NA HAJI NASSOR, PEMBA
WAHAMASISHAJI jamii kisiwani Pemba, wamekumbushwa kuacha ushabiki wa kisiasa na kumdharau mtu yeyote, wakati wanapofanya ushawishi na utetezi kwa jamii wa kudai haki zao zikwemo za kisiasa na demokrasia.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said ofisi kwake Chakechake, wakati akiwasilisha mada kwa wahamasishaji hao.
Alisema mshawishi mzuri na mtetezi ni yule anaejitenga na ushabiki wa kisiasa wa moja kwa moja na kuhakikisha anawashirikisha watu wote.
Alieleza kuwa jamii itawaamini ikiwa wataweza kuzuia hisia zao kisiasa wakati wanapofanya utetezi juu ya jambo fulani.
"Pamoja na sifa kadhaa lakini kujionyesha wazi wazi kwa mshawishi na mtetezi wa kudai haki za wanawake au jamii huweza kumkosesha kusikilizwa na kundi jengine, "alisema.
Hata hivyo alisema wakati wanapofanya zoezi hilo lazima wajifunze kuzielewa sheria na kanuni zinazowaongoza.
Mapema akiwasilisha mada ya ufuatiliaji wa rasilimali za umma PETS Mratibu wa miradi kutoka Mwemvuli wa asasi za kiraia Pemba PACSO Mohamed Najim Omar, alisema ni haki ya kikatiba kufanya hivyo.
Alisema kinachohitajika kwa muhusika ni kufuata taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kuiomba taasisi inayotaka kufanyiwa ufuatiliaji.
Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Jumuiya ya PEGAO Hafidh Abdi Said, alisema bado jamii inataka kuelimishwa juu ya nafasi na mchango wa mwanawake katika taifa.
Hata hivyo aliwataka wahamasishaji hao kuyafanyia uchambuzi matatizo wanayoyaibua kwa jamii, ili kuona yanafikishwa sehemu husika kwa ufumbuzi.
Nae Mratibu wa miradi kutoka PEGAO Dina Juma Makota aliwapongeza wahasishaji hao na kuwataka waendelee kuisaidia jamii juu ya elimu ya kudai haki zao.
Mhamasishaji jamii kutoka wilaya ya Chakechake Dk. Amour Rashid alisema licha ya changamoto wanazokabiliana nazo lakini hawakati tamaa.
Mwisho
Comments
Post a Comment