NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
JANDO ni kumkata mtoto au
kumfanyia tohara kwa kuondosha gozi la juu kwenye uume.
Jando au
tohara ni kitu cha lazima kwa wanaume hasa jamii ya waislamu kwani humuweka katika
hali ya usafi na usalama katika afya yake.
Pamoja na
kuwa jando/ tohara ni lazima kwa vijana wa kiume na watoto wa kiume, lakini
baadhi ya vijiji walifanya kama utamaduni maalumu, hasa pale walipoutekeleza
kwa muda maalumu na kuwakusanya pamoja huku zikiambatana na sherehe.
Na kila
sehemu walikuwa na utaratibu wao wa kuwatia watoto wao wa kiume jandoni, ambao
ulikuwa ni utamaduni maalumu wanaojiwekea.
Wanajamii
wa vijiji vya Micheweni Pemba, ni miongoni mwa watu ambao, jando walilifanya
kama utamaduni kwa kuwakusanya watoto wa kiume na kuwaweka sehemu moja, huku
kukifanyika shughuli mbali mbali za kimila zilizoambatana na sherehe baada ya
kupona kidonda.
Hamad
Mbwana Shaame mkaazi wa shehia ya Majenzi Wilaya ya Micheweni anaelezea jando
mwanzo ilikuwa kama sherehe, ingawa sasa utamaduni huo umepotea katika jamii
yao.
Walikuwa
wanasubiriwa watoto wa kiume mpaka wafikie miaka kumi na kuendelea, ndipo wazee
katika mtaa ule hushauriana siku ambayo watawatia jandoni.
"Ilikuwa
wanaliita ‘kumbi’ watu wa hapa kwetu Micheweni, hivyo walikuwa wanawakusanya
watoto angalau kumi na kuwatia kumbini kwa kusubiri kufanyiwa jando,"
anasema.
Hamad anaelezea,
walikuwa wanajengewa uwa wa makuti (boma iliyozungushwa makuti) na wanakaa humo
wiki mbili mpaka tatu, huku wazazi wa watoto hao wakitayarisha chakula cha kila
siku na kuwapelekea kumbini hapo.
Wakati
anapokwenda mzazi kupeleka chakula, anakuwa na wimbo maalumu anaoimba na wale
watoto walimo kumbini wanaitikia.
Mkaazi
huyo wa Majenzi aliuwimba wimbo huo kuwa ni... ‘cha jumbe... na watoto wanaitikia... too na kije too...’ ambapo
huurejea takribani mara tatu.
"Ilikuwa
chakula kinakusanywa, baadae mzazi mmoja ambae anahusika na wale watoto walimo
kumbini anakwenda kukipeleka," anaeleza.
Baada ya
kupona watoto wale, inapigwa ngoma inayoitwa 'unjuguu' huku wakiwa wamevishwa nguo nzuri na baadae kutolewa kila
mmoja kupelekwa kwao.
"Na
hawa vijana wa kiume na wao tulikuwa tunawaita wari kama vile vijana wa kike
kwa sababu na wao ni wapya," anahadithia.
Saada
Sheha Ali anasema, wazee zamani walikuwa wanafanya hivyo ili watoto wao
wajifunze mambo mbali mbali kwa sababu kwenye kumbi hiyo, walikuwa
wanaelimishwa na kupewa nasaha ambazo zinawasaidia katika maisha yao ya kila
siku.
Vijana
hao walikuwa wavumilivu kutokana na kuwa wanapotiwa jandoni hawakuwahi kuekewa
ganzi, hivyo yale maumivu waliyoyapata yaliwajenga ukakamavu na uvumilivu.
"Ndio
maana wazee wetu zamani wanapooa wanakaa na wake zao mpaka mmoja anakufa lakini
hawaachani, ingawa sasa hivi mtoto anajikuta yuko vizuri tu hajui uchungu, hivyo
uvumilivu umekuwa mdogo," anafahamisha.
Akitaja
vifaa ambavyo vilitumiwa kwa ajili ya kufanyiwa jando kuwa ni visu ambavyo
vilikuwa vikifuliwa na kunolewa kwa vinoo.
Aliekuwa
akiwatahiri (jando) watoto hao, ni mwanaume ambae aliitwa 'mngariba' na
walikuwa ni maalumu.
Saada
Said Kombo ambae ni mkaazi wa Micheweni anasema kumtia mtoto jandoni, wao walikuwa
wanaita ‘kukuwaza’.
Anafahamisha,
mzazi anapompeleka mwanawe kwa mngariba, humwambia kuwa...tayari mtoto wake
anataka kukuwazwa, hivyo anapangiwa muda wa kumpeleka kukatwa huku wakikusanywa
pamoja na wenzake.
"Wanakuwa
watoto wengi, hivyo anachukuliwa mmoja mmoja na kuwekwa kwenye kinu na baadae
linavunjwa dafu halafu ndio anakatwa," anaeleza.
Baada ya kumaliza
kukatwa, ananyweshwa maji ya dafu pale pale ili apate kukojoa haraka, kwani
wengine wanapokatwa hukaa mda mrefu hawajapata haja ndogo, jambo ambalo
linawaletea maumivu.
Anafafanua,
zamani walikuwa wakikatwa watu wazima sio watoto wadogo kama siku hizi, ambapo
kila mzazi alikuwa anapeleka visu na kulazwa kwenye maji kuanzia usiku mpaka
asubuhi, ndipo hutolewa kwa ajili ya kufanyiwa kazi ya kukatia.
