945,000, Micheweni shilingi 2010, 000 na wilaya
ya Mkoani shilingi milioni 1.800 kuanzia mwaka 2011 hadi 2018.
Meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO, tawi la Pemba Mohamed Juma
Othman, amesema wamefarajika kuona kunaongezeko la mapato kwa shirika hilo.
Alisema, moja ya kichecheo cha kukuza mapato yao, ni kuondosha gharama
za nguzo na kuwepo kwa mkopo wa huduma ya umeme kwa wananchi.
‘’Tunaendelea kujipanga ili kuhakikisha mapato ya ZECO yanaongezeka
mara mbili, na vipo vijiji vyenye wastani wa nyumba 80 hadi 120 katika wilaya
ya Micheweni na hata Mkoani hazijafikiwa na huduma yetu,’’alieleza.
Baadhi ya wananchi wakizungumza na mwandishi wa habari mjini Chake
chake, wamesema kama mashirika yameongeza mapato, hakunabudi kuandaliwa
mazingira zaidi ili kuimarisha kazi zao.
Hassan Omar Haji ambae ni mfanyabiashara wa chakula, alisema wakati
umefika sasa kwa serikali, kuhakikisha hakuna shirika la serikali
litakaloporomoka kimapato.
Nae Aisha Hilali Makame wa Mtambile, alisema kama mashirika yameongeza
mapato, yake hakuna budi kuimarisha miradi na miundombinu ya jamii.
Kazija Himid Mohamed wa Mizingani alisema, anamatumaini makubwa na
uongozi wa rais Dk. Mwinyi kuwa, kuongezeka huko kwa mapato, iwe chanzo za
kuimarisha miundombinu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alitaka wote
waliotajwa kwenye ripoti hiyo kuchukuliwa hatua.
Mwisho
Comments
Post a Comment