WAZIRI wa
Uvuvi na Uchumi wa Buluu Zanzibar, Massoud Ali Mohamed, amewataka wananchi
kuendelea kuyathamani Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwani ndio msingi wa
maendeleo yaliopo.
Waziri Massoud,
alitoa raia hiyo jana, wakati alipomaliza shughuli za ufunguzi wa kituo cha
kisasa cha ununuzi wa karafuu, eneo la Kiwani wilaya ya Mkoani Pemba, ikiwa ni
sehemu ya shamra shamra za miaka 62 ya mapinduzi.
Alisema kuwa,
mapinduzi sio hadithi ya kuvutia pekee, bali ni kuwepo kwa maendeleo kila
sekta, kama ilivyokuwa azma ya waasisi wa taifa hili.
Alieleza
kuwa, kwa mfano Kiwani iliyokuwepo kabla ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964
na ya sasa ni tofauti, kwa kuwepo miundombinu ya kisasa, kwenye sekta ya afya,
elimu, maji safi na salama na barabara.
Alieleza
kuwa, hayo ndio thamani na umuhimu wa kufanyika kwa mapinduzi hayo, na sasa ipo
haja kwa wananchi na hasa wapenda maendeleo, kuyathamini na kuyaenzi kwa nguvu zao
zote.
‘’Niwatake
wananchi wa Zanzibar, kwamba upo umuhimu wa kuyaenzi mapinduzi haya, kwani sio
hadithi pekee, bali ni uwepo wa maendeleo makubwa, kila sekta,’’alifafanua.
Akizungumzia
uwepo wa kituo hicho Kiwani, aliwataka wananchi kukimbilia hapo, kwa ajili ya
kuuza karafuu zao.
Alieleza
kuwa, usafirishaji magendo wa zao hilo, usiwe na nafasi, kwani sasa yale
matakwa ya wakulima, ikiwemo vipimo vya kisasa visivyopunja, vimeshapatikana.
‘’Sasa
wakulima wa zao la karafuu, ule mtindo mbaya wa kulitorosha zao hilo nje ya
nchi muuache, maana kwanza bei ni nzuri na sasa tunavituo na mizani za
kisasa,’’alifafanua.
Aidha Waziri
Massoud, aliwapongeza ‘ZSTC’ kwa hatua yao ya kuja na mfumo wa mabadiliko ya
ununuzi wa zao hilo, ambao kwa kiasa kikubwa, umeshandosha malalamiko.
Mapema
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Zanzibar ‘ZSTC’ Soud Said Ali,
amesema ufunguzi wa kituo hicho, ni dhamira ya serikali ya awamu ya nane,
katika kuliimarisha zao la karafuu.
Alieleza
kuwa, ujenzi huo umeakisi falsafa ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,
ambayo imejikita katika kuwafikia maendeleo endelevu, wananchi wote.
Aidha alifafanua
kuwa, ujenzi wa kituo na vyingine ni utekelezaji wa mpango kazi wa ZSTC, kusimamia,
kuratibu, uimarishaji wa mifumo ya soko la zao la karafuu.
‘’Lengo kuu
ni kuongeza ufanisi, uwazi, kuimarisha upatikanaji wa haki na usawa katika
ununuzi, usafirishaji wa zao hilo, na kulibakishia na ubora wake, katika soko
la dunia,’’alifafanua.
Katibu Mkuu
wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Dk. Habiba Hassan Omar, alisema
kituo kama hicho kilichopo Kiwani, vitajengwa shehia za Kengeja na Ngwachani
hapo baadae.
Mkuu wa
wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, alisema kazi inayofanywa na ZSTC, inafaa
kuungwa mkono na wakulima wa zao la karafuu, kwa kuziuza karafuu hizo, kwenye
vituo vya serikali.
‘’Ifike
pahala sasa, karafuu zote wakulima waache kuzitorosha na sasa kuzileta ZSTC,
maana mifumo ya ununuzi kuanzia majengo hadi vipo, vimeshaondoa shaka
kwao,’’alifafanua.
Mradi wa
ujenzi wa kituo hicho, ulianza utekelezaji wake mwaka wa fedha 2023/2024, baada
ya ZSTC kutangaaza zabuni, kama sheria za manunuzi, ilivyo.
Ambapo hadi
kukamilika, umegharimu shilingi milioni 406.418 ikijumuisha na ongezeko la
thamani ‘VAT’, na zabuni yake ilitangaazwa Machi 12, 2025 kupitia mfumo wa
serikali wa manunuzi.
Kisha baada
ya mchakato wa ushindani, kampuni ya Kin Investment LTD, ilikabidhiwa jukumu la
ujenzi, huku usimamizi na ushauri elekezi, ukiwa chini ya Wakala wa majengo
Zanzibar ZBA.
Mkataba wa ujenzi, ulikuwa ni wa miezi 12, na kutekelezwa kwa awamu tatu, ikiwemo ya usanifu wa jengo la upatikanaji wa ithibati, ujenzi wa kituo chenyewe na awamu ya tatu ni ujenzi wa miundombinu saidizi, ikiwemo vyoo na uzio.
Mwisho
Comments
Post a Comment