|
|
|
SAID
ABDULL-RAMAN, PEMBA
WAKULIMA
wa zao la Karafuu Kisiwani Pemba, wametakiwa kuvuna zao hilo, lililopevuka na
kuacha kuvuna karafuu changa, kwani kufanya hivyo, ni kupoteza ubora wa zao
hilo.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Biashara Maendeleo
ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban, wakati akizindua zoezi la uvunaji wa zao
hilo katika mashamba ya mikarafuu Kichunjuu Mtambili wilaya ya Mkoani Pemba.
Alisema, kuwa endapo wakulima wa zao hilo
wataweza kuvuna karafuu zinazostahiki, wataweza kupata faida kubwa kwao na kwa
Serikali, kwa kule kuliongezea thamano zao hilo.
Waziri Shaaban alifahamisha kuwa, kwa mwaka huu
Serikali imedhamiria kurudisha hadhi ya zao la karafuu ya Zanzibar, kuwa na
ubora wake, ambapo tayari Shirika la biashara la taifa ZSTC limeshakaa na wadau
wake.
"Mashine ambazo tumeziweka katika vituo
vyetu vya kununulia karafuu ziko salama, na zimethibishwa na kuthibitika kwamba
zina ubora na wala haziharibu karafuu, kama inavyodaiwa na baadhi ya
watu," alisema Waziri huyo.
"Katika suala la ubora wa karafuu, hili ni
kutokana ushughulikiaji wake kuanzia inapovunwa, uanikaji wake lakini hata
matunzo yake, hii ndio njia itakayosaidia kupata karafuu mzuri," alieleza.
Sambamba na hayo, alieleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, inatambua changamoto zote zilizomo kwenye kilimo cha zap
hilo, hivyo Serikali niajadili changamoto hizo na kuhakikisha inahuwisha kilimo
hicho.
Mapema Waziri Shaaban, aliwatahadharisha wananchi
wote ambao wanajushughulisha na wizi wa karafuu na kusema kuwa kwa sasa
muarubaini wa tatizo hilo limeshapatikana.
"Kwa wale ambao wanajishughulisha na
utoroshaji wa Karafuu,(magendo) mbinu zao tumeshazijua, tutaendelea
kushirikiana na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama ili kuona vitendo hivyo
vinathibitiwa," alisema Waziri Shaaban.
Nae mkulima wa zao hilo, Hafidh Makame Haji wa Michenzani
Mkoani, alisema kuwa, kwa mwaka huu mauzo ya karafuu ni tofauti na miaka
iliyopita, hasa katika sehemu ya kupasishia karafuu kutokana na uwekwaji wa
mashine maalum.
"Kwa wakulima wenzangu tuendelee kuchukuwa hatua za makusudi za kuweka mazingira safi katika mashamba yetu ili tuweze kupata mavuno mazuri," alisema Hafidh.
Comments
Post a Comment