NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WAZIRI wa
Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amewataka
wafanyabiashara wa Kengeja wilaya ya Mkoani, kuacha kuuza biashara zao
pembezoni mwa barabara, na badala yake wayatumie masoko yanayojengwa.
Waziri Pembe
alitoa raia hiyo jana, wakati alipomaliza shughuli ya uwekaji wa jiwe la msingi
la soko la kisasa, la sokoni Kengeja wilayani humo, ikiwa ni shamra shamra za
miaka 62 ya mapinduzi.
Alisema kuwa,
mapinduzi yalifanyika kwa dhamira kadhaa, ikiwemo kuwakomboa wajasiriamali na
wafanyabiashara, ikiwemo kuzipandisha hadhi bidhaa zao, na kuzihamishia sokoni
kutoka pembezoni mwa barabara.
Alieleza
kuwa, utamaduni wa kufanyabishara katika mazingira hatarisha ikiwemo pembezoni
mwa barabara, kwenye misingi ya maji taka, huu sio wakati wakati wake tena, na
badala yake waingie masokoni.
Waziri huyo
alieleza kuwa, hasa ndani ya utawala wa serikali ya awamu ya nane, imekuwa ikifanya
kila juhudi kuhakikisha wajasirimali na wafanyabiashara, wanazipandisha hadi
bidhaa zao.
‘’Leo tukiwa
ndani ya shamra shamra za miaka 62 ya mapinduzi Zanzibar, Kengeja lipo soko
lenye hadhi, ni wajibu wetu sasa kuhama pembezoni mwa barabara na kuingia sokoni
humo, litakapomalizika,’’alishauri.
Akizungumzia
faida na dhana ya mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964, alisema ni pamoja na
kujitawala, ili kupanga mikakati kwa aina ya mahitaji.
Hivyo
amewakumbusha wananchi, kuendelea kuyaenzi na kuyathamini mapinduzi hayo, ili
maendeleo yaongezeke katika sekta mbali mbali.
Katika hatua
nyingine, Waziri huyo wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, amewakumbusha
wananchi, umuhimu wa kutunza na kuendeleza amani, iliyopo.
Naibu Katibu
Mkuu wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara
Maalum za SMZ Mikidadi Mbarouk Mzee, alisema ujenzi wa soko hilo, umelenga
zaidi wafanyabiashara wadogo.
Alisema
mradi huo unajumuisha majengo matatu, ikiwemo soko lenye vizimba 40, ambavyo
kila kimoja kinaweza kutumiwa na wajasiriamali wawili.
Alifafanua
kuwa, eneo la pili ni ujenzi wa milango mitano ya maduka pamoja na ujenzi wa
vyoo sita na uzio kwa ajili ya kudhibiti mipaka ya soko hilo.
Aidha Naibu
Katibu Mkuu huyo, alieleza kuwa pindi soko hilo litakapokamilika, wastani wa
ajira 50 zitapatikana, kwa maeneo kadhaa ikiwemo ulinzi.
‘’Sisi
TAMISEMI ndio hasa wenye jukumu la kuhakikisha zile ahadi za Rais wa Zanzibar
Dk. Hussein Ali Mwinyi za ajira kadhaa, tunazizalisha kupitia miradi kama
hii,’’alifafanua.
Mapema Mkuu
wa mkoa wa kusini Pemba Rashid Hadid Rashid, alisema ndani ya mkoa huo yapo
masoko manane, ya kisasa likiwemo la Mtambile, Kipitacho, Machomane,
Michakaini, Mbuyuni na Vitongoji.
Zaidi ya shilingi
milioni 413.655, zinatarajiwa kutumika hadi kukamilika wa ujenzi wa soko hilo,
linalojengwa na KVZ Construction, ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi milioni
242.538 sawa na asilimia 58.63 zimeshatumika.
Ambapo fedha
zilizobakia kulipwa mkandarasani ni shilingi milioni 122.923, huku gharama za ujenzi
wa soko hilo zinatokana na fedha za makusanyo kupitia baraza la mji Mkoani.
Mradi wa
ujenzi wa soko hilo ulianza, Julai 8 mwaka 2025 na unatarajiwa kumalizika mwezi
Machi 8 mwakani, chini ya msimamizi wa mshauri elekezi, Wakala wa majengo
Zanzibar ‘ZBA’.
MWISHO
Comments
Post a Comment