"Tulikuwa
tunawalipa wangariba wetu, lakini kipindi hicho tuliwapa kila mzazi shilingi
mia tatu tu lakini ilikuwa ni pesa kubwa," anafafanua.
Sharifu
Massoud Hamad analielezea jando lilivyokuwa likifanyika zamani kuwa, watoto wa
kiume walikuwa wanaachwa mpaka wanakuwa wakubwa, kwani waliamini wanapokatwa
wadogo kuna baadhi ya vitu vinaweza kubakia (magozi).
Mama huyo
anahadithia kuwa, utamaduni huo umeondoka na sasa mtoto anakatwa akiwa ndani ya
siku arubaini baada ya kuzaliwa.
"Zamani
ilikuwa wanaachwa mpaka wanakuwa balekh, wanakusanywa pamoja na kufanyiwa
tohara/jando, wanajengewa uwa uliozungushwa makuti au majani ya mgomba
makavu," anahadithia mama huyo.
"Kulikuwa
na nyimbo wanaimbiwa na wao wanaitikia lakini ikiwa watanyamaza kimya chakula
kinarudishwa, kwani ilikuwa mpelekaji chakula hawezi kuingia ndani humo bila ya
kuitikiwa," anaeleza.
Anasema,
lengo la kuimbiwa nyimbo hiyo lilikuwa ni kwamba wajifunike nguo kwani walikuwa
wanakaa bila nguo, ili wapate upepo na kidonda kikauke haraka.
Sheha wa
shehia ya Majenzi Faki Kombo Hamad anasema, kulikuwa na mzee ambae kwa hapo
kijijini kwao na vijiji jirani walimtumia kwa kuwakata watoto wa kiume.
"Tulikuwa
tunawekwa pamoja vijana wapatao 20, baadae anachaguliwa mmoja anaitwa kiranja
(kiongozi), sasa huyu huchukuliwa mwanzo kwenda kukatwa huku tunamuona,"
anaeleza sheha huyo.
Walikuwa
wanawekwa kwenye kinu na baadae wanakuja kaka zao ambao wameshakuwa watu wazima
ili kuwafumba macho, hivyo hukaa hapo kumbini mpaka watakapopona ndipo
hupelekwa nyumbani kwao.
FAIDA YA
UTAMADUNI WA JANDO
Hamad
Mbwana yeye anasema, watu walijuana na kusaidiana sana kwani ikiwa mzazi mmoja
hana cha kumlisha mtoto wake, basi anachangiwa na wenzake mpaka anaondoka
kumbini.
Anasema
Sharifu Massoud, watoto hao walikuwa wanakatwa bila ya ganzi, hivyo ilisaidia
kwa wale wenye matatizo ya mishipa kuondoka moja kwa moja tofauti na sasa.
"Mtoto
ikiwa ana mshipa akichomwa sindano tu unakimbia kwa muda ule, likitoka ganzi tu
na mshipa unarudi pale pale," anafafanua.
"Mwanangu
alikuwa na mshipa, hospitali zote nilizimaliza lakini hakupona na alikuwa
akivimba, lakini niliambiwa na daktari moja kuwa nimpeleke akakatwe kwa hao
wangariba bila ya ganzi, nashkuru sana kwa sababu mpaka leo hii mshipa ule
haukuja tena, ulipotea kabisa" anahadithia mama huyo.
Muuguzi
wa kituo cha afya Maziwa Ng’ombe Wilaya ya Micheweni Aisha Omar Salum anasema,
jando ni muhimu kwani inamuepusha mwanaume na magonjwa ya kuambukiza (S.T.I)
‘’Unapofanyiwa
tohara inamzuia mwanaume kupata maradhi ya kujamiiana kutokana na kuwa uchafua
haubakii baada ya kufanya tendo la ndoa’’, anaelezea daktari huyo.
ATHARI
ZINAZOWEZA KUJITOKEZA IWAPO WATOTO HAWAKUFANYIWA TOHARA
Muuguzi
huyo anasema, athari inayojitokeza iwapo mwanaume hakufanyiwa tohara au kutiwa jandoni,
anaweza kupata maradhi ya kujamiiana, kwani anapofanya tendo la ndoa uchafu
unabaki ndani yake.
Anasema,
mwanaume anapofanyiwa tohara huwa anakatwa gozi katika sehemu ndogo ya uume
wake, hivyo ikiwa halikutolewa, yale maji maji baada ya kujamiiana yanabakia
jambo ambalo ni hatari kwa afya yake.
‘’Anaweza
hata kupata saratani kwenye tenzi dume kutokana na uchafu huo ambao hubakia
kila anapojamiiana’’, anafafanua.
NINI
KIFANYIKE?
Hamad
Mbwana anasema, mambo mengine yanapaswa kubakia, pamoja na kuwa jamii inaenda
na utandawazi lakini jando la pamoja linahitaji kurudishwa.
"Hata
kama ataitwa daktari kuwatahiri lakini wawekwe kama zamani, hii itasaidia sana
kujuana na kushirikiana," anaeleza.
Dk. Aisha
anasema, ni vyema kuendelea kufanyiwa jando watoto wakiwa wadogo ili wakikua
wajione tayari wameshafanyiwa, kwani wanapofanyiwa wakubwa inawaathiri
kisaikolojia.
‘’Kwa
vile inakuwa ni wakubwa tayari, wanajiona kama wanadhalilishwa, hivyo
wanaathirika kisaikolojia, kwa hiyo kutiwa jandoni wakiwa wadogo ’’
anafahamisha.
MWISHO.

.jpg)
Comments
Post a Comment