NA HAJI NASSOR, PEMBA
KAMATI ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, imesema
kazi inayofanywa na kamati za kupambana na ukatili na udhalilishaji kisiwani
Pemba, ni nzuri na zinafaa kuungwa mkono na wananchi, ikiwa wanataka kuondoa
matendo hayo.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo
Mohamed Ahmada Salim, wakati akighairisha kikao maaluma cha kupokea na kujadili
ripoti za miezi mitatu za kamati hizo, kilichofanyika ukumbi wa Kiwanda cha
Mafuta ya Makonyo Wawi Chake chake.
Alisema suala la kufuatilia au kuibu matendo ya
ukatili na udhalilishaji kwa jamii, ni jambo zito na huandamwa na changamoto
kadhaa, ingawa kwa kamati hizo, zinaonesha mafanikio makubwa.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, matendo hayo
hufanyika kwa siri kubwa, hivyo huwa kunahitaji ujuzi na uweledi wa hali ya juu
kuyaibua na kisha kuyafuatilia.
‘’Kwa niaba ya kamati hii, lazima wajumbe nyinyi
wa kamati zote nne za Pemba tuwapongeze, maana kazi mnayoifanya ni kubwa na
bado hamjakata tamaa, licha ya changamoto mnazokumbana nazo,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa Kamati
ya ustawi wa Jamii, alisema kamati hasa zinazohitaji umakini mkubwa ni zile
kama ya wilaya ya Chake chake na Wete ambazo, zinamkusanyiko mkubwa wa watu.
Kwa upande Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Mwantatu Mbarka Khamis, alizitaka kama hizo, kuzidisha ushirikiano miongoni
mwao, ili kusaidiana maarifa, wakati wanapowahudumia wananachi.
Alieleza kuwa, hilo linaweza kujenga uthubu kwa
kule kubadilisha uzoefu miongoni mwao, na hasa kwa vile zipo baadhi ya kamati
zimefanikiwa kupunguza idadi ya makossa ya ukatili.
Mjumbe wa kamati hiyo, Zawadi Amour Nassor,
alisema lazima mkazo uweke katika wilaya, ambazo zimearipoti matukio ya
ulawiti, kwani haziashiria mwisho mzuri kwa watoto wa kiume.
Nae Bihindi Hamad Khamis, alisema bado kuna
hatari za uwezekano wa watoto wa wilaya ya Micheweni wanaofanya kazi ya ajira
za kubanja kokoto, kutendewa vitendo vya ulawiti na ubakaji, kama mkazo
haukuwekwa.
Akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi kwa kipindi
cha mwezi wa Aprili hadi Juni mwaka huu, Katibu wa kamati ya kupambana na
ukatili na udhalilishaji ya wilaya ya Chake chake Kassim Ali Omar, alisema
wamekuwa wakijikita zaidi kutoa elimu kwa jamii.
Alieleza kuwa, hilo liemfanikiwa na ndio maana,
kunaongezeko la matukio yalioripotiwa kufikia 24 kutoka 14 ya kipindi cha miezi
mitatu kama hiyo, kwa mwaka uliomalizika.
‘’Inawezekana matukio yanaongezeka, lakini sisi
kadiri yanavyoripotiwa, huona ndio elimu kwa wananchi na watoto imewafikia, na
ndio maana wapo wanaowaripoti hadi wazazi au waalim wao,’’alieleza.
Katibu tawala wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, alisema kwa kipindi cha miezi mitatu, walipokea matukio 37 yakiwepo ya ubakaji matano, utelekezwaji 21, ulawiti matukio mawili na makosa ya mvutano wa malezi matatu.
Hata hivyo amesema changamoto kubwa, ni jamii
kutobadili mtazamo na kuendelea kuzifanyia sulhu kesi hizo, jambo ambalo
huwarejesha nyuma katika jitihada zao.
Nae mjumbe wa Kamati ya kama hiyo ya wilaya ya
Wete, Siti Suleiman Juma, alisema wamefanikiwa kuwafikia wananchi 1,760 kutoka
shehia za Mchanga mdogo, Kojani, Mpambani na Kambini juu ya elimu ya kupinga
ukatili na udhalilishaji.
Mwisho
Comments
Post a Comment